Advertise with Us

Advertise with Us

DHall

DHall

Pages

July 10, 2014

Huyu ndiye waziri jangili!!


Apachikwa majina ya utani, buibui au pweza..

Ni kwa umahiri wake kuunganisha majangili..


WAZIRI aliyeukwaa wadhifa huo katika mabadiliko ya mwisho ya Baraza la Mawaziri yaliyofanyika mapema mwaka huu, akiongoza wizara nyeti, amebainika kuratibu mtandao wa ujangili wenye mizizi yake wilayani Manyoni na maeneo mengine mkoani Singida, vyanzo vya uhakika vya habari vimeeleza.
Waziri huyo (jina linahifadhiwa kwa sasa) amekuwa na mawakala maalumu katika maeneo ya karibu na mapori kunakoendeshwa ujangili na mara kwa mara, hufika wilayani Manyoni kuhakiki ufanisi wa mtandao wake huo wa ujangili, huku gazeti hili likielezwa kwamba, taarifa zake ziko ‘mikononi’ mwa vyombo muhimu vya dola nchini.
Kutoka wilayani Manyoni, mkoani Singida, taarifa za ‘kiintelijensia’ zinafichua kwamba mtandao wa waziri huyo unaongozwa na mfanyabiashara (jina linahifadhiwa) wa maduka ya vifaa. Mfanyabiashara huyo ni mkazi wa kitongoji cha Mnyang’ombe mjini Manyoni na kazi zake hizo ndani ya mtandao wa ujangili huzifanya hadi mkoani Tabora.
Inadaiwa kwamba ukaribu kati ya mfanyabiashara huyo na waziri husika umejijengea nguvu zaidi kutokana na umakini wake katika kufanikisha matukio ya ujangili.
Taarifa zinabainisha kwamba mfanyabiashara huyo amekuwa na vijana maalumu ambao kazi yao ni kukusanya pembe za ndovu kutoka katika maeneo ya Itigi, Ilangali lakini katika kituo cha Manyoni, mfanyabiashara huyo hufanya kazi hiyo yeye binafsi.
Vijana hao (majina yanahifadhiwa pamoja namba zao za simu), mmoja anaishi Manyoni akimiliki namba tatu za mtandao wa aina mmoja wa simu za mkononi, mwenzake mwingine ni mwenyeji katika vijiji vinavyopakana na Pori la Akiba Rungwa, maeneo ya Kizigo. Kijana huyo wa Kizigo ndiye mnunuzi wa meno yote ya tembo yanayopatikana maeneo hayo kwa niaba ya mtandao huo.
Mbali na vijana hao wawili, yupo kijana mwingine (jina linahifadhiwa kwa sasa), huyu ni mkazi wa kijiji cha Ilangali, naye akiwa anamiliki namba tatu tofauti za simu za mtandao mmoja wa mawasiliano ya simu za mkononi. Kazi kubwa ya kijana huyu katika mgawanyo wa majukumu ya kijangili ni kuhifadhi silaha sambamba na kununua meno ya tembo kwa ‘wadau’ hapo kijiji cha Ilangali na baada ya kununua meno hayo, mfanyabiashara wa Manyoni hufika kuyachukua.
Mbinu za usafirishaji
Baada ya kazi ya ununuzi na ukusanyaji kukamilika, meno ya tembo yaliyopatikana, husafirishwa kwa njia ya reli ya kati chini ya usimamizi wa mfanyakazi mmoja wa Shirika la Reli Tanzania (jina linahifadhiwa) mwenye makazi yake mjini Morogoro.
Mfanyakazi huyo husimamia usafirishaji wa meno hayo kutoka Tabora hadi Itigi ambako hapo hupokelewa na mfanyabiashara (wa Manyoni) ambaye huyahifadhi hapo Manyoni.
Yakiwa hapo Manyoni, meno hayo huhifadhiwa kwa mmiliki wa mojawapo ya hoteli kubwa na maarufu mjini Manyoni, mwenye asili ya mikoa ya kanda ya kaskazini, ambaye yeye huwasiliana na waziri kwa ajili ya maelekezo zaidi juu ya namna ya kusafirisha meno hayo.
Taarifa za kiuchunguzi zinazidi kubainisha kwamba mara nyingi, waziri husika hufika hapo Manyoni kwa ajili ya kuchukua “mzigo” na kila anapokwenda huongozana na mwanamke mmoja, mwenye lafudhi ya watu kutoka mikoa ya kanda ya kaskazini (jina linahifadhiwa).
Mwanamke huyo ndiye hutumiwa kusafirisha meno hayo yaliyokusanywa yakiwamo ya kutoka ‘kituo’ chao cha Puma, mkoani Singida, ili hatimaye kuyafikisha wanakokubaliana yafike.
