Advertise with Us

Advertise with Us

DHall

DHall

Pages

November 2, 2013

Ushauri wa bure kwa CHADEMA kuelekea 2014-2015!


Kanda ya MASHARIKI Dar es Salaam na Pwani ni miongoni mwa Kanda kumi zilizoundwa ili kukidhi mkakati wa M4C na Chaguzi ndani ya Chama, aidha mfumo huu unatumika kama mwanzo wa utekelezaji wa mapendekezo ya sera ya majimbo ambayo CHADEMA imekuwa ikipendekeza kwenye Ilani yake ya Uchaguzi kipindi cha Kampeni 2010, lengo ikiwa kupunguza Madaraka ya Rais na ukubwa wa Serikali  ili kuharakisha maendeleo kwa kutumia rasilimali za maeneo husika. Kanda zingine ni KUSINI ambayo ni Lindi na Mtwara, KASKAZINI Kilimanjaro, Arusha na Manyara, KANDA YA KATI Morogoro, Dodoma na Singida,  NYANDA ZA  JUU KUSINI Njombe, Iringa, Mbeya na Ruvuma, MAGHARIBI Rukwa, Katavi, Tabora na Kigoma, Kanda ya ZIWA MASHARIKI Shinyanga, Simiyu na Mara, ZIWA MAGHARIBI Mwanza, Geita na Kagera na kwa upande wa  ZANZIBAR Pemba na Unguja.
Kamati Kuu katika Kikao cha tarehe 09/11/2012 iliazimia kwamba, mara baada ya Muundo wa Kanda kukamilika na waratibu wa Kanda kuajiliwa, M4C inatakiwa kuongoza zoezi la Uchaguzi  wa ndani ya Chama. Uchaguzi wa Chama unatakiwa kukamilika ndani ya mwaka 2013. Mapendekezo haya yalitolewa mwanzoni mwa mwaka 2011, baada ya kubaini kwamba tunapokwenda kwenye Uchaguzi wa Chama na wakati huo huo kuna Chaguzi za Kiserikali madhalani kuchagua Wenyeviti wa Serikali ya Vijiji/Serikali ya Mtaa  karibu na Uchaguzi Mkuu inaleta mkanganyiko mkubwa ndani ya Chama kama vile kushughulikia rufani mbalimbali  za wagombea ambao kwa namna moja au nyingine hajaridhika na matokeo katika chaguzi ndani ya chama na wakati mwingine kusababisha kukosa ushindi, hivyo msisitizo ukawa Uchaguzi ndani chama unatakiwa ufanyike mapema kabla ya Chaguzi za Kiserikali bila kuathili Utaratibu wa Uchaguzi kama Katiba ya Chadema inavyoelekeza katika Sura ya Sita Ibara ya 6.3.1 (a) – (e) na Muda wa Uongozi Ibara ya 6. 3 . 2 kifungu (a) – (e)
Lakini mpaka naandika makala hii kumekuwa na sintofahamu ya muda mrefu kwa wanachama wengi na baadhi ya viongozi hasa wa Ngazi ya Misingi, Matawi na Kata kuhusu mienendo ya uendeshaji wa shughuli za chama hususani baada ya hizi kanda kuanzishwa, pia kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa Katiba ya chama tangu Uanzishwaji wa hizi Kanda, kumekuwa na Mifumo kandamizi na lazimishi bila kufuata Kanuni, Misingi, Falsafa na Itifaki za CHAMA kwa kuzingatia wajibu na nafasi ya kila Kiongozi katika eneo lake la kazi.
Kuna zoezi la CHADEMA ni MSINGI ambalo limekuwa ni Siri. Na limekuwa siri  kwa viongozi waliopo bila kujua kinachoendelea ni kitu gani ambacho ni Siri katika Ujenzi wa Chama mpaka wengine msishirikishwe. Lakini zoezi limegundulika kuwa ni maandalizi ya kuelekea CHAGUZI za ndani ya CHAMA aidha waendeshaji wa mazoezi haya wanafanya kwa interests zao yaani kujijenga na sio kujenga CHAMA ndio maana hawapiti  kwenye ofisi za Chama wala kuwaona viongozi wa Kata husika. Kwa madai kwamba  wamefundishwa