Advertise with Us

Advertise with Us

DHall

DHall

Pages

April 12, 2014

Hotuba ya Tundu Lissu iliyokatishwa kwa makusudi na TBC- Sehemu ya Pili!

Mjumbe wa Bunge maalum la Katiba Mhe. Tundu Lissu alipokuwa akitoa Hotuba ya Maoni ya walio wachache kutoka katika Kamati Na. 4 kabla ya Kukatiwa matangazo na Kituo cha matangazo cha TBC 

<<<<<<<<<< Sehemu ya Pili >>>>>>>>

EXIT ‘TANGANYIKA’ ENTER ‘TANZANIA’!

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Kuna sababu nyingine ya kuacha kutumia jina la ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.’ Sababu hiyo ni utata wa kisheria na kikatiba ambao umegubika jina la ‘Tanzania’ tangu lilipoanza kutumiwa nusu karne iliyopita. Ili kufahamu vyema jambo hili ni vizuri kuanzia ‘Hati ya Kuzaliwa ya Muungano’, yaani Hati ya Makubaliano ya Muungano. Kwa maudhui yake, Hati hiyo inaonyesha wazi kwamba jina la Jamhuri mpya itakayoundwa kwa mujibu wake ni ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.’

Jina hili linathibitishwa na Sheria ya Kuthibitisha Mapatano ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, iliyotungwa na Bunge la Jamhuri ya Tanganyika, siku tatu tu baada ya Hati ya Muungano kusainiwa: “Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar zitakuwa, kuanzia Siku ya Muungano na milele baada ya hapo, zimeungana kuwa Jamhuri moja yenye mamlaka kamili itakayoitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.”

Sheria hiyo ilitungwa na Bunge Maalum, sio na Bunge la kawaida, na kwa sababu hiyo ina haiba ya katiba. Ndio maana tangu mwaka 1965 kwenye Katiba ya Muda, na hadi sasa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano, Sheria hiyo ni Nyongeza kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano na haiwezi kubadilishwa bila kuungwa mkono na theluthi mbili ya wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wakikaa kama wajumbe wa Bunge Maalum.

Hata hivyo, mnamo tarehe 3 Disemba, 1964, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar – likiwa limekaa kama Bunge la kawaida - lilitunga Sheria ya Kutangaza Jina la Jamhuri ya Muungano, ya mwaka 1964, yaani, The United Republic (Declaration of Name) Act, 1964. Sheria hiyo ilibadilisha masharti ya kifungu cha 4 cha Sheria ya Kuthibitisha Mapatano ya Muungano ambacho kilitangaza jina la Jamhuri ya Muungano kuwa ni ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.’

Kifungu cha 2(1) cha Sheria hiyo mpya kilitamka kwamba: “Bila kujali masharti ya kifungu cha 4 cha Sheria za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, inatangazwa kwamba kuanzia sasa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar itajulikana kama Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sheria zilizopo za Tanganyika na Zanzibar zitatafsiriwa hivyo hivyo.” Mabadiliko haya ya jina la Jamhuri ya Muungano ni mfano mwingine wa utamaduni wa ukiukaji sheria (culture of illegality) ambao umegubika Muungano huu tangu siku ya kwanza ya kuzaliwa kwake:

(a) Kwa mujibu wa aya ya (iv) ya Hati ya Makubaliano ya Muungano, Bunge la Jamhuri ya Muungano halikuwa na mamlaka ya kubadilisha jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar;
(b) Kwa kuwa Sheria ya Kuthibitisha Mapatano ya Muungano ilitungwa na Bunge Maalum, na kwa hiyo ina haiba ya Katiba, Sheria ya Kutangaza Jina la Jamhuri ya Muungano – ambayo ni sheria ya kawaida – ni batili kwa vile na kwa kiasi inavyokinzana na Sheria ya Kuthibitisha Mapatano ya Muungano;
(c) Jina la ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanzania’ lilianza kutumiwa hata kabla ya Sheria ya Kutangaza Jina la Jamhuri ya Muungano kutungwa:
(i) Kifungu cha 2(2) cha Sheria hiyo kinasema kwamba “kutajwa kwa Jamhuri ya Muungano kama Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kipindi chochote kati ya tarehe ishirini na nane ya Oktoba, 1964 na kuanza kutumika kwa Sheria hii kutachukuliwa kuwa ni kutajwa kihalali na muafaka na uhalali wa tendo lolote hautahojiwa kwa sababu tu ya matumizi ya (jina hilo) badala ya lile la Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.” Hii inadhihirisha kwamba jina la ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanzania’ lilianza kutumika tarehe 28 Oktoba, 1964, bila ya uhalali wowote wa kisheria;
(ii) Tarehe 2 Novemba, 1964, yaani mwezi mmoja kabla ya Sheria ya Kutangaza Jina la Jamhuri ya Muungano kutungwa, Ubalozi wa Kudumu wa Jamhuri ya Tanganyika katika Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani, ulimtumia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa waraka wa kidiplomasia (note verbale) ukimjulisha kwamba “Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kuanzia sasa, itajulikana kama Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”
Waraka huo haukuwa na jina, cheo wala sahihi ya Ofisa wa Ubalozi wa Kudumu aliyeutuma lakini uligongwa muhuri wenye nembo ya taifa iliyoandikwa ‘Jamhuri ya Tanganyika.’ Kifungu cha 12 cha Sheria ya Nembo za Taifa, yaani National Emblems Act, Sura ya 10 ya Sheria za Tanzania, kinaelekeza kwamba “popote nembo ya taifa inapotumiwa katika waraka au kitu chochote, matumizi hayo yatahalalishwa au kuthibitishwa na sahihi ya mtunzaji wa nembo hiyo.”

Kwa vile note verbale iliyomjulisha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa juu ya mabadiliko ya jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliwekewa nembo ya taifa ya Tanganyika bila kusainiwa na mtunzaji wa nembo hiyo, ni wazi kwamba note verbale hiyo haikuwa na uhalali wowote.

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Kwa sababu ya mazingira ya kisiasa ya utawala wa kiimla wa chama kimoja, kwa miaka mingi ilikuwa vigumu kuhoji uhalali wa matumizi ya jina la ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.’ Hata hivyo, wapo watu wachache ambao wamehoji uhalali wa jina hili. Hivyo, kwa mfano, marehemu George Liundi, aliyekuwa Msajili wa Vyama vya Siasa wa kwanza mara baada ya kurudishwa kwa mfumo wa vyama vya siasa nchini aliwahi kusema yafuatayo katika Kongamano la Vyama vya Siasa lililofanyika katika Hotel ya Golden Tulip, Dar es Salaam, kati ya tarehe 12-14 Disemba, 2002:

“Prior to the enactment of the Interim Constitution of 1965, another constitutional problem appears to have been created by the change of name of the United Republic of Tanganyika and Zanzibar to the United Republic of Tanzania, with effect from 11th December 1964.... This change of name calls for scrutiny, because on the face of it the measure appears to have put into question the constitutional status (in terms of national sovereignty) of both the territories formerly constituting the Republic of Tanganyika and Zanzibar respectively.”

Kwa maneno mengine:

“Kabla ya kutungwa kwa Katiba ya Mpito ya 1965, tatizo lingine la kikatiba linaelekea lilitengenezwa na mabadiliko ya jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwenda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuanzia tarehe 11 Disemba, 1964.... Mabadiliko haya ya jina yanahitaji kuchunguzwa kwa sababu, kwa juu juu tu hatua hii inaonekana ilihoji hadhi ya kikatiba (kwa maana ya uhuru wa kitaifa) wa maeneo ambayo yalijumuisha Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar.”

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Ni wazi, kwa misingi hii ya kisheria, jina la ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanzania’ ni batili kisheria, licha ya ukweli kwamba limetumika kwa nusu karne. Kwa maoni yetu, kama kweli tunaamini – kama inavyopendekeza Tume - kwamba ‘msingi mkuu’ wa Jamhuri ya Muungano ni Hati ya Makubaliano ya Muungano, wakati umefika wa kuyaheshimu Makubaliano ya Muungano kwa kurudisha matumizi ya jina lililotumiwa katika Makubaliano hayo, yaani Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

‘HATI YA MAKUBALIANO YA MUUNGANO’

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Tarehe 22 Aprili, 1964 Rais wa Jamhuri ya Tanganyika, Mwalimu Julius K. Nyerere, na Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, Sheikh Abedi Amani Karume walitia saini Hati ya Makubaliano ya Muungano kati ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Hati hiyo ndiyo inayotajwa katika ibara ya 1(1) na (3) ya Rasimu. Wakati wa mjadala wa Sura ya Kwanza na ya Sita, wajumbe wa Kamati Namba Nne – kama ilivyokuwa kwa wajumbe wa Kamati nyingine za Bunge lako tukufu – waliletewa nakala ya Sheria ya Kuthibitisha Mapatano ya Muungano, Sheria Na. 22 ya 1964, yaani The Union of Tanganyika and Zanzibar Act, Sura ya 557 ya Sheria za Tanzania. Nakala ya Sheria hiyo ilitolewa baada ya baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalum kuomba kupatiwa nakala halisi ya Hati ya Makubaliano ya Muungano iliyosainiwa na Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume.

Ijapokuwa nakala ya Sheria ya Kuthibitisha Mapatano ya Muungano waliyogawiwa wajumbe imeambatanisha Hati ya Makubaliano ya Muungano kati ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar kama Nyongeza ya Sheria hiyo, hicho sicho walichoomba wajumbe wa Bunge Maalum. Nakala ya Sheria ya Kuthibitisha Mapatano ya Muungano sio, na haiwezi kuwa, mbadala wa nakala halisi ya Hati ya Makubaliano ya Muungano. Hii ni kwa sababu, Nyongeza ya Sheria waliyogawiwa wajumbe – ambayo inadaiwa kuwa ndio Hati ya Makubaliano ya Muungano - haina saini za Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume. Ni vigumu, kwa hiyo, kuthibitisha kama kweli kile kinachodaiwa kuwa ni Hati ya Makubaliano ya Muungano ndicho hicho walichokubaliana waasisi hao wa Muungano kwa kutia saini zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Suala la kushindwa kupatikana kwa nakala halisi ya Hati ya Makubaliano ya Muungano sio jambo dogo. Suala hili ndio ufunguo wa kuelewa mgogoro mkubwa wa kikatiba na kisiasa ambao umeugubika Muungano katika nusu karne ya maisha yake. Hii ni kwa sababu, katika kipindi chote hicho, kumekuwa na mgogoro mkubwa kuhusu kitu gani hasa Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume walikubaliana kwa niaba ya nchi zao. Bila kupatikana kwa nakala halisi ya Hati, uhalali mzima wa Muungano wenyewe, na wa mambo yote yaliyofanyika kwa jina la Muungano kwa takriban nusu karne, unakuwa kwenye mashaka makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Siku moja baada ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kuzaliwa, yaani tarehe 27 Aprili 1964, Mwanasheria Mkuu na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. C.A. Stavropoulos alimwandikia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. U Thant, waraka wa kiofisi uliohusu ‘Uanachama Katika Umoja wa Mataifa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.’ Kwa mujibu wa Bw. Stavropoulos, waraka wake ulitokana na taarifa za vyombo vya habari zilizoonyesha kwamba Tanganyika na Zanzibar, ‘ambazo kabla zilikuwa wanachama tofauti wa Umoja wa Mataifa’, zilikuwa zimeungana na kuunda dola moja yenye uwakilishi wa pamoja nchi za nje. Kwa vile Serikali za Jamhuri ya Tanganyika na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar zilikuwa hazijapeleka taarifa rasmi Umoja wa Mataifa juu ya Muungano wa nchi zao, Bw. Stavropoulos alipendekeza kwamba “mwakilishi wa Tanganyika ataarifiwe juu ya haja ya kupata tamko rasmi kutoka kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano ... kuhusu kuanzishwa kwa Jamhuri hiyo ... na hati mpya za utambulisho wa mwakilishi mmoja kutoka Jamhuri (ya Muungano). (Itakuwa vizuri vile vile kwa mwakilishi husika kutupatia nakala ya makubaliano yaliyopelekea Muungano huo.)”

