Jeshi la Polisi mkoani Kiliamanjaro, limeingia katika kashfa baada ya askari wake wawili kudaiwa kumlisha sumu mtuhumiwa waliyemkamata na mbao zinazodaiwa kuvunwa isivyo halali na kusababisha kifo chake.
Habari zilizopatikana jana kutoka wilayani Rombo na kuthibitishwa na baadhi ya maofisa wa polisi mkoani hapa, zilidai kuwa tukio hilo lilitokea Novemba 17, mwaka huu, katika kijiji cha Kiraeni ambako polisi hao wakiwa na pikipiki, walimkamata mtuhumiwa na vipande vinane vya mbao na kisha kumtaka awape rushwa ya sh 400,000.
Kwa mujibu wa mashuhuda waliozungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu kutoka Rombo, askari hao wanadaiwa kumpa vitisho vya kila aina marehemu aliyetajwa kwa jina la Hubert Massawe na baadaye kupewa sh 100,000.
Mashuhuda hao walidai kuwa baada ya askari hao kupewa kiasi hicho walimshurutisha marehemu awamalizie kiasi kilichobaki na kwenda naye hadi nyumbani kwake ambako hawakuambulia chochote kutokana na kutokuwa na fedha zaidi.
Kamanda wa polisi mkoani Kilimanjaro, Robert Boaz, hakuwa tayari jana kuthibitisha tuhuma hizo baada ya kutuma ujumbe mfupi kwa maandishi kupitia simu yake ya kiganjani kuwa yuko kwenye mkutano.
Naye Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa [TAKUKURU] wilayani Rombo, Chuzela Shija, alisema taasisi yake imeanzisha uchunguzi juu ya tukio hilo kutokana na kile alichodai kuwa linahusu tuhuma za rushwa.
Inadaiwa kuwa askari hao baada ya kuona mtuhumiwa ameshikwa na jazba,walimpa maji yaliyokuwa kwenye chupa yanayoamika kuwa ni sumu na kumlazimisha ayanywe.
Kwa mujibu wa mashuhuda hao, mtuhumiwa alichukua maji hayo na kuingia nayo ndani na aliporudi alinza kujisikia vibaya na kukimbizwa katika zahanati ya kijiji cha Kiraeni lakini kutokana na kuzidiwa na sumu hiyo alikimbizwa hospitali ya wilaya ya Huruma na alifariki Novemba 18, mwaka huu.
Machi mwaka huu, askari watatu wa kituo cha polisi cha Tarakea wilayani Rombo walifukuzwa kazi kwa fedheha wakituhumiwa kufanya vitendo vya kulidhalilisha jeshi hilo baada ya kuuza mali ya mfanyabiashara mmoja wilayani Rombo, Genes Shayo, bila ridhaa yake na bila yeye kuwapo.
Askari waliofukuzwa kazi ni pamoja na aliyekuwa dereva wa mkuu wa kituo cha polisi Tarakea, mwenye namba D.3289 Sajenti Joseph, F.3677 PC. Esebius kutoka idara ya upelelezi wa makosa ya jinai na F.6620 PC. Johnson ambaye ni askari wa kawaida.
Chanzo: Jf http://www.jamiiforums.com/jukwaa-la-sheria-the-law-forum/358397-polisi-wadaiwa-kumlisha-sumu-mtuhumiwa.html
No comments:
Post a Comment