wasiitumie Katiba ya chama kama mwongozo na pia wasipite kwenye Ofisi wala kuuona Uongozi uliopo isipokuwa watumie mbinu kutoka kwenye kitabu cha mafunzo na Programme za Chama kuanzisha Misingi na Brigedi Nyekundu (Kikosi cha Ulinzi) na kamwe wasiwahusishe wadau kama vile Uongozi wa Wilaya/Jimbo au Kata na anayefahamu ni Mbunge pekee na watu wachache waliohudhuria Mafunzo hayo katika Mkoa wa DODOMA,  “anayeona  zoezi hili si shirikishi mlango upo wazi anaweza kujiondoa CHADEMA” je kauli kama hizi za kuogofya ni nzuri kwenye muktadha wa afya ya Demokrasia ? 
Ukitaka kujua njia hata zilizotumika ni haramu na kufanya  zoezi lote kuwa haramu hata namna ya kuwapata watu walioenda kuchukua mafunzo, hakuna waraka wowote kwenda kwenye Majimbo/Wilaya, Kata au Matawi ambayo ndio yenye watu kutoka kwenye Misingi wala hakukua na vigezo vilivyotolewa kwa ajili Ushiriki wa Semina ya Mafunzo. Kwa mfano utaratibu huu uliokiuka Katiba ya Chama umeleta mkanganyiko mkubwa hasa katika Jimbo la Kawe. Aidha haya yote yamefanywa sio kwa bahati mbaya, ni kwa makusudi kwa sababu Jimbo la Kawe ni jimbo ambalo lilikuwa na mgogoro wa muda mrefu dhidi ya ugumu wa kuwandoa viongozi waliokula Fedha za Jimbo ( Ruzuku iliokuwa ikitolewa kila mwezi na Chama ), lakini kuna msemo usemao “usipo stahajabu ya Musa utayaona ya firahuni”,  hao mafisadi  ndio miongoni mwa waliopata nafasi ya kuhudhuria mafunzo ya CHAMA na ndio  wamekuwa wakufunzi wa CHADEMA ni MSINGI na Kamanda Mkuu wa Red Brigade katika lilelile Jimbo wanalotuhumiwa na hakuna chombo ama Kikao chochote cha Chama kilichowasafisha tangu mwaka jana hadi tarehe 6 mwezi January 2013 wakati Kamati ya Kikosi Kazi ya Jimbo kuundwa. 
Mtindo wanaoutumia ni njia ya kupigiana simu na wakati mwingine kutafuta sehemu iliojificha na endapo watabahatika kumpata mwanachama au mpenzi wa CHADEMA ambao hawajui tuhuma zao katika eneo husika wanamwapisha asitoe taarifa yoyote kwa Mwenyekiti au Katibu wake wa Msingi, Tawi au Kata katika eneo lake kwa gia ya kuwaaminisha kuwa mkakati huo wa programme ya Chadema ni MSINGI ni sawa na Usalama wa Taifa hivyo haipaswi Kiongozi wako kujua wala kuhoji.
 Ki-ukweli na ki-uhalisia zoezi linaloendelea katika Kanda ya Mashariki  Dar es Salaam na Pwani hususani katika JIMBO LA KAWE sijui hali ikoje katika Majimbo ya TEMEKE, UKONGA, ILALA, SEGEREA, KIGAMBONI, UBUNGO na KINONDONI ni zoezi tenganifu na si shirikishi isipokuwa linaleta makundi na migogoro isiyo ya lazima kati ya viongozi waliopo na vikundi vinavyoundwa bila Kamati tendaji za viongozi husika katika Kata au Tawi kwa maana ya Mtaa kushiriki. Jambo hili linaweza likaonekana dogo na kubezwa na Uongozi wa Kitaifa na wakati mwingine hoja zao zinaweza zikapuuzwa  kwa sababu mbalimbali; mfano wa kipuuzi kusema Chama hakipo kwenye eneo fulani au kazi haziendi na kufikiri mifumo kandamizi ambayo siyo shirikishi ndio bora katika Ujenzi wa Chama kuelekea 2014 na 2015 Uchaguzi wa Serikali ya Mtaa na Uchaguzi Mkuu.