Ijapokuwa tarehe 6 Mei, 1964, Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ilipeleka taarifa ya maandishi iliyodai kuambatanisha nakala ya Hati ya Makubaliano ya Muungano, kuna mashaka ya msingi kama kweli Hati hiyo ilipelekwa Umoja wa Mataifa. Hii ni kwa sababu, tarehe 14 Mei, 1964, yaani wiki moja baadae na takriban wiki tatu baada ya Muungano, Bw. Stavropoulos alimwandikia Deputy Chief de Cabinet wa Umoja wa Mataifa Bw. Jose Rolz-Bennett kumwelekeza apeleke ujumbe wa simu ya maandishi kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, kuhusu masharti ya kusajili Hati ya Makubaliano ya Muungano katika Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa kama inavyotakiwa na ibara ya 102 ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa. “... Serikali inayosajili inatakiwa kuwasilisha kwa Sekretarieti nakala moja ya Makubaliano iliyothibitishwa kwamba ni nakala ya kweli na kamili ... nakala mbili za ziada na taarifa inayohusu tarehe na namna ya kutiliwa nguvu Makubaliano hayo.”

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Sasa kuna uthibitisho kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano haijawahi kuwasilisha Hati ya Makubaliano ya Muungano katika Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa. Tarehe 25 Machi 2009, Afisa Habari za Kisheria kwenye Kitengo cha Mikataba ya Kimataifa katika Ofisi inayoshughulikia masuala ya kisheria ya Umoja wa Mataifa Bw. Andrei Kolomoets, alimtaarifu mtafiti mmoja kwa maandishi kwamba: “Hakuna ushahidi wowote kwamba Hati ya Makubaliano ya Muungano ilisajiliwa kwenye Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa. Kama ingesajiliwa, kungelikuwa na hati ya usajili iliyoambatanishwa. Nimeangalia, hakuna kitu hicho.”

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Kwa miaka yote hamsini ya Muungano, nakala ya Hati ya Makubaliano ya Muungano haijawahi kuonyeshwa hadharani. Aidha, hata ilipodaiwa mahakamani katika Mahakama Kuu ya Zanzibar, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Iddi Pandu Hassan, alisema katika barua yake ya tarehe 22 Juni, 2005 kwamba: “Ofisi yangu haikuweka kumbu kumbu ya nakala ya mkataba wa asili (original) wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hapo tarehe 26 Aprili, 1964.”

Kwa ushahidi huu kutoka Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, na wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, hakuna shaka tena kwamba Hati ya Makubaliano inayozungumzwa katika ibara 1(1) na (3) ya Rasimu haijawahi kuwepo. Hii ndio kusema kwamba hakuna ajuaye ni kitu gani hasa Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume walisaini siku hiyo ya tarehe 22 Aprili, 1964. Kwa maoni yetu, hiki ndio chanzo cha sintofahamu na migogoro yote kuhusu Muungano huu.

UTEKELEZAJI WA ‘MAKUBALIANO YA MUUNGANO’

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Hata kama tukikubali, in arguendo, kwamba kile kilichopo kwenye Sheria ya Kuthibitisha Mapatano ya Muungano ndio Hati yenyewe ya Makubaliano ya Muungano, bado kuna hoja kubwa na ya msingi kwamba Hati hiyo haiwezi kuwa msingi wa Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar tunalolipendekeza. Hii ni kwa sababu, katika miaka hamsini tangu kusainiwa kwa Hati ya Makubaliano ya Muungano na kuzaliwa kwa Muungano, Makubaliano hayo yamechakachuliwa na kuvunjwa karibu kila mahali na kwa kipindi chote cha kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano. Kabla hatujaanika uchakachuaji huu, ni muhimu tuyarejelee masharti yaliyomo kwenye hiyo inayoitwa Hati ya Makubaliano ya Muungano.

Aya ya (i) ya Hati ya Makubaliano inatamka kwamba “Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar zitaungana na kuwa Jamhuri moja huru.” Aya ya (ii) inaweka Kipindi cha Mpito cha kuanzia tarehe ya kuanza kwa Muungano hadi tarehe ya Bunge Maalum kukutana na kupitisha Katiba kwa ajili ya Jamhuri ya Muungano. Katika kipindi hicho “... Jamhuri ya Muungano itaongozwa kwa mujibu wa masharti ya aya za (iii) hadi (vi) za Hati ya Makubaliano.”

