Bandari ya Tanga.
Boti ndogo iitwayo Mv. Sarwak iliyokuwa ikisafiri kati ya Tanga na Zanzibar imezama leo kati ya muda wa saa tano za asubuhi na saa saba za mchana na mpaka sasa watu 10 wameokolewa na kukimbiziwa hopspitali visiwani humo huku wengine wawili wakiwa hawajulikani waliko.
Taarifa kutoka Zanzibar zimeeleza kuwa tayari msako dhidi ya watu hao wawili unaendelea na kwamba, majeruhi wako katika eneo la Vikokotoni visiwani humo.
Imeelezwa kuwa raia wawili kutoka Uholanzi na mmoja wa Ufaransa ni miongoni mwa abiria 10 walionusurika baada ya kupatiwa 'life jacket' kabla ya kuzama kwa chombo hicho na baadaye kuokolewa.
Kwa mujibu wa walionusurika wameeleza kwamba, boti hiyo ndogo ilizama baada ya pampu zake zinazotumika kuondoa maji kuharibika ghafla na hivyo maji kujaa wakati ikiendelea na safari kati ya eneo la Pangani, Tanga na Vikokotoni, Zanzibar.
Tukio hilo lililojiri leo limekumbushia ajali kubwa zaidi iliyotokea Julai 18 wakati meli ya Mv Skagit iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam kuelekea Zanzibar ilipozama katika eneo la Chumbe na kusababisha vifo vya abiria wanaokadiriwa kuwa zaidi ya 200.
No comments:
Post a Comment