Demokrasia ndio Msingi Mkuu wa kutoa haki sio tu ya kuomba Uongozi na kupigiwa kura au fursa ya kupiga kura bali pia kushirikishwa kikamilifu na kutoa mawazo pia kupata taarifa sahihi. Kwa mujibu wa nyaraka mbalimbali kuhusu Ujenzi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo ( CHADEMA ) haioneshi kuwabagua viongozi wa kada mbalimbali katika Chama, lakini hili zoezi la CHADEMA ni Msingi ambayo dhana yake inatokana  na operation za M4C zinaendeshwa kwa minajili ya kuwatenga baadhi ya viongozi ambao kwa namna moja au nyingine wameonekana wakifanya kazi za Chama bila ya kujipendekeza kwa wabunge au madiwani wao, dhana yao kubwa ikiwa ni kusimamia Falsafa, Kanuni na Misingi ya Chama, aidha wameonekana kuwa mwiba kwa watu wachache wenye maslahi binafsi na kuamua kutumia nafasi au uwezo wao kuwatenga.
Hili jambo limeshaanza kuleta mpasuko na mgogoro mkubwa, na ikiwa viongozi husika wa Kanda ya Mashariki au Makao Makuu wasipofanyia kazi maoni na ushauri wa wadau hasa viongozi linaweza kuwa janga hasa katika Kanda yetu ya Dar es Salaam na Pwani. Nini kifanyike, napendekeza kwamba hatua za haraka zifanyike kwa Wakuu wa Kanda kukutana na Kufanya Vikao vya Majadiliano na wadau ambao watakuwa viongozi wa Jimbo/Wilaya na Viongozi wote wa Kata katika kila Jimbo kwa nyakati tofauti ili kupata njia bora na nyepesi ambayo itawashirikisha viongozi wote bila kuwabagua.
Pili napendekeza pia programu zote katika Ujenzi wa Chama zihakisi mifumo yote ya Kiongozi Kikatiba kwa kufuata na kuzingatia falsafa, kanuni na itifaki za Chama.
Na mwisho ninaonya lugha za kibaguzi kutumika wakati wa kutengeneza team work, mfano kutumia  maneno kwamba, "unajua viongozi wengi ni wakukaimishwa na mamluki" lugha hizo zisitumike au kitendo cha Kiongozi au Mwanachama kusema "mimi tu na fulani ndio tulichaguliwa" iwe kwenye Ngazi ya Wilaya/Jimbo au Kata, haiwezi kuleta dhana ya  ujumla ya kupoka matumizi ya Katiba ya Chama katika shughuli za Ujenzi wa Chama; ikumbukwe kila zoezi la muundo wa Ujenzi wa Chama ikiwemo Chadema ni Msingi ni lazima izingatie mashariti ya: Muundo wa Uongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) unaanza Ngazi ya chini kabisa ambayo ndio Msingi wa CHAMA kwa mujibu wa KATIBA YA CHAMA Ibara ya 7.1.1 ikifuatiwa na Ngazi zingine Tawi Ibara ya 7.2.1 , Kata Ibara ya 7.3.1, Wilaya/ Jimbo la Uchaguzi Ibara ya 7.4.1 , Mkoa Ibara ya 7.5.1 na Ngazi ya juu kabisa ni Ngazi ya Taifa Ibara ya 7.7.1.
Athari na adha ya zoezi hili zimekwisha anza kujitokeza kwenye baadhi ya majimbo mbalimbali katika Mkoa wa Dar es Salaam inawezekana tukapuuza kama tulivyozoea kujipa matumaini ya kusadikika bila kufanya utafiti au kufika kwa wadau na kuhoji ni nini hasa kinachopingwa katika zoezi hili zuri lisilo na malipo ambalo kila Kiongozi angependa kushiriki kwa uwazi na hatimaye kutengeneza timu nzuri ili kufikia malengo ya Programu ya CHADEMA ni MISINGI kwa wakati.  Tuchukue hatua Mapema
CHADEMA TUMAINI LA WATANZANIA 
Na: Msomaji wetu

No comments:

Post a Comment