Waziri huyo anapokuwa Manyoni amekuwa na kawaida ya kuwakusanya washirika wake katika mtandao huo na wote hupata malazi yao katika moja ya hoteli kubwa na maarufu hapo Manyoni.
Wakiwa hapo Manyoni na bosi (waziri) genge hilo la kijangili hujiimarisha kiulinzi kwa kuweka watu wa kulinda hoteli husika na hata kudadisi wageni wengine wanaofika hotelini hapo.
Katika maeneo ya Singinda, mjini Puma, yupo kijana maalumu anayetumiwa na waziri huyo ambaye anatajwa kuwa na undugu wa namna fulani na mteule huyo wa Rais Kikwete. Kijana huyu hutumia namba za mitandao miwili tofauti ya simu za mkononi.
Huyu kazi yake kubwa ni kuwaunganisha wawindaji (wenyewe majangili huita wapigaji) na wakati mwingine hutokea waziri ndiye anayekusanya mzigo. Wakati uchunguzi huu ulipokuwa ukifanyika, kijana huyo alikuwa na meno ya tembo yaliyokuwa yamehifadhiwa eneo la Tinde, mkoani Shinyanga. Hata hivyo, uaminifu wa kijana huyo si mkubwa kwa sababu uchunguzi wetu umebaini wakati mwingine ‘huchota’ mzigo kiasi fulani na kuuza kinyemela bila mtandao kujua.
Kijana huyo, kati ya kazi alizowahi kufanya ni kuwaunganisha baadhi ya vijana na mwindaji kutoka Wilaya ya Igunga (jina na mawasiliano yake yanahifadhiwa). Mwindaji huyo wa Igunga anamiliki bunduki aina ya Rifle (namba inahifadhiwa) na wakati uchunguzi wa gazeti hili ukifanyika, alikuwa na vipande sita vya meno ya tembo ambavyo ni sawa na meno matatu.
Kwa wakati huo tukifanya uchunguzi, waziri husika alitoa maelekezo vijana wake wasimamishe shughuli zao kwa muda.
Huko wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, Waziri husika anashirikiana na mtu (jina linahifadhiwa) ambaye anafanya biashara ya ng’ombe kama kinga ya kuficha shughuli zake za ujangili. Mtu huyu ni mnunuzi wa meno ya tembo na hukusanya meno yanayotoka katika mapori ya Moyowosi, Kigosi, Burigi, Biharamulo na Kimisi.
Hivi karibuni, mtu huyo amekuwa akikusanya meno ya tembo yanayotoka Moyowosi na amekuwa na wadau wake ambao ni watumishi wa serikali katika mapori ya Burigi na Biharamulo. Mtu huyo amenunuliwa na waziri husika gari aina ya Rav4, kwa ajili ya kukusanya meno ya tembo maeneo ya vijiji vinavyozunguka mapori hayo.
Katika maeneo ya Ilongelo na Ngamo, mkoani Singida, huko waziri husika anaendesha mtandao wake wa ujangili kwa kushirikiana na tajiri mmoja, mwenye asili ya Mkoa wa Simiyu ambaye naye anao mtandao mkubwa unaowahusisha vigogo kadhaa, akiwamo mmoja wa wabunge aliyepata kupigia kelele kuhusu ufisadi bungeni, zikiwamo fedha za akaunti za Uswisi, mbunge huyu ni mwenyeji wa kanda ya ziwa na ni kijana kwa umri.
Taarifa za kiuchunguzi zinabainisha kwamba meno ya tembo yanayokusanywa maeneo ya Singida, Kahama na Meatu hufikishwa katika kijiji cha Ngamo ambako waziri husika akiwa na mwanamke mmoja mkazi wa moja ya mikoa ya kaskazini ambaye ndiye mwenye jukumu la kusafirisha meno hayo.
Mtandao wa waziri huyo umejipanua zaidi katika operesheni za kijangili, ukihusisha Wilaya ya Babati, mkoani Manyara. Huko Babati, katika kijiji cha Mayoka, kuna tawi la ujangili la waziri huyo.
Msimamizi wa shughuli za kijangili eneo hilo ni mtu (jina linahifadhiwa) ambaye mara kwa mara huwapo Dodoma kila waziri husika anapokuwa huko kwa shughuli za Bunge. Huyu mtu ndiye husimamia ukusanyaji meno ya tembo kutoka maeneo ya Magugu na Mayoka, wakipata meno hayo kutoka katika Hifadhi ya Taifa Tarangire na ushoroba wa Tarangire – Manyara.
Kutokana na umahiri wa kuunganisha mitandao wa kijangili nchi nzima, waziri huyo kwa baadhi ya watu analinganishwa na pweza au buibui kutokana na kunasa na kuunda mtandao mpana. 

Chanzo Gazeti la Raia Mwema


No comments:

Post a Comment