Advertise with Us

Advertise with Us

DHall

DHall

Pages

April 12, 2014

Hotuba ya Tundu Lissu iliyokatishwa kwa makusudi na TBC- Sehemu ya Kwanza!

Mjumbe wa Bunge maalum la Katiba Mhe. Tundu Lissu alipokuwa akitoa Hotuba ya Maoni ya walio wachache kutoka katika Kamati Na. 4 kabla ya Kukatiwa matangazo na Kituo cha matangazo cha TBC

MAONI YA WAJUMBE WALIO WA WACHACHE KATIKA KAMATI NAMBA NNE KUHUSU SURA YA KWANZA NA SURA YA SITA YA RASIMU YA KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

[Kanuni ya 32(4) ya Kanuni za Bunge Maalum, 2014]

UTANGULIZI

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Sura ya Kwanza na Sura ya Sita ya Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (‘Rasimu’) ndizo msingi ambao Rasimu yote imejengwa juu yao. Wakati Sura ya Kwanza inagusa suala la muundo wa Muungano katika ibara moja tu kati ya ibara tisa, Sura yote ya Sita inahusu ‘Muundo wa Jamhuri ya Muungano.’ Suala la Muungano na hasa Muundo wake limetawala mjadala wa kisiasa na kikatiba wa Tanzania kwa zaidi ya miaka thelathini. Ndio maana katika waraka wake wa siri kwa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (‘CCM’), Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa ya chama hicho imetamka kwamba “muundo wa Muungano ndiyo moyo wa Rasimu na ndiyo unaoamua ibara nyingine zikae vipi.”

Suala hili pia limetawala mchakato wa Katiba Mpya tangu ulipoanza miaka mitatu iliyopita. Kama alivyosema Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Joseph Sinde Warioba wakati wa kuwasilisha Ripoti ya Tume yake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Zanzibar tarehe 30 Disemba, 2013: “Moja ya mambo ambayo yamejadiliwa sana na kwa hisia kali tangu Rasimu ya awali ilipotolewa ... ni Muungano wa Tanzania. Jambo kubwa limekuwa juu ya muundo wa Muungano.”

Umuhimu wa suala hili unathibitishwa pia na uamuzi wa Kamati ya Uongozi ya Bunge Maalum kuelekeza kwamba Kamati zake Namba Moja hadi Kumi na Mbili zianze kujadili Sura ya Kwanza na ya Sita ya Rasimu. Haya ni maoni ya wajumbe walio wachache wa Kamati Namba Nne juu ya Sura hizi mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Mjadala wa Kamati Namba Nne kuhusu Sura za Kwanza na Sita za Rasimu unathibitisha pia umuhimu wa suala la muundo wa Muungano katika mjadala mzima wa Rasimu. Kama Taarifa ya Kamati yetu inavyoonyesha, Kamati Namba Nne imeshindwa kufanya uamuzi kuhusu suala hili katika ibara za 1 na 60 za Rasimu. Katika ibara ya 1 ya Sura ya Kwanza, wajumbe walio wengi walipata kura 22, ambayo ndiyo theluthi mbili ya kura za wajumbe wote 33 wa Tanzania Bara wa Kamati Namba Nne. Kwa upande wa Zanzibar, wajumbe walio wengi walipata kura 9 ambayo ni pungufu ya kura 13 zinazohitajika ili kufikisha idadi ya theluthi mbili ya wajumbe wote 19 wa Zanzibar.

Kwa upande wa ibara ya 60, wajumbe walio wengi walipata kura 22 za wajumbe kutoka Tanzania Bara, ambazo ni theluthi mbili ya idadi ya wajumbe wote 33 kutoka Tanzania Bara. Aidha, kwa Zanzibar, wajumbe walio wengi walipata kura 8, ambazo pia ni pungufu ya kura 13 zinazotakiwa kufikisha idadi ya theluthi mbili ya wajumbe wote 19 kutoka Zanzibar. Kwa sababu hiyo, ibara za 1 na 60 za Rasimu hazikupitishwa au kuamuliwa na Kamati Namba Nne kama inavyotakiwa na kifungu cha 26(2) cha Sheria na kanuni ya 64(1) ya Kanuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Sasa tunaomba kwa ridhaa yako, tuwasilishe hoja na sababu za maoni ya wajumbe walio wachache katika Kamati Namba Nne kuhusu Sura hizi mbili ambazo ndio ‘moyo wa Rasimu.’

SURA YA KWANZA

Sura ya Kwanza ya Rasimu inahusu ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.’ Sehemu ya Kwanza ya Sura hiyo inazungumzia ‘jina, mipaka, alama, lugha na tunu za Taifa.’ Ibara ya 1 inaitambulisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; ibara ya 2 inatangaza ‘eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania’; na ibara ya 3 inaweka utaratibu wa ‘alama na sikukuu za Taifa.’ Vile vile ibara ya 4 inaweka utaratibu wa lugha ya Taifa na lugha za alama, wakati ibara ya 5 inahusu ‘tunu za Taifa.’

Kwa upande wake, Sehemu ya Pili ya Sura ya Kwanza inaweka masharti ya ‘mamlaka ya wananchi, utii na hifadhi ya Katiba. Ibara ya 6 ya Sehemu hiyo inatoa ufafanuzi wa ‘mamlaka ya wananchi’; ibara ya 7 inafafanua uhusiano kati ya ‘watu na Serikali’; ibara ya 8 inashurutisha ‘ukuu na utii wa Katiba’; na ibara ya 9 na ya mwisho inaweka ‘hifadhi ya utawala wa Katiba.’

IBARA YA 1

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Kama maelezo yake ya pembeni (marginal note) yanavyoonyesha, ibara ya 1 inaitambulisha ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.’ Ibara ya 1(1) inatamka kwamba “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Shirikisho lenye mamlaka kamili ambayo imetokana na Muungano wa nchi mbili za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ambazo kabla ya Hati za Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964 zilikuwa nchi huru.”

Kwa upande wake, ibara ya 1(2) inafafanua kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania “ni Shirikisho la kidemokrasia linalofuata mfumo wa vyama vingi vya siasa, usawa wa binadamu, kujitegemea, utawala wa sheria, kuheshimu haki za binadamu na lisilofungamana na dini.” Mwisho, ibara ya 1(3) inatukumbusha kwamba “Hati ya Makubaliano ya Muungano ... ndio msingi mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba hii, kwa kadri itakavyorekebishwa, itakuwa ni mwendelezo wa Makubaliano hayo.”

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Wajumbe walio wachache wa Kamati Namba Nne wanapendekeza mabadiliko ya jina la nchi yetu kutoka jina la sasa la ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanzania’ kuwa jina jipya la ‘Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar.’ Aidha, wajumbe hao wanapendekeza kuacha kutajwa kwa Hati ya Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964 katika ibara ya 1(1) na (3) ya Rasimu. Badala yake, inapendekezwa kwamba Katiba hii ndiyo iwe msingi wa Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar.

Kwa mapendekezo haya, ibara ya 1(1) itasomeka kama ifuatavyo: “Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar ni Shirikisho ambalo limetokana na Muungano wa nchi mbili za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.” Kwa mantiki hiyo, ibara ya 1(2) itasomeka: “Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar ni Shirikisho la kidemokrasia linalofuata mfumo wa vyama vingi vya siasa, usawa wa binadamu, kujitegemea, utawala wa sheria, kuheshimu haki za binadamu na lisilofungamana na dini.” Aidha, ibara ya 1(3) itasomeka: “Katiba hii ndio msingi mkuu wa Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar.” Zifuatazo ni hoja na sababu za mapendekezo haya.

SHIRIKISHO AU MUUNGANO?

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Katika nusu karne ya uhai wake, nchi yetu imeitwa ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.’ Hata hivyo, katika kipindi chote hicho, Katiba na Sheria za nchi yetu hazijawahi kufafanua kwa uwazi aina au haiba ya ‘Muungano’ huu. Matokeo ya kukosekana kwa ufafanuzi huu ni kwamba katika nusu karne hiyo, kumekuwa na mjadala mkubwa wa kikatiba, kisiasa na kitaaluma kuhusu suala la kama Jamhuri ya Muungano ni dola ya muungano (a unitary state), au ni dola ya shirikisho (a federal state). Majibu ya swali hili yamekuwa na athari za moja kwa utambulisho, haki, maslahi na wajibu wa Washirika wa Muungano huo, yaani Tanganyika na Zanzibar, na hasa kwa wananchi wa nchi hizi mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Kukosekana kwa ufafanuzi wa aina ya muungano wetu haujawa suala la mijadala ya kisiasa na kikatiba peke yake, bali kumekuwa ni chanzo cha migogoro mikubwa ya kisiasa baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Migogoro hii ilianza tangu mwanzo kabisa wa Muungano wakati wa sakata la kuwa na ubalozi wa iliyokuwa Ujerumani Magharibi kwa upande wa Tanganyika na ubalozi wa iliyokuwa Ujerumani Mashariki kwa upande wa Zanzibar.

Aidha, kati ya mwaka 1964-1967 ulizuka mgogoro mkubwa kuhusiana na uwakilishi wa Zanzibar katika iliyokuwa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki na uanzishwaji wa Benki Kuu ya Tanzania; kuunganishwa kwa vyama vya ASP na TANU na kuundwa kwa CCM mwaka 1977, na katika mjadala wa marekebisho ya Katiba wa mwaka na baadae ‘kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar’ mwaka 1983/1984.

Baadae mwaka 1988 ulitokea mgogoro mkubwa uliopelekea kung’olewa madarakani kwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Maalim Seif Shariff Hamad na baadae kufukuzwa katika CCM; wakati wa harakati za kudai kura ya maoni kuhusiana na Muungano mwaka 1989/1990; wakati wa mjadala wa kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1991; wakati wa sakata la Zanzibar kujiunga na Umoja wa Nchi za Kiislamu (Organization of Islamic Countries - OIC) mwaka 1993; wakati wa mjadala wa G-55 na madai ya kuanzishwa kwa Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano mwaka 1994, na Uchaguzi Mkuu wa 1995 huko Zanzibar.

Milenia Mpya ilipoanza ilianza na mgogoro kuhusu matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 uliopelekea mauaji ya Januari 2001 huko Zanzibar. Mgogoro huo ulifuatiwa na mgogoro juu ya suala la ugunduzi wa mafuta visiwani Zanzibar; harakati za kuanzishwa kwa Shirikisho la Afrika Mashariki na hivi karibuni kupitishwa kwa Marekebisho ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar ya 1984 mwaka 2010.

Zaidi ya migogoro hii, Serikali ya Jamhuri ya Muungano na ile ya Mapinduzi zanzibar zimeunda tume na kamati nyingi ili kupata dawa ya ‘Kero za Muungano.’ Serikali ya Mapinduzi Zanzibar peke yake imeunda tume na kamati 13 katika kipindi kifupi cha miaka 12 kuanzia mwaka 1992 hadi 2004; wakati Serikali ya Jamhuri ya Muungano imeunda tume na kamati nane kushughulikia matatizo hayo. Licha ya jitihada zote hizo, ‘Kero za Muungano’ hazijapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Tangu miaka ya mwanzo ya Jamhuri ya Muungano kulikuwa na mitazamo miwili tofauti miongoni mwa waasisi na viongozi wakuu wa Jamhuri ya Muungano. Mitazamo hii tofauti inathibitishwa na kauli ya Mwalimu Julius K. Nyerere, mwasisi na Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano katika Mkutano Maalum wa Halmashauri Kuu ya CCM uliofanyika Dodoma kati ya tarehe 24-30 Januari, 1984: “... Muungano wa Tanzania ukiangalia kwa jicho la Zanzibar ni wa shirikisho lakini ukiangalia kutoka upande wa Tanzania Bara ni Serikali moja.”

Mwalimu alikuwa akimjibu Makamu Mwenyekiti wa CCM, Makamu wa Rais na Rais wa Zanzibar wakati huo, Alhaj Aboud Jumbe Mwinyi aliyesema kwamba Muungano wa Tanzania umeunda Shirikisho (Federation) na sio Serikali moja (Unitary State). Mjadala huo ulipelekea ‘kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar’ na kung’olewa madarakani kwa Jumbe, Waziri Kiongozi wake Ramadhani Haji Faki na Mwanasheria Mkuu Bashir Kwaw Swanzy. Aidha, Wolfgang Dourado, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar wakati Hati ya Muungano inasainiwa, na mkosoaji mkubwa wa Muungano huo, aliwekwa kizuizini kwa kuunga mkono hoja za Rais Aboud Jumbe.

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Miaka kumi baada ya ‘kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar’ Jamhuri ya Muungano ilikabiliwa na mgogoro mwingine tena wa kikatiba na kisiasa, mara hii ukitokana na Zanzibar kujiunga na OIC. Kitendo hicho kilizua tafrani kubwa ya kisiasa pale Bunge la Jamhuri ya Muungano lilipopitisha Azimio la kutaka kuanzishwa kwa Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano mwezi Agosti, 1993. Azimio hilo liliungwa mkono na Serikali ya Jamhuri ya Muungano, kitendo kilichomfanya Mwalimu Nyerere kuingilia kati na kuzima jaribio hilo.

