Mwenyekiti wa Chama cha Walimu nchini Kenya KNUT Bwn. Wilson Sossion [Kulia] na Katibu mkuu wa chama hicho Bwn. David Okuta.
Chama cha
waalimu nchini Kenya KNUT hatimaye kimetangaza kusitisha mgomo wao uliodumu kwa
majuma matatu wakishinikiza kulipwa nyongeza ya msahara pamoja na marupurupu
mengine na Serikali.
Viongozi wa chama hicho walikuwa na mazungumzo na waziri wa fedha wa Kenya
Njeru Githae hapo jana ambapo walikubaliana na mapendekezo mapya ya Serikali ya
kukubali kulipa walimu hao kiasi cha shilingi bilioni 13.5 za Kenya kwa mkupuo.
Awali walimu hao walisisitiza kuendelea na mgomo wao iwapo Serikali
ingeendelea na msimamo wake wa awali wa kutaka kulipa fedha hizo kwa awamu
jambo ambalo walimu walipinga na kuapa kuendelea na mgomo wao.
Aliyetangaza kusitishwa kwa mgomo wa waalimu nchini humo ni katibu mkuu wa
KNUT David Okutta ambaye amesema baada ya kamati ya chama hicho kupiga kura na
kukubaliana wanatangaza rasmi kusitisha mgomo na kurejea kazini siku ya
Jumanne.
Mwenyekiti wa chama hicho Wilson Sossion amewaambia waandishi wa habari kuwa
mpango wa Serikali unakubalika na kwamba waalimu wanatakiwa kuanza kazi mara
moja na fedha zao zitaanza kulipwa kuanzia mwezi wa kumi.
Nae naibu katibu mkuu wa chama hicho Xavier Nyamu amesisitiza kuwa hakuna
mwalimu yeyote atakayechukuliwa hatua na Serikali kwa kosa la kushiriki mgomo
huo na kwamba mgomo ulikuwa halali.
Waziri wa elimu nchini humo Mutula Kilonzo amesisitiza kutekelezwa kwa
makubaliano hayo na kuagiza walimu kurejea kazini mapema kesho asubuhi ili
kutoa mafunzo kwa wanafunzi ambao walikosa masomo kwa wiki tatu.
Hivi sasa mwalimu atapokea kima cha chini cha shilingi elfu 19 wakati yule
wa kiwango cha juu atapokea kiasi cha shilingi laki moja na elfu arobaini.
Katika hatua nyingine baraza la mitihani nchini humo limetangaza tarehe ya
mtihani wa taifa kubakia ile ile licha ya wadau mbalimbali wa elimu nchini humo
kupendekeza tarehe hiyo kusogezwa mbele.
Mtihani wa taifa nchini humo umepangwa kufanyika october 3 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment