Hatimaye kile kilichokuwa kumejificha sasa kimewekwa wazi kwamba Kiongozi mmoja wa ngazi ya juu katika Baraza la vijana CHADEMA-BAVICHA ndiye yuko katika harakati za kumchafua Kiongozi wa upinzani nchini Dr Wilbroad Slaa na ameapa kumuangamiza kisiasa kiongozi huyo kipenzi cha watanzania.

Taarifa za uhakika zilizoibuliwa na gazeti la Tanzania Daima Jumapili zinadai mkakati huo uliopangwa kwa ustadi mkubwa ulianza kwa Katibu wa Itikadi na uenezi wa CCM Nape Nauye kuhoji sababu za Dr Slaa kumiliki kadi ya CCM huku akiwa kiongozi wa upinzani.

Baada ya tamko la Nape kundi hilo linaloongozwa na kiongozi huyo wa BAVICHA lilipokea mamilioni ya fedha kutoka kwa wanamkakati hao na kutakiwa kutembea nchi nzima kushinikiza Dr Slaa afukuzwe CHADEMA.

Mkakati wa kwanza ulianza hivi majuzi kwa mtu anayejiita mjumbe wa mkutano mkuu wa CHADEMA Eddo Mwamalala kuitisha mkutano na waandishi Dar na kutaka Dr Slaa atimuliwe mara moja kwa kitendo chake cha kuendelea kumiliki kadi ya CCM. Kundi hilo litaendelea na ziara hizo wiki ijayo katika mikoa kadhaa.

Taarifa zinadai Dr Slaa amekuwa mwiba mchungu kwa chama tawala na chama hicho kiko hatarini kuondolewa madarakani. Inadaiwa mipango mbalimbali imepangwa kuhujumu CHADEMA na mkakati wa kwanza ni kumdhoofisha Dr Slaa.

Ingawa gazeti hilo halijamtaja kiongozi huyo wa BAVICHA lakini ni kwa muda mrefu sasa Makamu Mwenyekiti wa BAVICHA Juliana Shonza amekuwa akihusishwa na makundi yanayomhujumu Mwenyekiti wa BAVICHA John Heche.