Viongozi wa vyama vinavyounda umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA)
Aidha, umeibua shutuma nzito ukidai kuwa serikali imetenga Sh. bilioni 2.5, kwa ajili ya kutoa mada kwenye vyombo mbalimbali vya habari kutaka wananchi waipigie kura ya ndiyo wakati hairuhusiwi kisheria.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, Prof. Ibrahim Lipumba, alisema sheria ya kura ya maoni inaielekeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kusimamia mchakato wa kura ya maoni kuanzia kuboresha daftari la wapigakura hadi kutangaza tarehe ya kupigakura ya maoni.
Alisema kinyume cha sheria hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, alikaririwa akitangaza kuwa kura ya maoni itafanyika Machi 30 wakati Rais Jakaya Kikwete naye alitangaza kuwa kura hiyo itapigwa Aprili, mwakani.
Alisema uboreshaji wa daftari haujafanyika, wala kazi ya kutoa elimu kwa umma inayopaswa kufanywa na Nec bado haijaanza, lakini katika hali ya kushangaza tayari serikali imetangaza tarehe ya kupiga kura.
“Lakini la kustaajabisha ni kwamba Ikulu imeandaa mpango ambao umeelekezwa na Rais Kikwete wa kufanya kampeni utakaogharimu Sh. bilioni 2.5 kwa kutumia vyombo vya habari ili kuwashawishi wananchi waipigie kura ya ndiyo Katiba inayopendekezwa kwa sababu ni ya serikali,” alisema.
Prof. Lipumba alisema sheria haijaviruhusu vyombo vya serikali wajibu wa kufanya kampeni badala yake ni Nec na asasi za kiraia zenye jukumu la kutoa elimu kwa raia na kuunda makundi mawili ya kufanya kampeni.
“Sasa serikali ambayo haimo ndani ya sheria imejisajili yenyewe na kuandaa mpango wa kufanya kampeni. Inasikitisha ambavyo Rais Kikwete haheshimu sheria za nchi…anaanzisha kikundi ndani ya Ikulu kitakachotumia fedha za wananchi kufanya kampeni hii,” alisema.
Kwa upande wake, Katibu wa Ukawa, Dk. Wilbrod Slaa, alisema umoja huo umepata waraka wa Ikulu unaoeleza namna fedha hizo zitakavyotumika ‘kunyonga’ mawazo ya wananchi kwenye kuamua hatma ya Katiba pendekezwa ambao utagharimu kiasi hicho cha fedha.
Alisema katika waraka huo, Rais Kikwete amemwelekeza Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuitangaza Katiba pendekezwa ili waipigie kura ya ndiyo ilhali Rais alipaswa kuelekeza wananchi waisome na kuielewa ndipo wapige kura ya ndiyo au hapana kwa utashi wao.
“Kifungu cha tatu cha waraka huu kinaeleza kuwa Rais Kikwete ametoa maelekezo ya kutaka wananchi waipigie Katiba pendekezwa kura ya ndiyo ili kuiepusha serikali na aibu na tahayari ambayo inaweza kutokea kama wananchi wataikataa Katiba,” alisema.
Dk. Slaa ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chadema, alisema mpango huo unahusisha kampeni ya kuandaa vipindi kwenye televisheni, radio na makala kwenye magazeti ambazo zote zitalipiwa.
Naye Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia, alisema umoja huo haujachoka na hautakata tamaa katika kudai Katiba mpya na kwamba suala la Katiba linahitaji maridhiano na siyo mabavu. Alisema hakuna mtu mwenye haki ya kuamua kuhusu Katiba pendekezwa na kuhofia kwamba mpasuko mkubwa zaidi utaendelea kutokea nchini.
WAMPA POLE WARIOBAUmoja huo umempa pole aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, na kumtaka awe ‘ngangari’ kuendelea kudai Katiba.
Alisema asasi za kiraia ikiwamo Taasisi ya Mwalimu Nyerere zina haki kisheria ya kutoa elimu kwa umma na kwamba alichofanyiwa Jaji Warioba ni ukiukwaji wa sheria hiyo.