Baadae Mwalimu aliandika kitabu alichokiita Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania kilichochapishwa mwaka 1994. Katika kitabu chake, Mwalimu anarejea mkanganyiko ambao umekuwepo kuhusu aina ya Muungano huu kwa maneno yafuatayo:

“Nchi zinapoungana na kuwa nchi moja mifumo ya kawaida ya miundo ya Katiba ni miwili: Kwa mfumo wa kwanza kila nchi itafuta serikali yake, na nchi mpya inayozaliwa itakuwa ni nchi moja yenye serikali moja. Katika mfumo wa pili kila nchi itajivua madaraka fulani ambayo yatashikwa na serikali ya shirikisho, na itakuwa na serikali ambayo itakuwa na mamlaka juu ya mambo yaliyobaki. Mambo yatakayoshikwa na serikali ya shirikisho ni yale ambayo yakibaki katika mamlaka ya nchi zilizoungana, basi kwa kweli nchi hizo zitakuwa hazikuungana kuwa nchi moja, bali zinaendelea kuwa nchi mbili zenye ushirikiano mkubwa katika mambo fulani fulani.... Shirikisho halisi la nchi mbili litakuwa ni nchi moja yenye serikali tatu, Serikali ya shirikisho na serikali mbili za zile nchi mbili za awali zilizoungana kuzaa nchi mpya moja.”

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Mwaka ambao Mwalimu Nyerere alichapisha Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania, Makamu Mwenyekiti wake wa CCM na Makamu Rais wake hadi Januari 1984, Alhaj Aboud Jumbe, aliyekuwa pia Waziri wa Afya wa Zanzibar wakati Muungano unazaliwa na baadae Rais wa Pili wa Zanzibar, naye alichapisha The Partnership: Muungano wa Tanganyika na Zanzibar: Miaka 30 ya Dhoruba. Katika kitabu hicho, Alhaj Jumbe anathibitisha kwamba “Ibara za Mkataba wa Muungano ziliweka bayana mfumo ambao serikali kuu na serikali shiriki katika Muungano kuwa na nguvu zinazoendeana, yaani, mfumo wa shirikisho ambao kuna mgawiko wa mahakama, baraza la kutunga sheria na urais baina ya serikali kuu na serikali mbili au zaidi, na kila serikali ikiwa na nguvu kamili ndani ya mamlaka yake.”

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Aina ya dola iliyotokana na Hati ya Makubaliano ya Muungano haikuwahangaisha waasisi wa Muungano ama viongozi wake wakuu peke yao. Hata ndani ya makorido ya mamlaka, mjadala juu ya suala hili umekuwa mkubwa na umeundiwa Tume na Kamati mbali mbali za kulichunguza. Kwa mfano, hata kabla ya kuchapishwa kwa Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania na The Partner-ship, tarehe 6 Aprili, 1992, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Dk. Salmin Amour aliunda Kamati ya Baraza la Mapinduzi ya Kujenga Hoja Juu ya Masuala ya Muungano wa Tanzania, maarufu kama Kamati ya Amina Salum Ali kutokana na jina la Mwenyekiti wake. Mheshimiwa Ali Juma Shamuhuna, ambaye ni mjumbe wa Bunge hili Maalum, alikuwa Katibu wa Kamati hiyo.

Pamoja na mambo mengine, Kamati ya Amina Salum Ali ililichunguza suala la aina ya Muungano uliozaliwa na Hati ya Makubaliano ya Muungano. Jibu la Kamati hiyo lilikubaliana na nusu ya hoja ya Mwalimu Nyerere na nusu ya hoja ya Alhaj Aboud Jumbe: “... Muungano wa Tanzania, haidhuru unaitwa ‘Union’, lakini uko kati na kati baina ya ‘Union’ na Shirikisho. Kuwepo kwa Serikali ya Muungano yenye madaraka makubwa ni kielelezo cha sura ya ‘Union’. Sura hii inazidi kutiliwa nguvu na kile kitendo cha Tanganyika kuvua madaraka yake yote na kuyaingiza katika Serikali ya Muungano. Kwa upande mwengine kuwepo kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye madaraka kamili Zanzibar juu ya mambo yote yasiyokuwa ya Muungano, ni kielelezo dhahiri cha sura ya Shirikisho. Kwa hivyo, Muungano huu ni wa aina yake.”

