MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba,
ameibua suala zito akikihusisha chama chake na “kumnusuru” Rais Jakaya
Kikwete katika uchaguzi mkuu uliopita.
Profesa Lipumba alitoboa siri hiyo
katika Msikiti wa Idrissa, Kariakoo, jijini Dar es Salaam, alikokwenda
kuswali swala ya Ijumaa, miezi kadhaa iliyopita.
Kwa mujibu wa video ya tukio hilo, ambayo gazeti la Tanzania Daima limekiri kuwa na nakala
yake, Profesa Lipumba alikaribishwa kuzungumza na waumini hao mara baada
ya utangulizi uliotolewa na Imamu wa msikiti huo, Sheikh Ali Basaleh,
aliyemtaka awaeleze Waislamu hali ya kisiasa nchini kuelekea Uchaguzi
Mkuu wa 2015.
Huku akisisitiza juu ya umuhimu wa mshikamano wa kiimani, Profesa
Lipumba alianza kwa kuzungumzia matokeo ya uchaguzi mkuu wa 2010, na
ushindani mkali wa kisiasa uliokuwapo.
Alisema hawaoni matunda ya jitihada walizofanya kumnusuru Rais Kikwete
asishindwe, kwani hata chini ya uongozi wake, Waislamu wameendelea
kutothaminiwa.
“Ninyi masheikh mnajua vizuri zaidi hali ya kisiasa ilivyokuwa, kwamba
ilibidi zifanyike juhudi za makusudi ili kuokoa jahazi. Lakini pamoja
na kuliokoa jahazi, hali halisi inaonyesha mpaka sasa hakuna matunda
yoyote yaliyopatikana, na tupo katika mtihani mgumu zaidi,” alisema.
Katika hali ambayo inasemekana ushindi wa Rais Kikwete ulipatikana kwa
mbinu, huku wengine wakiituhumu Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa
ilimnusuru mgombea wa CCM, kauli hii ya Profesa Lipumba inadokeza kwamba
anajua mkakati zaidi wa kazi ya Tume ya Uchaguzi.
Katika hali isiyo ya kawaida, Profesa Lipumba anaonekana kuhamasisha
Waislamu kujipanga akisema “wenzetu wameanza kujipanga” kuelekea 2015.
“Kwahiyo kama Waislamu tunataka kupata haki zetu, kama tunataka kuishi
kama raia wa daraja la kwanza katika nchi yetu, lazima tujipange
kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015; na sisi tuanze kujipanga kwa sababu
wenzetu wameanza kujipanga, vinginevyo tutaendelea kubaki maskini na
raia wa daraja la nne katika nchi yetu wenyewe.
“Mwaka 2010 wakati mshindi wa uchaguzi wa rais alipotangazwa, mimi
nilikwenda kwenye hafla ya kutangazwa matokeo, na nilikwenda makusudi
tu, siyo kwamba uchaguzi ulikuwa huru na wa haki, ila nilikwenda
makusudi kwa kujua hali ya kisiasa ilivyokuwa wakati huo.
“Huku nilikutana na Sheikh Basaleh. Nilipokutana naye, alinipongeza;
sijui kama yeye anakumbuka, akaniambia ‘umeweka mbele imani yako na
umekuwa mwelewa wa mambo.’”
Hata hivyo, licha ya Profesa Lipumba kuwaambia Waislamu wajipange kwa
ajili ya uchaguzi mkuu, hakusema wajipange kupitia chama kipi.
Lakini alisisitiza kwamba uchaguzi ujao ni zaidi ya siasa au rais yupi
anafaa, bali maslahi, hasa ya rasilimali nyeti zinazopatikana katika
ukanda wa Pwani ya Mashariki, eneo ambalo alisema linakaliwa zaidi na
watu wenye imani ya Kiislamu.
Katika moja ya kauli zake, Profesa Lipumba alisema kwamba kuna chama
kimoja kinataka kuchukua madaraka ya nchi, lakini kinasaidiwa na mataifa
ya magharibi, yasiyoenzi wala kuthamini imani ya Kiislamu.
Kwa muda sasa, zimekuwapo tetesi kwamba CCM imekuwa inafanya siasa za
udini dhidi ya vyama vya upinzani, hasa inapoona maslahi yake yapo
hatarini.
Mwaka 2010 makada kadhaa wa CCM walitumia mitandao ya simu kuchonga
(spoofing) ujumbe wa simu ulioshambulia mgombea mmoja wa upinzani,
ukimhusisha na imani yake.
Kauli ya Lipumba imethibitisha pia minong’ono iliyokuwapo muda mrefu
kuwa baadhi ya kura za Profesa Lipumba zilipotelea kwa Rais Kikwete.
Katika uchaguzi huo, Lipumba alitangazwa kushika namba ya tatu, nyuma ya Rais Kikwete na Dk. Willibrod Slaa wa CHADEMA.
Alipoulizwa kuhusu ziara yake msikitini na kauli aliyotoa, Profesa
Lipumba alikiri kwamba alikwenda kuzungumzia hali ya kisiasa nchini.
Hata hivyo alisema inawezekana video hiyo imechakachuliwa kwa kuungaunga
vipande vya matamshi wanavyovitaka badala ya hotuba nzima.
Hata hivyo, video iliyotazamwa na waandishi wa habari hii, ambayo
nakala yake imetunzwa na gazeti hili, haionekani kukatwakatwa.
Katika tukio hilo, Sheikh Baseleh ndiye anayeanza kuzungumza huku
akisoma kipande cha gazeti lililomnukuu Waziri wa Uwezeshaji na
Uwekezaji, Dk. Mary Nagu, akizungumzia mchakato wa katiba, kwamba Tume
ya Katiba “haitazingatia maoni ya wachache”, na kwamba mambo ya dini
yasiingizwe kwenye katiba.
