Advertise with Us

Advertise with Us

DHall

DHall

Pages

December 2, 2012

-§- Serikali yatumia "Bilioni 40" kuendesha kesi ya "DOWANS"!


 MBUNGE wa Ubungo (CHADEMA), John Mnyika ametoboa siri kuhusu kesi ya Dowans akisema kuwa serikali imetumia dola za Kimarekani milioni 29, sawa na zaidi ya sh bilioni 40 (sh bil. 45.7) kwa ajili ya uendeshaji wake.
Kesi hiyo ya kupinga kulipa faini ya dola milioni 65 zinazodaiwa na kampuni hiyo, tayari imekatiwa rufaa na TANESCO na Desemba 5 mwaka huu itaanza kusikilizwa katika Mahakama ya Rufaa Tanzania.
Mnyika alitoboa siri hiyo juzi jijini Mwanza, wakati alipokuwa akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni ya Movement for Change (M4C), ya chama hicho Kanda ya Ziwa, iliyofanyika Hoteli ya Gold Crest kisha kufanikiwa kupata jumla ya sh milioni 29.354. Ilihudhuriwa na wabunge, madiwani na viongozi mbalimbali wa CHADEMA.
Mnyika ambaye pia ni Mkurugenzi wa Masuala ya Habari na Uenezi wa CHADEMA taifa, alibainisha kuwa Serikali ya Tanzania imeonekana kuchezea fedha za walipa kodi, kwani pamoja na kutumia fedha hizo zote katika kuendeshea kesi ya Dowans lakini bado haijamalizika.
“Dowans wanaidai serikali yetu dola za Kimarekani milioni 65. Na katika uendeshaji wa kesi hii Tanzania imetumia dola milioni 29, sawa na zaidi ya sh bilioni 40…na kesi bado inaendelea, hii ni moja ya udhaifu wa serikali,” alisema Mnyika huku akishangiliwa.
Mbali na hilo, Mnyika pia aliwageukia vigogo wanaodaiwa kuficha mamilioni ya fedha nchini Uswisi akisema kuwa baadhi yao ni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Alisema watuhumiwa hao wa ufisadi walihongwa mamilioni hayo ya fedha na baadhi ya wawekezaji wanaoingia Tanzania kufanya utafiti wa uchimbaji madini na mafuta, na kwamba wanafahamu idadi ya fedha hizo na wamiliki wake.
Katika hotuba yake, Mnyika aliyekuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo wa M4C, ambaye pia aliambatana na mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA taifa, Godbless Lema, alisema kwamba vigogo hao wa CCM wamehongwa fedha nyingi na baadhi ya wawekezaji wanaomiliki makampuni hayo ya utafiti wa mafuta na madini.
“Ushahidi upo, mamilioni waliyoficha Uswisi wamehongwa na baadhi ya matajiri wenye makampuni yanayofanya utafiti wa kuchimba madini na mafuta hapa nchini kwetu Tanzania. Itafika siku tutawataja kwa majina,” alisema mbunge huyo wa Ubungo, ambaye hakufafanua zaidi ya hapo.
Aliitaka pia Serikali ya CCM chini ya Rais Jakaya Kikwete kuacha kuziba pamba masikioni katika hilo, bali ifanye uchunguzi wake wa haraka kisha iwakamate na kuwafungulia kesi mahakamani watuhumiwa wote wa ufisadi huo wa kutisha.
Pamoja na hilo, Mnyika alisisitiza kuwa Rais Kikwete ni kiongozi dhaifu, kwani ameshindwa kuwawajibisha mawaziri na watendaji wake wanaoonekana kushindwa kutekeleza vema majukumu yao katika kuwatumikia Watanzania kama walivyoapa.
Alisema inashangaza Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kutaka mawaziri wahojiwe na kujieleza kwenye vikao vya chama pale wanapoonekana kushindwa kazi, na kuhoji sababu za Rais Kikwete kushindwa kuwawajibisha viongozi na watendaji wake hao hadi kazi hiyo ifanywe na chama.

Kufuatia hali hiyo, Mnyika aliwasihi Watanzania wote kuunganisha nguvu ya pamoja na CHADEMA ili kuusaka ukombozi wa nchi hii ifikapo mwaka 2015 kwa kuiondoa madarakani CCM.
Katika uzinduzi huo wa M4C, Mnyika pamoja na mbunge wa Musoma mjini mkoani Mara, Vincent Nyerere walichangia kiasi cha sh milioni mbili kwa kila mmoja, huku Mbunge wa Nyamagana, Ezekiel Wenje na Lema kila mmoja akichangia sh milioni moja.
Baadhi ya wajumbe wengine waliochangia na fedha zao kwenye mabano ni Meya wa Musoma, Alex Kisurura (sh milioni moja), Naibu Meya wa Musoma, James Bwire (sh 800,000), na mbunge wa Ilemela jijini Mwanza, Highness Kiwia ambaye alichangia sh milioni moja.

Chanzo: Tanzania daima

No comments:

Post a Comment