Nakumbuka katika kampeni za uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 ziligubikwa na matukio mengi ya kila namna mazuri kwa mabaya ambayo kwa namna moja au nyingine mengi yalipelekea kuwakera sana wananchi wapenda amani na utulivu, na jambo moja wapo ambalo kwa upande wangu ni baya lilikuwa ni matumizi mabaya ya Simu za Mkononi ilihali mamlaka husika ya Udhibiti wa Mawasiliano
Tanzania (TCRA) na Jeshi la Polisi likionekana kufurahishwa na kitendo hicho hata kuacha hali hiyo kuendelea kutukia pasipo kuchukua hatua zozote zile.
Ikumbukwe kwamba Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano
Tanzania (TCRA) inajivunia usajili wa simu za mkononi, ilikuwa inadai simu za mkononi zinatumiwa kufanya uhalifu.
Uhalifu uliotajwa ni pamoja na kutukana, kupanga wizi na, au hujuma;
kutoa vitisho kwa watu mbalimbali; kutoa taarifa za upotoshaji na wakati
wote huo bila mhusika kufahamika.
Serikali ilidai simu zikisajiliwa, kazi yake ya “ulinzi wa amani”
itakuwa imerahisishwa. Simu zilisajiliwa. Wamiliki walisajiliwa. Je,
serikali na TCRA wanaweza kutuambia simu Na. +3588976578 na +3588108226
ni za nchi gani, mtandao gani na mmiliki wake ni nani?
Tuliuliza TCRA waeleze asili ya namba hizo lakini hawakueleza.
Tukahoji kampuni ya nje inaweza kutuma ujumbe ukaingia kwenye simu za
Watanzania bila kushirikiana na kampuni yoyote nchini petu? Jibu likawa
hapana.
Tukaambiwa mchezo huo unachezwa na wataalamu wa kompyuta mahali
fulani Dar es Salaam. Tukasema kama ni hivyo, tuwafuate wataalamu wa
intelejensia ya kujua al-Shaabab wanavyochukia maandamano ya CHADEMA
lakini wakafurahia mikusanyiko ya CCM – Polisi.
Polisi wakasema hawazijui namba. Iwapo polisi na TCRA hawajui na
hawataki kudhibiti namba zisizojulikana, ni dhahiri mfumo wa utawala
ulishiriki kufanikisha kashfa dhidi ya Dk. Slaa.
Tulipiga hodi kwa Msajili wa Vyama Vya Siasa. Bwana huyu akasema
hajaziona namba hizo hivyo hawezi kuzungumzia kitu asichokijua.
Chombo cha mwisho kilikuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Wao
wakasema polisi wanaweza kuwa katika nafasi nzuri ya kuzungumzia lakini
si wao.
Ujumbe wa kashfa unasambazwa dhidi ya mgombea lakini Polisi, TCRA,
NEC na Msajili wakajiweka kando. Hivi ingekuaje kama ujumbe ule wa
kashfa ungekuwa dhidi ya mgombea wa CCM?
Kwa ufupi tu ni kwamba Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano
Tanzania (TCRA) Jeshi la Polisi na makampuni ya Simu za mikononi na mamlaka nyinginezo zijiandae kwani katika
kampeni za uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015 kwa hali yoyote ile Wananchi hawatarajii tena
kupokea ujumbe wa kashfa kutoka katika mitandao ya simu kama ilivyokuwa
katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 ambapo pasipo mapenzi yao kuomba wala kutaarifiwa Wananchi walio wengi walijikuta wakipokea
ujumbe katika simu zao za mikononi uliokuwa ukikikashifu Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) au Mgombea wa kiti cha Urais Mh. Dr. Wilbroad Slaa
achilia mbali Ujumbe wa uchochezi wa mambo ya kidini na kikabila ambao ulikuwa ukitumwa na baadhi ya mitandao ya simu za mikononi ya hapa nchini kupitia katika namba hizi (+3588976578 na +3588108226
) namba ambazo zaidi ya ujumbe wa kashfa zilioubeba labda kwa agizo au lengo maalum Wananchi walio wengi hawakuweza kujua mara moja ni za nchi gani na kwanini Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano
Tanzania (TCRA) na jeshi la Polisi ilifumbia macho matumizi hayo mabaya ya Simu za mikononi.
Hali hiyo inatoa picha ya wazi kwamba aidha Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ilihusika moja kwa moja na vitendo hivyo vya kukichafua kwa makusudi Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Mgombea wake (Dr. Slaa) ili kukisaidia kaweza kurudi madarakani au la kuna watu wachache ambao walitenda makosa hayo kwa nia au lengo la kuvuruga amani na utulivu uliopo nchini, ingawa bado maswali yanatabaki kuwa:
1. Ni kwanini mpaka leo Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano
Tanzania (TCRA) na jeshi la Polisi hawajachukua hatua wala kutoa tamko lolote kuhusiana na matumizi mabaya ya simu za mikononi yaliyotokea tena wakati wa kipindi muhimu cha Uchaguzi Mkuu (2010)?!
2. Je Usajili wa line za simu za mikononi una faida gani ilihali mamlaka husika ikishindwa kusimamia zoezi husika la udhibiti wa matumizi mabaya ya simu za mikononi?!
3. Kwa kilichotokea katika kampeni za uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 je ni nani wa kulaumiwa??!!
a. Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),
b. Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano
Tanzania (TCRA),
c. Jeshi la Polisi,
d. Mitandao ya Simu,
e. Wananchi au
f. Simu za Mikononi
No comments:
Post a Comment