MTAZAMO WA KITAALUMA

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Hati ya Makubaliano ya Muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar imejadiliwa sana na kwa miaka mingi katika ulingo wa kitaaluma. Mjadala huu umehusu, kwa kiasi kikubwa, aina na muundo wa Muungano huu. Katika kitabu chake Tanzania: The Legal Foundations of the Union, kilichochapishwa kwa mara ya kwanza mwezi Januari, 1990, Profesa Issa Shivji alisema, baada ya uchambuzi wa kina wa Hati ya Muungano, kwamba Makubaliano ya Muungano yalitengeneza katiba ya shirikisho. Kwa mujibu wa Profesa Shivji, katiba za shirikisho zina sifa kuu zifuatazo ambazo alisema zipo katika Hati ya Muungano:

a. Kuna mgawanyo wa wazi wa madaraka kati ya serikali kuu na serikali za sehemu za muungano ambayo yapo katika ngazi moja;
b. Mamlaka ya serikali kuu yaliyowekewa mipaka ya wazi wakati mamlaka yaliyobaki yako mikononi mwa serikali za sehemu za muungano;
c. Serikali zote, yaani serikali kuu na serikali za sehemu za muungano zinagusa maisha ya wananchi wao moja kwa moja tofauti na serikali ya mkataba (confederation) ambako serikali za sehemu ndizo zinazogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.
Kwa maneno ya Profesa Shivji, kwa kuyaangalia Makubaliano ya Muungano kutoka upande wa Zanzibar na Tanganyika na kwa ujumla wao, “... msingi wa shirikisho ndio wenye nguvu na Makubaliano ya Muungano yanaweza kutafsiriwa kwa usahihi kama katiba ya shirikisho.” Kwingineko katika kitabu hicho, Profesa Shivji alidai kwamba: “Kwa vyovyote vile, ni wazi kwamba Makubaliano ya Muungano sio katiba ya muungano (unitary constitution).”

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Msimamo wa Profesa Shivji kuhusu Makubaliano ya Muungano kuwa ni katiba ya shirikisho umeshikiliwa kwa miaka mingi na wasomi wengine wa Muungano huu. Hivyo, kwa mfano, katika kitabu chao cha Tanzania Treaty Practice kilichochapishwa mwaka 1973, Earl E. Seaton na S.T. Maliti walikubali kwamba Makubaliano ya Muungano yaliunda katiba ya shirikisho na sio katiba ya muungano.

Miaka kumi baadae, Wolfgang Dourado, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar wakati Hati ya Muungano inasainiwa, naye alidai kwamba Makubaliano ya Muungano hayakutengeneza dola la muungano bali yalitengeneza ‘shirikisho la kweli.’ Wasomi wengine ambao wameitaja Katiba ya Tanzania kama katiba ya shirikisho na wala sio ya muungano ni Profesa B.P. Srivastava katika makala yake ya mwaka 1984 ‘The Constitution of the United Republic of Tanzania 1977: Some Salient Features, Some Riddles’, na Profesa Palamagamba J.A.M. Kabudi, katika International Law Examination of the Union of Tanganyika and Zanzibar: A Federal or Unitary State?, ambayo ni matokeo ya utafiti aliouwasilisha mwaka 1986 kwa ajili ya Shahada yake ya Uzamili ya Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mwaka 2009 The Legal Foundations of the Union kilichapishwa kwa mara ya pili, mara hii kikiwa na Utangulizi wa Profesa Yash Ghai, Mkuu wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wa kwanza kutoka Afrika Mashariki na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Kenya iliyozaa Katiba Mpya ya Kenya ya mwaka 2010.

Kwenye Utangulizi wake Profesa Ghai anasema kwamba licha ya Tanzania kutokuwepo katika orodha za mashirikisho zilizoandaliwa na wasomi au na Jukwaa la Kimataifa la Mashirikisho (International Forum of Federations); na licha ya Katiba ya Tanzania kutokutumia neno ‘shirikisho’, bado Tanzania ni shirikisho.

