Mbunge wa Nyamagana (CHADEMA)
Mh. Ezekiah Wenje
Hii ndio hotuba ya Mbunge wa Nyamagana Mh. Ezekiah Wenje ilicholeta utata Bungeni na kupelekea kikao cha Bunge kusitishwa mpaka mida ya alasiri.
3.0. VYAMA VYA SIASA NA MISAADA KUTOKA NJE YA NCHI.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Umoja wa Mataifa ‘United Nations University’(UNU-WIDER) ya mwezi Aprili 2012 iliyoandaliwa na Aili Mari Tripp ilionyesha kuwa misaada ya wahisani kutoka nje katika mabadiliko ya kisiasa Tanzania ‘Donor Assistance and Political Reform in Tanzania’, inaonyesha kuwa Tanzania imepokea misaada kutoka nje yenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 26.85 toka mwaka 1990-2010.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa ripoti hiyo ni kuwa Tanzania ni nchi inayoongoza kusini mwa jangwa la Sahara kwa kupokea misaada mingi kutoka nje ya nchi na hasa kutoka mataifa ya Ulaya na taasisi za nchi za Uingereza, Marekani, Ujerumani, Uholanzi, Norway, Canada, Sweden, na taasisi kama Benki ya Dunia, IMF ,UNDP ,UNICEF na mengineyo.
Pamoja na misaada yote hiyo, bado tumeendelea kuwa nchi maskini sana duniani pamoja na kuwa na rasilimali lukuki ambazo tumepewa na Mungu ila tunashindwa kuzitumia kwa manufaa ya watanzania na badala yake tumeendelea kudanganywa na vimisaada vidogo vidogo na kubadilishana na rasilimali zetu kama madini, misitu ,wanyama nk kwa ajili ya misaada hiyo.
Mheshimiwa Spika, pamoja na misaada hiyo kwa serikali hii ya CCM bado vyama vya siasa vimekuwa na mahusiano na baadhi ya vyama vingine vya siasa katika mataifa ya magharibi na vimekuwa vikipokea misaada ya aina mbalimbali kama fedha , nyenzo na mengineyo kadiri ya makubaliano na mirengo ya kiitikadi ya vyama husika.Pamoja na ukweli huo bado vipo vyama vya siasa vinavyopotosha umma kuhusiana na misaada vinayopokea kutoka nje ya nchi na vyama hivi vimekuwa mstari wa mbele kueneza propaganda za uongo kuwa vyenyewe havipokei misaada kutoka nchi za magharibi.
Mheshimiwa Spika, CCM wao ‘wanajiita’ kuwa wapo mrengo wa kijamaa/kikomunisti na wamekuwa wakipokea misaada mingi sana ya fedha na nyenzo kutoka Umoja wa Vyama vya Kikomunisti Ulimwenguni ‘Socialist International’ kutoka katika nchi kama za Ujerumani kupitia SDP ,Uingereza kupitia chama cha Labour,China kupitia chama cha Kikomunist ,Marekani kupitia chama cha Democrats. Pamoja na misaada ya kifedha na kiufundi ambayo CCM imekuwa ikipata kutoka nje wamekuwa hawatangazi hadharani hata mara moja kuhusiana na kiasi ambacho wamekuwa wakipokea na hivyo kila kitu kwao imekuwa ni siri kuu ya viongozi wao.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa chama cha CUF, kutokana na itikadi zake za mrengo wa Kiliberali ambazo miongoni mwa misingi yake mikuu ni pamoja na “kupigania haki za ndoa ya jinsia moja, usagaji na ushoga”. Hii ni kwa mujibu wa tangazo lao kwenye mtandao wao wa umoja wa maliberali ulimwenguni, likiungwa mkono na Waziri wa Haki na Usawa wa Uingereza, Lynn Featherstone kutoka chama cha Liberal Democrats wakati chama hicho (www.liberal-international.org) kilipokuwa kinapitisha azimio la kuruhusu ndoa za jinsia moja kama haki ya mtu mmoja mmoja, wanashirikiana na vyama kama vile LPC ya Canada, Det Radikale Venstre cha Norway, FDP cha Ujerumani, Israel Liberal Group cha Israel,PDS cha Senegal na Liberal Democrats cha Uingereza.
Kutokana na umoja huo, CUF wamekuwa wakipata msaada wa kifedha na nyenzo nyingine mbalimbali kutoka kwa vyama hivyo vya mrengo wa Kiliberali na msaada wa mwisho ni hivi majuzi mwezi Machi 2013 waliposaini makubaliano na chama cha Kiliberali kutoka Norway.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa CHADEMA, wapo kwenye Umoja wa Vyama vya Kidemokrasia Ulimwenguni (International Democratic Union - IDU). Huu ni umoja wa vyama ambavyo vipo kwenye mrengo wa kati na ambavyo msingi wake mkuu ni pamoja na kuwa na familia, kama taasisi muhimu katika jamii, ikimaanisha kwamba: “tunapinga vitendo vyote vya ushoga na usagaji”. Tunatetea demokrasia, haki za binadamu na kupambana na ufisadi katika serikali. Vyama wanachama wa umoja huu ni pamoja na Conservative Party cha UK, CPP cha Norway, Republican cha Marekani na vingine vinavyofuata mrengo huo.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya upinzani Bungeni, inavitaka vyama vyote ambavyo vimekuwa na mahusiano na vyama vya nje viweke wazi mikataba yao na malengo ya mahusiano hayo ikiwa ni pamoja na misaada ambayo vimekuwa vikipokea kutoka kwenye nchi hizo.
No comments:
Post a Comment