Katika ufafanuzi wake, Sheikh Basaleh anasema Dk. Nagu alizungumza
mambo haya mbele ya waumini wa Kanisa la Chang’ombe kwenye uzinduzi wa
kwaya; na kwamba miongoni mwa mambo ambayo yanaitwa ya kidini
yasiyotakiwa kuingizwa kwenye katiba ni Mahakama ya Kadhi Mkuu.
Baadaye anamkaribisha Profesa Lipumba, ambaye naye katika hotuba yake,
pamoja na mambo mengine, anakosoa msimamo wa serikali kutaka Waislamu
waanzishe mahakama yao ya kadhi, akisema mahakama ni chombo cha dola
ambacho hakipaswi kuwa nje ya mfumo wa serikali.
Mara baada ya Profesa Lipumba kuhitimisha hotuba yake, Sheikh Basaleh
alimkaribisha Sheikh Musa Kundecha, ambaye naye alisisitiza kauli ya
Profesa Lipumba kuwataka Waislamu wajipange kwa ajili ya 2015.
Vile vile alifafanua kuwa “wachache” waliozungumzwa na Dk. Nagu ni
Waislamu, kwani zilishatoka taarifa katika kituo cha TBC kuwa idadi ya
wasiokuwa Waislamu nchini ni asilimia 52.
“Mimi sijaiona hiyo video ila nimeisikia tu kuwa ipo inauzwa mitaani
na makanisani, lakini inawezekana waliorekodi wamenichakachua maana
imekuwa siku nyingi kidogo tangu niende kuongea pale Msikiti wa Idrissa.
Yamewezekana wameungaunga vipande wanavyovitaka ili kunipaka matope
mimi na CUF kuwa tuna udini,” alifafanua Profesa Lipumba.
Alipotakiwa akutane na waandishi wa habari hii ili waiangalie kwa
pamoja video hiyo ili kujua ukweli kama ni video halisi au ya
kuchakachua, Profesa Lipumba alisema waandishi waende kumwona Naibu
Mkurugenzi wa Habari na Mahusiano ya Umma, Abdul Kambaya.
Alipopigiwa simu, Kambaya hakutoa ushirikiano kwa waandishi. Badala
yake aliwashambulia kuwa wana ajenda ya siri dhidi ya CUF, akisema
wanafuatilia na kuona makosa ya viongozi wa CUF tu na kufumbia macho
vitendo vya wanasiasa wengine wanapokwenda makanisani.
“Nyie waandishi wa Tanzania mmezidi, yaani ninyi mnaona matendo ya
viongozi wa CUF tu, wengine wakienda makanisani mbona hawafuatiliwi?
Mbona hamumfuatilii Lowassa akienda makanisani? Au mbona hamsemi Dk.
Slaa akienda kanisani? Sasa Profesa akienda msikitini kuongea na
Waislamu wenzake kuna kosa gani? Sasa ninyi andikeni chochote,” alifoka
na kukata simu.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF Tanzania Bara, Julius Mtatiro alipotakiwa
kuzungumzia video hiyo, alikataa katakata na kuwashauri waandishi
wawasiliane na ama Profesa Lipumba mwenyewe au Kambaya.
Itakumbukwa kuwa kumekuwepo tuhuma dhidi ya Rais Kikwete na CCM kuwa
mwaka 2010 waliendesha propaganda chafu za udini zenye lengo la kuwagawa
Watanzania hususan Wakristo na Waislamu kwa manufaa yao ya kisiasa.
Mwelekeo huo wa kisiasa wa Rais Kikwete na CCM unadaiwa kutokana na
hatua ya viongozi wa Kanisa Katoliki nchini kupitia Idara ya Uchungaji
kutoa waraka maalumu uliowataka Watanzania kuchagua viongozi waadilifu.
Waraka huo haukuifurahisha CCM, ambayo imekuwa inagubikwa na tuhuma
nyingi za ufisadi. Makada na viongozi wa CCM walijaribu kuupinga kwa
kuupotosha, wakisema unaingiza mambo ya dini katika siasa.
Kanisa Katoliki lina utaratibu wa muda mrefu wa kutoka nyaraka
kuelekeza waamini na wananchi juu ya mambo ya msingi katika jamii.
Katika hali hiyo, Rais Kikwete na CCM wanadaiwa kukimbilia kwa
viongozi wa Kiislamu na kuwaomba wawaunge mkono kwa kuwajaza maneno ya
uongo, kwamba Wakatoliki walikuwa wamewaagiza waumini wao kupigia kura
wagombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Inadaiwa waliwafitinisha zaidi kwa kuwaeleza kuwa aliyekuwa mgombea
kiti cha rais wa CHADEMA katika uchaguzi huo, Dk. Willibrod Slaa ambaye
ameshawahi kuwa Padri, alikuwa ametumwa na Kanisa Katoliki ili
kuendeleza utawala wa Kikristo nchini.
Propaganda hizo hazikuishia kwa viongozi na waumini wa Kiislamu tu,
bali zilielekezwa pia kwa viongozi na wafuasi wa CUF ambao walirubuniwa
na kushawishiwa kumpigia kura “Muislamu mwenzao” Rais Kikwete, huku
wakiahidiwa kuwa mwaka 2015 Waislamu wa CCM nao watampigia kura mgombea
wa CUF kwa hoja kuwa CCM watakuwa wamesimamisha mgombea Mkristo.
Licha ya madai hayo ya udini kuwa wazi kwa muda mrefu, lakini wakati
wote Rais Kikwete na CCM wamekuwa wakikanusha tuhuma hizo na kuziita
kuwa uongo na uzushi.
No comments:
Post a Comment