Advertise with Us

Advertise with Us

DHall

DHall

Pages

October 11, 2013

Pinda afuta agizo la Magufuli la wamiliki kutozwa 5% kwa kila gari litakalozidisha uzito!

 Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli na Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. mizengo Pinda (Picha kutoka Maktaba)

 Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. mizengo Pinda

Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda jana amefuta agizo lililotolewa na Waziri wa Ujenzi, John Magufuli la kuwataka wamiliki wa magari makubwa ya mizigo, kutozwa asilimia tano kwa kila gari litakalozidisha uzito na kuagiza kurudiwa kwa utaratibu wa zamani wa msamaha wa asilimia tano ya tozo hiyo.
Pinda pia ametoa muda wa mwezi mmoja kwa Wizara ya Ujenzi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Uchukuzi na Ofisi ya Waziri Mkuu kukutana na Chama cha Wamiliki wa Mabasi (Taboa),Chama cha Wamiliki wa
Malori (Tatoa) ili kukubaliana kwa pamoja kuhusu tozo hiyo. Agizo hilo la Magufuli alilolitoa takribani siku nne zilizopita, liliathiri kasi ya upakuaji wa mizigo katika bandari ya Dar es Salaam kutokana na mgomo huo wa malori.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Pinda alisema, katika mazingira yaliyopo sasa, ushirikiano kati ya Serikali na wadau unahitajika. “Ni lazima wadau washirikishwe ili kusiwe na malalamiko na mambo yaende vizuri,” alishauri Pinda.
Alisema, awali utaratibu uliokuwa unatumika ulipewa baraka na aliyekuwa Waziri wa Miundombinu (sasa Ujenzi), Basil Mramba ambaye baada ya wadau wa usafirishaji kulalamika kuhusu ubovu wa barabara na mizani, alitoa unafuu wa kupunguza asilimia tano ya uzito utakaosomwa katika mizani (utakaozidi).
“Lengo lake ilikuwa ni kufidia matatizo ya upungufu wa mizani kutoweza kupima kwa usahihi uzito wa magari yanayopimwa katika vituo mbalimbali vya mizani nchini, lakini hivi sasa mizani yetu ni mizuri na ya kisasa,” alisema na kuongeza:
“Lakini ikumbukwe kuwa agizo hilo lilikuwa kinyume na Sheria ya Usalama Barabarani sura ya 168 toleo la 2002 na kanuni zake za mwaka 2001, ambayo inazuia malori kuzidisha uzito. Mramba aliamua vile ili kumaliza hali iliyokuwa imejitokeza wakati akiwa Wizara ya Miundombinu,” aliongeza Pinda. Alisema kati ya kanuni hizo, kanuni ya 7(3) inatoa sharti la kama lori likibainika kuzidisha mzigo,sharti ni ama kupanga upya mzigo ili kupunguza uzito,kuushusha mzigo uliozidi au kupigwa faini mara nne ya faini ya kawaida. Pinda alisema baada ya kuibuka kwa mgomo huo alikutana na wadau wa usafirishaji na mawaziri wa wizara zenye dhamana na ujenzi na usafirishaji, kubaini kuwa kulikuwa na ulazima wa wizara hizo kukutana na wadau ili wakubaliane.
Bandari walia na mgomo
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA),imeeleza kuwa wananchi ndiyo watakaoumia kwa kulazimika kulipa hasara iliyotokana na mgomo huo.
Kaimu Meneja Mawasiliano wa Bandari hiyo, Janeth Ruzangi alisema hali hiyo itatokana na wafanyabiashara kulazimika kupandisha bei ya bidhaa mbalimbali zilizokwama kwa siku kadhaa bandarini hapo ili kufidia gharama walizotozwa na wamiliki wa meli.

No comments:

Post a Comment