Advertise with Us

Advertise with Us

DHall

DHall

Pages

November 1, 2012

-§- Takukuru yamnasa Mbunge mwingine wa CCM kwa tuhuma za rushwa!

 Mbunge wa Ilala-Mussa Hassan Zungu

WINGU la rushwa limeendelea kutanda katika Chama Cha Mapinduzi [CCM], na sasa Mbunge wake wa Ilala, Mussa Zungu, anashilikiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa [TAKUKURU], akituhumiwa kutoa rushwa kwa baadhi ya wajumbe wa Jumuiya ya Wazazi.

Zungu ambaye anakuwa mbunge wa pili wa CCM kunaswa na TAKUKURU kwa tuhuma za rushwa, anashikiliwa pamoja na wajumbe wawili wa jumuiya hiyo.
Mbunge huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bunge, alikuwa akigombea nafasi ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho [NEC] kupitia Jumuiya ya Wazazi Tanzania Bara na alinaswa juzi sambamba na Dk. Damas Mukasa na Fatuma Kasenga.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma, Yunis Munisi, alisema Zungu alikamatwa Oktoba 30, mwaka huu, siku moja kabla ya uchaguzi huo.

Akielezea mazingira ya kukamatwa kwao, alisema Zungu alikamatwa akiwa na wapambe wake wanne akitoa rushwa kwa wajumbe ili wampigie kura.
Kuhusu Dk. Mukasa ambaye alikuwa akigombea nafasi ya ujumbe wa Baraza Kuu la Wazazi Taifa na mjumbe wa Mkutano Mkuu CCM Taifa, Munisi alisema alikamatwa Oktoba 8, mwaka huu, nje ya Ukumbi wa Kilimani mjini hapa kwa kosa la kutoa rushwa kwa wajumbe ili wampigie kura.
Pamoja na hilo, wajumbe wengine wawili nao wanashikiliwa na TAKUKURU kwa kosa la kupokea rushwa kutoka kwa Dk. Mukasa ili wamchague.
Mgombea mwingine aliyekamatwa, Fatuma, ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Mbeya na Mkutano Mkuu Wazazi Taifa, alikamatwa saa tisa usiku wa kuamkia jana akiwa analipia baadhi ya wajumbe wa mkutano vyakula na vinywaji.
“Inaaminika kwamba huo ulikuwa ni ushawishi ili wajumbe wamchague...alikamatwa katika nyumba ya wageni ya Kitoli iliyopo eneo la Iringa Road mjini Dodoma,” alisema Munisi.
Alisema TAKUKURU imekuwa ikifuatilia taarifa za vitendo vya rushwa tangu kuanza kwa chaguzi za ndani za CCM kuanzia ngazi za chini hadi taifa kwa lengo la kuzuia na kupambana na vitendo hivyo.
Munisi alisema hatua hiyo imefanikiwa kuzuia vitendo vingi ambavyo vilitaka kutendeka baada ya kupata mipango hiyo na kuitibua kabla ya kufanikiwa.
Hata hivyo, alisema changamoto kubwa waliyokumbana nayo ni kitendo cha wajumbe kushirikiana na wagombea na wapambe wao katika vitendo vya rushwa, na hivyo kuwa shida kufanya ushirikiano.
Alisema changamoto nyingine inatokana na wananchi kudai wameona vitendo vya rushwa vikitendeka, lakini hawachukui hatua zozote za kutoa taarifa TAKUKURU.

Kuhusu tuhuma zinazowakabili akina Zungu na wenzake, alisema uchunguzi unaendelea.

Habari na Danson Kaijage

No comments:

Post a Comment