“Tanzania inakidhi vigezo vingi vya rasmi vya shirikisho: mahusiano kati ya sehemu zake tofauti yamewekwa katika katiba, ambayo ni sheria kuu, na hayawezi kubadilishwa katika ushirikisho wao bila kuungwa mkono na idadi mahsusi ya wabunge wa kutoka Zanzibar na Bara ... wakipiga kura tofauti tofauti. Katiba inaweza kufanyiwa marejeo na mahakama. Kuna aina mbili za serikali (serikali kuu na serikali za sehemu za shirikisho), kila moja ikiwa na mamlaka yaliyoainishwa wazi. Kuna mabunge ya shirikisho na ya sehemu yake ... na sheria za shirikisho na za sehemu yake zikitumika katika nchi.”

MTAZAMO WA TUME

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Tume ya Mabadiliko ya Katiba (‘Tume’) imetoa maelezo marefu kuhusu madhumuni, lengo na sababu za mapendekezo ya ibara ya 1 ya Rasimu. Pamoja na mengine, kwa mujibu wa Tume, “... lengo la ibara hii ni kuainisha aina na hadhi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa ni Muungano wa Shirikisho lenye Mamlaka Kamili (Sovereign Federal State). Hatua hii ina lengo la kuimarisha Muungano kwa kuipa Mamlaka ya Kidola Jamhuri ya Muungano na kubainisha utambulisho, uwezo na mamlaka ya Nchi Washirika katika Muungano.”

Malengo mengine ambayo Tume imeyataja malengo mengine kuwa ni “... kuainisha mfumo wa utawala wa Jamhuri ya Muungano na kupanua misingi muhimu ya nchi ...”; na kuonyesha kuwa “Hati ya Muungano ya 1964 ndio chimbuko la Muungano wa Tanzania ... na ... kuipa hadhi ya kikatiba Hati hiyo ... kwa ... (kuiingiza) ndani ya Katiba kama ibara inayosimama yenyewe.”

Tume imetaja sababu za mapendekezo haya kuwa ni kutekeleza matakwa ya kifungu cha 9(2)(a) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, yaliyoitaka Tume “... kuongozwa na misingi mikuu ya kitaifa na maadili ya jamii ya kuhifadhi na kudumisha kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano.” Aidha, kwa mujibu wa Tume, mapendekezo haya yatahifadhi asili, taswira na hadhi ya Jamhuri ya Muungano katika jumuiya ya kimataifa kama inavyotakiwa na Mkataba wa Montevideo Kuhusu Haki na Wajibu wa Nchi wa mwaka 1933, ambao unatambua nchi yenye muundo wa shirikisho kuwa ni dola katika sheria za kimataifa.

Tume imetambua ukweli wa kihistoria kwamba kumekuwepo mjadala wa miaka mingi miongoni mwa Watanzania “kuhusu aina ya Muungano uliopo Tanzania iwapo ni shirikisho au la.” Kwa sababu hiyo, pendekezo hili litaondoa “utata wa aina na muundo wa Muungano ambao umesababisha kuvunjwa kwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano na Serikali zote mbili mara kadhaa.”

Tume iliridhika kwamba Jamhuri ya Muungano ni Shirikisho. Kwa maneno yake: “Shirikisho hili linatokana na muungano wa hiari wa Tanganyika na Zanzibar ambazo zilikuwa Jamhuri zenye mamlaka kamili kabla ya kuungana tarehe 26 Aprili 1964.” Tume inafafanua kwamba, kwa kawaida nchi ambazo zimeingia katika muungano zinaweza kuchukua moja kati ya sura tatu:

i. Muungano wa Serikali Moja (Unitary State);
ii. Muungano wa Shirikisho (Federation); na
iii. Muungano wa Mkataba (Confederation).
Kwa mujibu wa Tume, “... mfumo wa shirikisho unakuwepo pale ambapo nchi mbili au zaidi zimeungana na hazikuunda serikali moja. Kwa maana hiyo shirikisho ... linamaanisha mfumo wa utawala wa nchi wenye sifa zifuatazo:

1. Kunakuwa na ngazi mbili za serikali zonazotawala eneo moja la nchi na raia wale wale; moja ikisimamia mambo ya muungano (shirikisho) na nyingine mambo yasiyo ya muungano (yasiyo ya shirikisho);
2. Kila ngazi ya serikali, yaani ile ya shirikisho na ile ya nchi washirika inakuwa na mamlaka kamili na maeneo ya utendaji na uhakikisho wa kikatiba wa uhuru wa kutoingiliana baina ya serikali hizo katika maeneo waliyo na madaraka nayo bila ya kushauriana....;
3. Katika muundo huu, serikali ya muungano ndiyo yenye mamlaka juu ya masuala yote yaliyokubaliwa kuwa ya muungano (shirikisho). Serikali za nchi washirika zinakuwa na mamlaka ya kikatiba ya kushughulikia mambo yasiyo ya muungano katika maeneo yao ya utawala; na
4. Katika muungano wa shirikisho mamlaka kuu ya kidola (sovereign powers and functions) yapo chini ya serikali ya shirikisho (muungano).”
Mheshimiwa Mwenyekiti,

Pamoja na kushindwa kufikisha idadi ya kura inayotakiwa na kifungu cha 26(2) cha Sheria na kanuni ya 64(1), Wajumbe walio wengi – karibu wote wanachama wa CCM – wamependekeza kufutwa kwa ibara ya 1(1) na (2) ya Rasimu. Badala yake, wajumbe hao wanapendekeza ibara mpya ya 1(1) isomeke kama ifuatavyo: “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi yenye mamlaka kamili ambayo imetokana na Muungano wa nchi mbili za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, ambazo kabla ya Hati ya Makubaliano ya mwaka 1964 zilikuwa nchi huru.”

Tofauti pekee ya mapendekezo haya na mapendekezo ya ibara ya 1(1) ya Rasimu ni neno ‘Shirikisho.’ Hii ina maana kwamba, licha ya ushahidi mkubwa wa kitaalamu tuliouonyesha hapa, wajumbe walio wengi wa Kamati Namba Nne wanaamini kwamba Jamhuri ya Muungano sio Shirikisho. Kwa mapendekezo haya, wajumbe na wanachama hawa wa CCM wanapendekeza kuendeleza status quo, yaani sintofahamu ya kama Muungano huu ulitengeneza dola ya ki-Shirikisho au dola ya ki-Muungano, ambayo imeugubika Muungano kwa nusu karne ya uhai wake. Mapendekezo haya yataendeleza pia migogoro ya kikatiba na ya kisiasa ambayo imekuwa ni sehemu ya uhai wa Muungano huu katika kipindi hicho hadi kubatizwa jina la ‘Kero za Muungano.’

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Kwa kuzingatia uchambuzi huu, ni wazi kwamba kuendelea kutumia jina la ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanzania’ kunaendeleza hisia potofu kwamba Makubaliano ya Muungano yalianzisha dola ya muungano (unitary state) na sio dola ya shirikisho (federal state). Aidha, kufanya hivyo ni kuendeleza migogoro ya kisiasa na ya kikatiba ambayo, kama tulivyoonesha, imetokana na kukosekana kwa ufafanuzi juu ya aina ya muungano uliotokana na Hati ya Makubaliano ya Muungano. Hii, kwa maoni yetu, haiwezi kuwa dawa ya matatizo ya Muungano huu.

Kwa sababu hiyo, ili kuweka wazi aina ya muungano uliozaliwa na Hati ya Makubaliano ya Muungano; ili kuondoa hisia potofu kwamba Makubaliano hayo yalizaa dola ya muungano, ili kupata ufumbuzi wa kudumu wa ‘Kero za Muungano’, tunapendekeza kwamba maneno ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanzania’ yaliyoko katika ibara ya 1 na ya 2 na katika ibara nyingine zote za Rasimu yafutwe, na badala yake maneno ‘Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar’ yaingizwe katika ibara husika.

Mapendekezo yetu yana manufaa makubwa yafuatayo. Kwanza, yanaweka wazi kwamba muungano huu ni wa dola ya ki-Shirikisho na wala sio dola ya ki-Muungano. Pili, mapendekezo haya yanaweka bayana ukweli kwamba ni nchi mbili huru, yaani Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ndizo zilizoungana. Uzoefu wa nchi nyingine zilizoungana unaonyesha kwamba jina la muungano huweka bayana kwamba zilizoungana ni nchi zaidi ya moja. Mifano ya wazi ya jambo hili ni majina ya Marekani (United States of America); Uingereza (United Kingdom of Great Britain and Northern Ireland), na Umoja wa Falme za Kiarabu (United Arab Emirates). Aidha, Urusi ya zamani ilijulikana kama (Union of Soviet Socialist Republics) na Yugoslavia ya zamani ilikuwa inaitwa Federal Socialist Republics of Yugoslavia.

No comments:

Post a Comment