Pichani ni mtangazaji wa kituo cha Television cha ITV Ufo Saro katika picha ya pamoja na Rais Jakaya Kikwete alipokutana na waandishi mbalimbali Ikulu Decemba 12, 2012 (Picha kutoka Maktaba)
Kuna taarifa kwamba mtangazaji wa kituo cha Television cha ITV (Ufo Saro) amepigwa risasi na kujeruhiwa vibaya huko maeneo ya Kibamba leo Alfajiri na mama yake mzazi kuuliwa. habari zaidi zinasema kwamba aliyefyatua Risasi hizo ni mchumba wa Mtangazaji huyo anayefanya kazi katika shirika moja la UN, ambaye baada ya tukio hilo naye alijipiga risasi na kujiua.
Maisha Times Blog inaendelea kufuatilia tukio hili la kuhuzunisha na punde itakuletea habari hii kwa kina. Endelea kuwa nasi.
Source: Breaking News - Radio One
Ripoti kamili ya mauwaji ya kinyama Mauaji ya kutisha
• MTANGAZAJI ITV APIGWA RISASI NA MCHUMBA WAKE
MTANGAZAJI wa kituo cha runinga cha ITV, Ufoo Saro amenusurika kifo baada ya kujeruhiwa vibaya kwa kupigwa risasi mbili tumboni na kifuani na mzazi mwenzake, Antel Mushi ambaye ni mhandisi wa mawasiliano kwenye kikosi cha Umoja wa Mataifa (UN) kinachofanya kazi nchini Sudan.
Katika tukio hilo la kutisha lililotokea jana saa 12:30 asubuhi, Mushi pia alimuua mama mzazi wa Ufoo kwa kumpiga risasi kifuani na kisha kujiua mwenyewe kwa kujipiga risasi eneo la kidevu, iliyomfumua kichwani.
Mauaji hayo yalitokea eneo la Kibamba, Njia panda ya Shule, nyumbani kwa mama mzazi wa mtangazaji huyo, Anastazia Salo (58) ambako wawili hao; Ufoo na mpenzi wake walikuwa wamefika muda mfupi kabla tukio.
Mushi na Ufoo wamezaa mtoto mmoja, Alvinen Mushi (10), na wakati wanatoka nyumbani kuelekea kwa mama mzazi wa mtangazaji huyo, walimuacha mtoto wao akiwa amelala na dada yake wa kazi.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, tukio hilo linahusishwa na ugomvi wa kifamilia ambao hadi sasa haujafahamika chanzo chake.
Shuhuda wa tukio hilo, Habelis Innocent ambaye ni ndugu wa karibu wa Ufoo, aliliambia gazeti hili kuwa mtangazaji huyo alijeruhiwa vibaya eneo la tumboni na mkononi.
Habelis alisema kuwa mapema alfajiri jana, Ufoo na Mushi waliondoka nyumbani kwao eneo la Magari Saba kuelekea Kibamba kwa mama wa Ufoo, kwamba wakiwa njiani mtangazaji huyo alimpigia mama yake simu na kumwambia aondoke nyumbani haraka.
Alisema kuwa Ufoo alimtaka mama yake kuondoka nyumbani kwa kuwa mchumba wake ana hasira, na hivyo anaweza kufanya fujo, lakini baada ya mama huyo kupata taarifa hizo hakuweza kuondoka haraka hadi walipofika.
Habelis alifafanua kuwa walipofika nyumbani hapo waligonga mlango na kisha mama yao kuwafungulia. Kwamba muda huo alikuwa anajiandaa kwenda kanisani, lakini hakuweza tena kuendelea na alichokua anakifanya, badala yake aliketi kuwasikiliza kilichowaleta.
Kwa mujibu wa shuhuda huyo, wakati mama, Ufoo na Mushi wakiwa sebuleni yeye alikuwa chumbani huku akisikia mazungumzo yaliyodhihirisha kulikuwa na mgongano ambao ulitakiwa kutafutiwa ufumbuzi.
Alisema kuwa wakati mazungumzo hayo yakiendelea, ghafla akasikia mlio wa risasi na sauti ya mama akiomba msaada kutoka kwake, akimtaka atoke haraka aliko ili kama kufa wafe wote.
Habelis alisema kuwa alipotoka alikuta tayari mama yake ameuawa na baadaye Mushi alimpiga risasi ya tumboni na mkononi Ufoo.
“Baada ya kushuhudia tukio hilo, nilianza kujihami na kukimbilia kwenye chumba kingine huku nikiwaambia wenzangu niliokuwa nimelala nao wasitoke nje.
“Wakati natafuta namna ya kujihami kwa kupanda darini, Mushi alipiga risasi nne mfululizo ili mlango ufunguke zinipate, lakini alishindwa na hivyo alihamia chumba alichokuwa mdogo wa Ufoo na kupiga risasi mbili mfululizo ili zimpate yoyote aliyekuwemo,” alisema.
Aliongeza kuwa wakati akipiga risasi hizo, vijana waliokuwa katika chumba hicho walifanya jitihada za kubomoa dari na kisha kupata upenyo wa kujificha darini na hatimaye Mushi akawakosa.
Aliwataja wenzake hao waliokoswakoswa na risasi katika tukio hilo kuwa ni Godluck Saro na Jonasi Saro na kuongeza kuwa baadaye Mushi alikimbilia jikoni na kukuta jiko la gesi, aliwasha na kuchoma nguo ili nyumba ilipuke waliomo ndani wateketee.
Shuhuda huyo alisema kuwa baada ya kuchoma nguo, Mushi alirudi sebuleni na kisha kujimalizia mwenyewe kwa kujipiga risasi na kupoteza maisha papo hapo.
Ufoo alikimbizwa Hospitali ya Tumbi, Kibaha ambako alipatiwa huduma ya kwanza na kuhamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, uchunguzi wa awali uliofanyika katika gari alilotumia Mushi walikuta begi likiwa na kompyuta ndogo (laptop), kamba za kujinyongea, panga, pingu, kisu na risasi.
Akizungumza na waandishi wa habari hospitalini Muhimbili, Kova alisema kwa mujibu wa madaktari, hali ya mgonjwa ilikuwa inaendelea vizuri na alikuwa akitarajiwa kufanyiwa upasuaji nyakati za mchana.
Kova alisema japo mhusika alijiua baada ya kumuua mkwewe na kumjeruhi kwa risasi Ufoo, bado kitendo hicho hakiliondolei jeshi hilo kuchunguza tukio hilo.
Alisema kuwa wanatarajia Ufoo atakuwa miongoni mwa watu watakaolisaidia jeshi hilo kupata taarifa zaidi za tukio hilo.
Naye, ofisa upelelezi wa makosa ya jinai, Ahmed Msangi alisema hadi sasa hakuna taarifa kamili, bali jeshi limejigawa sehemu tatu, kila kundi likikusanya taarifa.
Alisema baada ya makundi hayo ambayo yalikuwa katika maeneo ya nyumbani lilikotokea tukio, Tumbi hospitali na Muhimbili, kukusanya taarifa watazitoa kwa waandishi wa habari.
Naye Mwenyekiti Mtendaji wa makampuni ya IPP, Reginald Mengi alisema kipindi hicho madaktari walikuwa wakiendelea na uchunguzi kwa ajili ya kukamilisha upasuaji.
Alisema kuwa hali yake Ufoo sio mbaya bali ilikuwa inaendelea vizuri akiwa chini ya uangalizi wa madaktari
Kisa mapenzi!
ReplyDeleteChezea penzi
ReplyDelete