“Jaji Warioba ni mtu mwenye heshima kubwa nchini, kwa CCM kuratibu mbinu hizi ni wazi kuna mkakati wa kuzuia mawazo ya watu wenye mawazo tofauti kutoa maoni yao,” alisema Prof. Lipumba.
Alisema vurugu alizofanyiwa Jaji Warioba zimelenga kuwanyamazisha wajumbe wa iliyokuwa Tume ya Katiba kueleza kilichopo kwenye Katiba pendekezwa.
Mbatia amemtaka Jaji Warioba na wananchi wengine kutokata tamaa kuhusu Katiba kwa kuwa kufanya hivyo hakutaivusha nchi.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bawacha), Halima Mdee, ameituhumu Ikulu kwamba imeandaa mkakati wa kuwadanganya wananchi na kuwashawishi kuipigia kura ya ndiyo Katiba inayopendekezwa kupitia vipindi vya Radio na Televisheni pamoja na kuchapisha makala katika magazeti.
Kwa mujibu wa Mdee, mkakati huo unaojulikana kama ‘ijue Katiba inayopendekezwa’ unatarajia kutumia Sh. bilioni 2.5 ambao kwa vipindi vya radio na televisheni pekee vimetengewa milioni 700.
Mdee alisema hayo wakati akihutubia wananchi wa kijiji cha Mwandoya, wilayani Meatu mkoani Simiyu juzi jioni ikiwa ni sehemu ya ziara yake anayoifanya katika mikoa ya Kanda ya Ziwa Mashariki.
Alisema lengo la mkakati huo ni kuiepusha serikali na aibu na tahayari ambayo inaweza kutokea, endapo wananchi wataikataa katika kura ya maoni.
Pia alisema ni kukabiliana na upotoshaji ambao Ikulu imedai unafanywa na makundi yanayoipinga katiba hiyo.
Mdee alisema vipindi hivyo pia vitahusisha radio za jamii kwenye wilaya na mikoa mbalimbali na kuandika makala mbalimbali kwenye magazeti ambazo zitakuwa zinaandikwa vichwa vya habari vyenye kushawishi kuunga mkono kupigia kura ya ndiyo Katiba inayopendekezwa.
Mdee alisema tayari Ikulu imeagiza kuwapo na kamati ya kudumu ya habari ya kusimamia mpango wa kuelimisha umma hadi pale itakapofanyika kura ya maoni.
Mdee alisema jumla ya jopo la watu 20 wameandaliwa kushiriki katika vipindi hivyo na kila kwamba kila mshiriki atakuwa analipwa kati ya Sh. 500,000 na Sh. 200,000 kwa kila kipindi.
“Wamechakachua maoni ya wananchi ambayo waliyapendekeza, wameweka ya kwao na kuyapitisha kwa lazima, sasa wameona kwamba upepo umewakalia vibaya kutokana na uchakachuaji huo sasa Ikulu imeamua kuweka mkakati wa kuwalaghai na kuwashinikiza wananchi waipigie kura ya ndiyo katiba ambayo wamechakachua maoni yao ili kufanikisha mipango yao,” alisema Mdee.
MAJIBU YA IKULU Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu, alipoulizwa kuhusiana na taarifa hiyo, alisema alichokisema Mdee ni Proposal (pendekezo) tu na siyo bajeti.
Alisema haoni tatizo kwa serikali kuandaa mpango huo kwa kuwa lengo lake ni kuelimisha umma juu ya Katiba inayopendekezwa.
“Mimi sioni ubaya serikali kuandaa kitu hicho kwa sababu lengo lake ni kutoa elimu kwa umma na kama yeye (Mdee) anavyozunguka nchi nzima kuipinga Katiba, vivyo hivyo kuna wengine watazunguka nchi nzima kuipigia kura ya ndiyo,” alisema Rweyemamu.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment