*Waiunga mkono tume ya Jaji Warioba na kutaka iheshimiwe,
*Watetea Maoni ya Wananchi yaliyomo kwenye Rasimu,
*Wasema Muundo wowote wa Serikali unafaa.
Maaskofu 32 wa Kanisa Katoliki Tanzania, wametoa waraka maalumu wa Pasaka wakiwataka wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kuheshimu maoni ya Watanzania yaliyomo katika Rasimu ya Katiba na kuweka pembeni itikadi za kisiasa katika mchakato wa kuandika Katiba Mpya.
“Tunalisihi na kulishauri Bunge Maalumu la Katiba kuheshimu mawazo yaliyowasilishwa na kutumia busara zilizopendekezwa za kujenga muundo wa Muungano utakaokidhi mahitaji ya utangamano, mshikamano, amani, maadili, uhuru na uwajibikaji wa viongozi na raia wa Tanzania,” walisema katika tamko hilo ambalo, Makamu wa Rais wa TEC, Askofu Severine Niwemugizi alithibitisha kuwa umetolewa na kanisa hilo.
Kauli ya viongozi hao ambayo ilisomwa katika makanisa mbalimbali nchini jana, imekuja ikiwa zimepita siku sita tangu Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia vikao vya Bunge Maalumu la Katiba kutokana na mvutano unaoendelea juu ya hoja ya muundo wa Serikali.
“Kazi ya kuandika Katiba ni ngumu na haishangazi kuona migongano ya hoja kwa makundi kinzani. Mawazo ya wengi yamewasilishwa kisheria na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa ajili ya kujadiliwa na Bunge Maalumu la Katiba,”.
“Sasa, tunashuhudia makundi yenye nguvu yakijaribu kushinikiza kuingizwa matakwa yake kwenye Katiba kwa njia zozote zile ili kujihakikishia kuendelea kulinda maslahi yake kisiasa"
“Kupungua kwa hisia za kujisikia watu wote ni taifa moja, ni dosari iliyoanza kukua taratibu na sasa inaonekana kuwa ndiyo ukweli,” walisema.
Walisema kasoro zilizojitokeza katika mambo mbalimbali ndiyo chanzo cha watu kutaka mabadiliko: “Watu wengi walitaka na wanataka mabadiliko au mageuzi ya msingi. Kwa msukumo huo ndiyo sababu ya kuingia katika mchakato wa kuandika katiba mpya"
“Tuandae Katiba ambayo itatupatia misingi imara ya maadili itakayotuongoza kupigana dhidi ya ubinafsi na ufisadi na kutetea haki za binadamu kwa wote,” walisema.
Hata hivyo, walisema iwapo utakuwapo muafaka na kukubaliana katika mambo muhimu kwa maisha ya mshikamano wa kitaifa ambayo katika Rasimu ya Katiba yameandikwa kwenye sura ya kwanza hadi ya tano, muundo wowote wa serikali unawezekana.
Walisema ili kufikia lengo la kuwa na Katiba bora ni lazima maoni ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba yaheshimiwe kama ambavyo imetamka Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
“Kuwe na nia njema ya kutafuta suluhisho la matatizo mengi ya utendaji katika dola zilizopo katika Muungano, kutokuwa wabinafsi pamoja na kuchambua matatizo ya sasa ya Muungano na kuridhia mfumo utakaomaliza matatizo hayo,” walisema.
Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC) la Ubungo, Dar es Salaam, Anthony Lusekelo maarufu ‘Mzee wa Upako’
MCHUNGAJI LUSEKELO;
Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC) la Ubungo, Dar es Salaam, Anthony Lusekelo maarufu ‘Mzee wa Upako’ amemtaka Rais Jakaya Kikwete kusitisha mchakato wa Katiba kwa lengo la kunusuru amani ya Taifa.
Lusekelo alisema siyo lazima Katiba Mpya ipatikane mikononi mwa Rais Kikwete kwa kuwa hatua iliyofikiwa kwa sasa ni kubwa, hivyo inaweza kuendelezwa na Rais atakayefuatia mwaka 2015.
Akizungumza jana katika ibada ya Pasaka, Lusekelo alisema hali inayoendelea kwa sasa inajenga hofu na kuwachanganya Watanzania kutokana na hofu ya Uchaguzi Mkuu ujao.
Alisema Bunge la Katiba kwa sasa limekuwa mfano wa klabu ya pombe za kienyeji kutokana na vurugu alizodai kuchangiwa na wajumbe wa CCM.
“Hakuna majadiliano ya kujenga hoja na badala yake tunasikia matusi tu yanarushwa... uamuzi wa Profesa Ibrahim Lipumba kutoka nje ulikuwa ni sahihi. Hata mimi iwapo ningekuwa mjumbe, ningekuwa wa kwanza kutoka,” alisema Lusekelo na kuongeza:
“Kwa hiyo ni vyema mchakato ukasitishwa kwa hatua iliyofikia ili Taifa litulie na wananchi wajiandae kwa Uchaguzi Mkuu ujao.”
ASKOFU GLORIOUS SHOO;
Askofu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), mjini Moshi, Kilimanjaro, Glorious Shoo amewatahadharisha wajumbe wa Bunge la Katiba kutotumia wingi wao bungeni kuzuia mabadiliko ya Katiba.
Akizungumza katika ibada ya Jubilee ya miaka 75 ya kanisa hilo, Askofu Shoo alisema umefika wakati ambao Watanzania wanataka mabadiliko, hivyo wajumbe wa Bunge Maalumu wasitumie wingi wao kuzuia mabadiliko.
“Tusilazimishe kwa wingi wetu kuzuia mabadiliko kwa sababu ukweli tunaposema wingi wetu ni pale bungeni tu, lakini wingi wetu sisi tulioko nje tunasikia kelele nyingi zinazolazimisha mabadiliko naiomba Serikali izingatie hilo,” alisema Askofu Shoo.
“Watu wanaosoma nyakati, wanajua ukifika wakati wa mabadiliko hakuna anayeweza kuzuia na ukijaribu kuyazuia mabadiliko hayo yanakuja kukubadilisha wewe,” alisema Askofu Shoo.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zachary Kakobe
ASKOFU KAKOBE;
Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zachary Kakobe ametangaza kuungana na wanaodai Serikali ya Tanganyika na kuahidi kujenga ari na shauku ya kuhakikisha inarejeshwa.
Akizungumza wakati wa ibada ya Pasaka iliyofanyika kanisani hapo jana, Askofu Kakobe alisema anafanya hivyo si kwa ushabiki ila ni kutokana na mipango ya Mungu, ambayo iliwezesha kuwapo kwa Tanganyika huru. Huku akishangiliwa na waumini wa kanisa hilo, Askofu Kakobe alisema wanaoidai Tanganyika katika Bunge la Katiba wapo sahihi na yeye anaungana nao na kuwa wanaopinga wamekosa hofu ya Mungu.
“Serikali ilitumia mamilioni ya shilingi kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru, lakini wanashindwa kutamka uhuru wa nchi gani!”
(Chanzo, Gazeti la Mwananchi, Jumatatu - 21/04/2014)
No comments:
Post a Comment