SEHEMU YA TATU
HAKI NA WAJIBU MUHIMU
Haki ya Usawa Usawa wa binadamu
Sheria ya 1984 Na.15 ib.6
12.-(1) Binadamu wote huzaliwa huru, na wote ni sawa.
(2) Kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na
kuthaminiwa utu wake.
Usawa mbele
ya Sheria ya
1984 Na.15 ib.6
13.-(1) Watu wote ni sawa mbele ya sheria, na wanayo haki,
bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya
sheria.
Sheria ya Na.4
ya 1992 ib.8
Sheria ya 2000
Na.3 ib.5
(2) Ni marufuku kwa sheria yoyote iliyotungwa na mamlaka
yoyote katika Jamhuri ya Muungano kuweka sharti lolote ambalo
ni la ubaguzi ama wa dhahiri au kwa taathira yake.
(3) Haki za raia, wajibu na maslahi ya kila mtu na jumuiya ya
watu yatalindwa na kuamuliwa na Mahakama na vyombo
vinginevyo vya Mamlaka ya Nchi vilivyowekwa na sheria au kwa mujibu wa sheria.
(6) Kwa madhumuni ya kuhakikisha usawa mbele ya sheria,
Mamlaka ya Nchi itaweka taratibu zinazofaa au zinazozingatia
misingi kwamba -
(a) wakati haki na wajibu wa mtu yeyote vinahitaji
kufanyiwa uamuzi wa mahakama au chombo
kinginecho kinachohusika, basi mtu huyo atakuwa na
haki ya kupewa fursa ya kusikilizwa kwa ukamilifu, na
pia haki ya kukata rufaa au kupata nafuu nyingine ya
kisheria kutokana na maamuzi ya mahakama au
chombo hicho kingenecho kinachohusika;
(b) ni marufuku kwa mtu aliyeshtakiwa kwa kosa la jinai
kutendewa kama mtu mwenye kosa hilo mpaka
itakapothibitika kuwa anayo hatia ya kutenda kosa
hilo;
(c) ni marufuku kwa mtu kuadhibiwa kwa sababu ya
kitendo chohote ambacho alipokitenda hakikuwa ni
kosa chini ya sheria, na pia kwamba ni marufuku kwa
adhabu kutolewa ambayo ni kubwa kuliko adhabu
iliyokuwapo wakati kosa linalohusika lilipotendwa;
(d) kwa ajili ya kuhifadhi haki ya usawa wa binadamu,
heshima ya mtu itatunzwa katika shughuli zote
zinazohusu upelelezi na uendeshaji wa mambo ya
jinai na katika shughuli nyinginezo ambazo mtu
anakuwa chini ya ulinzi bila uhuru, au katika
kuhakikisha utekelezaji wa adhabu;
(e) ni marufuku kwa mtu kuteswa, kuadhibiwa kinyama
au kupewa adhabu zinazomtweza au kumdhalilisha.
Haki ya Kuishi
Haki ya kuwa hai Sheria ya 1984 Na.15 ib.6
14. Kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata kutoka kwa jamii
hifadhi ya maisha yake, kwa mujibu wa sheria.
Haki ya Uhuru wa mtu binafsi Sheria ya 1984 Na.15 ib.6
15.-(1) Kila mtu anayo haki ya kuwa huru na kuishi kama
mtu huru.
(2) Kwa madhumuni ya kuhifadhi haki ya mtu kuwa huru na
kuishi kwa uhuru, itakuwa ni marufuku kwa mtu yeyote
kukamatwa, kufungwa, kufungiwa, kuwekwa kizuizini,
kuhamishwa kwa nguvu au kunyang'anywa uhuru wake
vinginevyo, isipokuwa tu-
(a) katika hali na kwa kufuata utaratibu uliowekwa na
sheria, au
(b) katika kutekeleza hukumu, amri au adhabu
iliyotolewa na mahakama kutokana na mtu kutiwa hatiani kwa kosa la jinai.
No comments:
Post a Comment