Advertise with Us

Advertise with Us

DHall

DHall

Pages

October 12, 2013

Tanzania- Nchi tajiri, Wananchi masikini!


Dhahabu

Tanzanite

Almasi

  Mlima Kilimanjaro ambao ni kivutio kikubwa kwa watalii

Mbuga na hifadhi mbalimbali za Wanyama ambazo ni kivutio kikubwa kwa watalii.

Wakati taarifa za ukuaji wa uchumi zikionyesha uchumi wa Tanzania unakua kwa asilimia saba kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita, bado mamilioni ya Watanzania wanaishi katika lindi la umaskini. Pamoja na ukuaji huu, asilimia 70 ya Watanzania wanaishi chini ya dola moja kwa siku, ambayo ni sawa na Sh 1,600.
Ni kweli kuwa Tanzania ni tajiri, lakini watu wake ni maskini! Swali hili la kwa nini Watanzania ni masikini linaulizwa na wengi, lakini jibu la uhakika halijapatikana. 
Nchi zinazotajwa leo kuwa tajiri kama Singapore, Korea Kusini, Malaysia na Taiwan zilikuwa pamoja na Tanzania katika fungu la nchi maskini sana duniani wakati tunapata uhuru mwaka 1961.
Nchi nilizozitaja hazina rasilimali nyingi kama Tanzania lakini zimetuacha tukiogelea katika lindi la umaskini wa kutisha licha ya kuwa na madini, gesi na rasilimali za mali asili na ardhi kubwa.
Utajiri wa maliasili ambao Mungu ameijalia Tanzania huwashtua wageni wengi wanaokuja kuitembelea na wengi wanashindwa kuelewa ni kwa nini bado tunaendelea kuwa maskini.
Siku moja nikiwa safarini kuelekea mkoani Arusha kikazi, nilikaa kwenye viti vinavyoambatana kwenye basi nikiwa sambamba na raia mmoja wa China, aliyejitambulisha kwangu kwa jina moja la Xia.
Kipindi chote cha safari tulikuwa hatuzungumzi, japokuwa nilitaka kumdodosa mambo mawili matatu. Nilisita kumuuliza chochote kwa kuhofia tusingeelewana kwenye mawasiliano, nikiamini kuwa lugha anayoijua ni Kichina tu.
Tulipokaribia kufika Wilaya ya Same, alinipa kamera yake na kuniomba nimsaidie kuchukua picha ya safu ya milima ya Upare, ambayo tulikuwa tukiipita kwa sababu nilikuwa nimekaa kiti cha dirishani. Niliifanya kazi hiyo kwa ufanisi mkubwa, jambo ambalo lilimfurahisha na urafiki ulianzia hapo.
Nilibaini kuwa anaweza kuongea lugha ya Kiswahili na Kiingereza kwa shida baada ya kunishukuru kwa kumpigia picha nzuri. 
Tulianza kuzungumza na katika mazungumzo yetu alinieleza kuwa amekuwa hapa nchini kwa zaidi ya mwaka na nusu. Lengo lake la kuwa nchini ni kuangalia fursa za uwekezaji katika sekta ya madini.
Alisema ameshatembeleza zaidi ya mikoa 15 na wilaya zaidi ya 40 akiangalia fursa za uwekezaji kwenye madini. Kwamba katika nchi za Afrika, mbali na Tanzania, alishatembelea nchi nyingine nane, lakini baada ya kufika Tanzania hakuona sababu ya kuendelea na safari katika nchi nyingine kutokana na fursa za uwekezaji alizoziona.
Mchina huyo alishangaa kwa nini Tanzania ni maskini wakati ina kila kitu cha kuiwezesha kuwa moja ya mataifa tajiri duniani na alinidokezea kwa sauti ya chini kuwa katika tembeatembea yake amekutana na raia wa kigeni wengi wanaojihusisha na biashara ya madini, bila kuwa na vibali vya kufanya kazi hapa nchini.
Alieleza kushangazwa na hali ya baadhi ya vijiji vyenye utajiri wa madini, huku wakazi wake wakiishi katika hali ya umaskini mkubwa wakati shughuli za uchimbaji zikifanyika bila usimamizi wowote.
Alichoniambia kwa sauti kubwa ni kwamba usimamizi katika sekta ya madini bado siyo mzuri, jambo ambalo linawapa mwanya wageni kunufaika zaidi.
Siyo jambo la kubishana kuwa ni kweli usimamizi wa uchimbaji madini sehemu nyingi nchini siyo wa kuridhisha, hivyo kampuni nyingi za kigeni zinaneemeka na utajiri wetu kuliko wananchi. 
Serikali imeshindwa kusimamia rasilimali za taifa. Ili tutoke hapa tulipo, viongozi wetu na wananchi tunapaswa kukubali kuwa tumechelewa kuandaa nguvu kazi ya kusimamia na kuendesha sekta za madini na nishati na kibaya zaidi, baadhi ya wanaoteuliwa kusimamia sekta ya madini siyo waaminifu.
Itakumbukwa kuwa, aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Augustine Mrema, alipata kueleza kuwa alikamata dhahabu ya mabilioni ya shilingi katika Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam ikisafirishwa kwa magendo kwenda nje ya nchi na mara nyingi tumesikia mchanga wa madini unapelekwa nje ya nchi, huku Watanzania wakiwa hawana la kufanya.
Mara kadhaa pia tumesikia makontena yanakamatwa nje ya nchi yakiwa na nyara za serikali. Ni jambo la kushangaza kuwa nyara hizo husafirishwa ndani ya nchi na kupita hadi zinapovushwa huku kukiwa na ulinzi kwenye mipaka yetu.
Hatujawahi kusikia uchunguzi wa kina uliofanyika na kubaini ni kwa namna gani nyara za serikali zinachukuliwa kutoka porini na kusafirishwa nje ya nchi, pamoja na kuupata mtandao mzima na kuuchukulia hatua za kisheria.
Tanzania imeendelea kuwa shamba la bibi ambalo mjanja yeyote anaweza kuja kuvuna na kuondoka pasipo kubughudhiwa. Ni jambo la kusikitisha kuwa katika kazi yangu hii ya uandishi wa habari nimeshashuhudia polisi wakishirikiana na wahalifu kufanikisha vitendo vya kuhujumu rasilimali za nchi.
Makampuni mengi ya kigeni yanaendelea kuonyesha nia ya kuwekeza kwenye gesi pamoja na uranium. Lakini yote yanataka kupewa mazingira mazuri ya uwekezaji (favourable investment condition) ili yaweze kuleta mitaji yao hapa nchini. 
Yapo malalamiko kuwa makampuni makubwa ni vinara wa kukwepa kodi, lakini serikali imeshindwa kuyashughulikia. Watu wa kawaida wenye vipato vidogo na vya kati, wakiwamo wafanyakazi ndio wanaolipa kodi kwa kuwa imeambatanishwa kwenye bidhaa wanazonunua na kwenye makato ya mishahara yao.
Ukwepaji kodi nchini hufanywa na makampuni makubwa kwa njia mbalimbali, ikiwamo kudanganya thamani ya mali zao, bidhaa na faida wanazopata ili mamlaka husika ziyatoze kodi ndogo.
Inakadiriwa kuwa, udanganyifu unaofanywa na makampuni ya madini unaifanya nchi ipoteze mapato yanayofikia dola za Kimarekani milioni moja kwa mwaka, sawa na Sh 1.6 trilioni ambayo ni sawa na bajeti ya miaka mitano ya Wizara ya Kilimo, ambayo ni Sh bilioni 200 kwa mwaka wa fedha 2012/2013.
Hii ndiyo Tanzania niliyoitazama leo, nchi tajiri, lakini watu wake maskini.

No comments:

Post a Comment