Naibu Waziri wa
Nishati na Madini Mhe. Stephen Masele.
Mbali na kutajwa katika njama hizo ambazo Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mjini, Anarose Nyamubi anadaiwa kukataa zisitekelezwe katika wialaya yake, Masele pia anahusishwa na kupanga kiasi cha fedha kilichotakiwa kutolewa kwa madiwani wawili wa CHADEMA kama wangeweza kufanikisha mkakati huo.
Tuhuma hizo nzito zilitolewa jana jijini Dar es Salaam na diwani wa Kata ya Ngokelo, Sebastian Peter kutoka mkoani Shinyanga wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya CHADEMA.
Hata hivyo, wawili hao Masele na Nyamubi hawakuweza kupatikana kujibu tuhuma hizo, na alipoulizwa msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso kama waliwahi kupokea malalamiko hayo, alisema hawana taarifa yoyote na kwamba hao waliotoa taarifa hizo wanapaswa kuziwasilisha polisi ili zifanyiwe kazi.
Peter maarufu kama Obama na diwani mwenzake wa kata ya Masekelo, Zakaria Mfukwa, alisema kuwa awali walihamia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa ahadi ya kuboreshewa maisha ukiwa ni mkakati wa Waziri Masele.
Alifafanua kuwa mkakati huo wa kuwauwa viongozi hao wa CHADEMA ulikuwa utekelezwe mapema Februari mwaka huu, wakati viongozi hao walipofika mkoani Shinyanga kwa ajili ya kukusanya maoni ya wanancchi juu ya muundo wa serikali.
Alisema mara baada ya aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Zitto Kabwe kusimamishwa uongozi wa chama hicho, walifuatwa na Habibu Mchange na kuelezwa kuwa kuna mpango unaoweza kuwaondoa katika lindi la umasikini ikiwa wataweza kuufanikisha.
“Baada ya maongezi ya aina mbali mbali na Mchange tulishindwa kupata muafaka lakini tuliendelea kuwasiliana na aliporudi Shinyanga akatueleza kuwa kuna mpango mzuri wa fedha na kwamba utasimamiwa na Waziri Masele na kwamba tutapata sh. milioni 180 kila mmoja,”alisema.
Aliongeza kuwa alipigiwa simu na Masele na kisha kuelekezwa kazi ya kufanya kuwa ni kutoa taarifa ya helikopta iliyombeba Dk. Slaa na Mnyika ingetua eneo gani itakapofika Shinyanga Mjini na kwamba ni nani wengine ambao wangekuwa katika msafara huo, huku wakielezwa kuwa jukumu lao lingeishia katika kutoa taarifa na mikakati ya ulipuaji ingesimamiwa na Masele.
Alisema katika mkakati huo, mkuu wa Wilaya ya Shinyanga mjini, Anarose Nyamubi ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya alikataa mpango huo kutekelezwa katika wilaya yake hali iliyowafanya wao wajiulize kama wana sababu ya kuendelea na jambo hilo.
“Nilipofikiria Taifa na nikafikiria namna msiba wa Dk. Slaa na Mnyika utakavyopokewa nikaona siwezi kutekeleza jambo hilo nilichoweza kuwashauri ni kwamba waandae mabango ya kumzomea Dk. Slaa,”alisema Peter.
Akizungumzia mikakati hiyo, Mwanasheria wa CHADEMA, Tundu Lissu, alisema siku zote wamekuwa wakiueleza umma juu ya njama zinazofanywa na CCM kupitia kwa watu waliofukuzwa ndani ya CHADEMA kama Habibu Mchange aliyetajwa kuwa nyuma ya uratibu wa mkakati huo kwa kushirikiana na CCM.
Alisema kitendo cha kutaka kulipua helikopta makosa yake yanaelekezwa katika sheria ya kukabiliana na ugaidi na kwamba jeshi la polisi linapaswa kuchukua hatua zinazostahili.
No comments:
Post a Comment