Masharti hayo ni kuwa katika kipindi hicho cha mpito, Jamhuri ya Muungano itaongozwa na Katiba ya Tanganyika ambayo itarekebishwa ili kuwezesha kuwepo kwa bunge na serikali ya na kwa ajili ya Zanzibar ambayo itaundwa kwa mujibu wa sheria za Zanzibar na yenye mamlaka kamili ndani ya Zanzibar kwa mambo yote isipokuwa kwa mambo ambayo yametengwa kwa ajili ya Bunge na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Aidha, kutakuwa na Makamu wawili wa Rais ambapo mmoja wao (ambaye kwa kawaida ni mkazi wa Zanzibar) atakuwa Mkuu wa Serikali ya na kwa ajili ya Zanzibar na atakuwa msaidizi mkuu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano katika utekelezaji wa majukumu yake kuhusu Zanzibar. Vile vile, kutakuwa na uwakilishi wa Zanzibar katika Bunge la Jamhuri ya Muungano; na mambo mengine yatakayohitajika ili kuipa uwezo Jamhuri ya Muungano na Hati za Muungano.

Masharti mengine ni kuwapo kwa orodha ya Mambo ya Muungano ambayo Bunge na Serikali ya Jamhuri ya Muungano zilipewa mamlaka kamili kwa Jamhuri ya Muungano yote nje ya mamlaka yake kamili kwa mambo yasiyokuwa ya Muungano ya na kwa ajili ya Tanganyika. Mambo ya Muungano ni pamoja na Katiba na Serikali ya Jamhuri ya Muungano; mambo ya nje; ulinzi; polisi; mamlaka ya hali ya hatari; uraia; uhamiaji; biashara ya nje na mikopo; utumishi wa umma wa Jamhuri ya Muungano; kodi ya mapato, kodi ya mashirika na ushuru wa forodha na wa bidhaa; na bandari, usafiri wa anga, posta na simu.

Masharti mengine ni kwamba sheria zilizokuwepo Tanganyika na Zanzibar kabla ya Muungano zitaendelea kutumika ‘katika maeneo yao’ hadi hapo zitakaporekebishwa ili kutilia nguvu Muungano na Hati za Muungano; au sheria mpya zitakapotungwa na mamlaka husika au kutolewa kwa amri ya Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa ajili ya utekelezaji wa Mambo ya Muungano kwa upande wa Zanzibar. Masharti ya mwisho ni kutangazwa kwa Mwalimu Julius K. Nyerere kuwa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano, na Sheikh Abeid Karume kuwa Makamu wa Rais kutoka Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Kwa mujibu wa aya ya (vii) ya Hati ya Muungano, Rais wa Jamhuri ya Muungano alipaswa, kwa makubaliano na Makamu wa Kwanza wa Rais, kuteua Tume kwa ajili ya kuandaa Katiba ya Jamhuri ya Muungano; na kuitisha Bunge Maalum lenye wawakilishi kutoka Tanganyika na kutoka Zanzibar na kwa idadi watakayoamua kwa lengo la kujadili na kupitisha Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Bunge hilo Maalum lilitakiwa kuitishwa ndani ya kipindi cha mwaka mmoja kuanzia tarehe ya kuzaliwa Muungano, yaani tarehe 26 Aprili, 1964. Hiki ndicho kilikuwa kipindi cha mpito kinachotajwa katika aya ya (ii) ya Hati ya Makubaliano.

Aya ya (viii) na ya mwisho ya Hati ya Makubaliano ililazimu Hati ya Makubaliano ya Muungano kuthibitishwa kwa Bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi na Baraza la Mawaziri la Zanzibar kutunga sheria za kuridhia Hati ya Makubaliano na kuanzishwa kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na ya Zanzibar kwa mujibu wa Hati ya Makubaliano.

HISTORIA YA UCHAKACHUAJI

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Sasa tunaomba tuthibitishe hoja yetu kwamba miaka hamsini ya Hati ya Makubaliano ya Muungano na ya Muungano ni nusu karne ya uchakachuaji na ya nchi yetu kuishi kwa uongo na ujanja ujanja:

1. Wakati Bunge la Tanganyika liliitishwa kwa dharura tarehe 25 Aprili, 1964 ili kupitisha sheria ya kuthibitisha Hati ya Makubaliano ya Muungano, na lilipitisha Sheria ya Kuthibitisha Mapatano ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, upo ushahidi wa kutosha kwamba Baraza la Mapinduzi na Baraza la Mawaziri la Zanzibar halijawahi kutunga sheria yoyote ya kuthibitisha Hati ya Makubaliano ya Muungano kwa kipindi chote cha maisha ya Muungano huu:
(a) Profesa Issa G. Shivji katika kitabu chake Pan Africanism or Pragmatism? Lessons of Tanganyika – Zanzibar Union amethibitisha kwamba kile kinachoitwa Sheria ya Kuthibitisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ya mwaka 1964 “... iliandaliwa na kuandikwa na maafisa wa sheria wa Tanganyika wakiwa Tanganyika.... Hii ni kwa sababu ya ukweli wa kisiasa uliokuwapo wakati huo ambapo Baraza la Mapinduzi kwa ujumla wake halikuukubali Muungano. Hakuna shaka kwamba Muungano ‘ulilazimishwa.’ Hivyo, maafisa wa kisheria wa kigeni wa Serikali ya Tanganyika (waliokuwa pia marafiki wa Nyerere) walitumia mbinu ya kisheria ya kuchapisha Sheria ya Kuthibitisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, 1964, (inayodaiwa kutungwa na Baraza la Mapinduzi Zanzibar) waliyoitengeneza wao, katika Gazeti rasmi la Serikali ya Jamhuri ya Muungano chini ya saini ya (Kaimu Mwanasheria Mkuu wa Tanganyika) P.R. Nines Fifoot.”
(b) Aliyekuwa Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu wa Baraza la Mwaziri wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar kati ya tarehe 18 Januari na Juni 1964, Salim Said Rashid ametamka yafuatayo kwa kiapo cha tarehe 22 Aprili 2006:
(i) Kwamba hakuwahi “... kupokea maagizo kutoka kwa Rais wa Zanzibar kwa ajili ya kuitisha kikao cha kujadili na kupitisha mkataba wa kuunganisha Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika.”
(ii) Kwamba “suala la kuunganisha Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika halikuwahi kujadiliwa na kikao chochote cha Baraza la Mapinduzi na Baraza la Mawaziri la Serikali ya Zanzibar au kujadiliwa na taasisi yoyote ya Serikali ya Zanzibar.”
(iii) Kwamba anakumbuka “... kupokea maagizo kutoka kwa Rais wa Zanzibar kuwa anataka kuufanya Muungano na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika na baadae alinionyesha mapendekezo ya rasimu ya Muungano kati ya Jamhuri ya (Watu wa) Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika.”
(iv) Kwamba “... rasimu hiyo ililetwa na Mawaziri kutoka Serikali ya Jamhuri ya Tanganyika na kukabidhiwa Rais ikiwa tayari imeshaandikwa kuunganishwa Jamhuri hizi mbili.”
(v) Kwamba baada ya kuonyeshwa mapendekezo hayo ya Muungano, “... niliagizwa na Rais wa Zanzibar nisimwonyeshe mtu yoyote na wala asipewe Mwanasheria wa Serikali ya Zanzibar.”
(vi) Kwamba “... sikupata maagizo yoyote kutoka kwa Rais ili kuwajulisha viongozi wa Baraza la Mapinduzi juu ya kuitisha kikao au kuja kushuhudia makubaliano ya kuunganisha nchi ya Zanzibar yakitiwa sahihi.”
(vii) Kwamba, kwa sababu hiyo, “... hakuna shughuli yoyote au kikao kilichofanyika kwa ajili ya kutia saini mkataba wa Muungano kwa mujibu wa decree Na. 5 ya mwaka 1964 ya Serikali ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.”
(viii) Bw. Rashid anaelezea utaratibu wa kisheria uliotakiwa kufuatwa: “... Kwa mujibu wa Presidential Decree ya 1964, kila jambo lilitakiwa kujadiliwa na kikao cha Baraza la Mapinduzi na kuarifiwa Mwanasheria Mkuu atayarishe presidential decree kwa mujibu wa utaratibu na baadae sisi tusaini nikiwa mimi Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Baraza la Mawaziri Zanzibar na asaini Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na baadae kutolewa katika official gazette (gazeti rasmi la serikali) huo ndio ulikuwa utaratibu.”
(ix) Kwamba kwa sababu utaratibu huo ulikiukwa, “... kitendo cha kuunganisha Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika hakikupata Baraka za Baraza la Mapinduzi na kuthibitishwa na kikao halali cha Baraza la Mawaziri la Zanzibar.”
(c) Katika kitabu chake The Partner-ship, Alhaj Aboud Jumbe amesema yafuatayo kuhusu kusainiwa kwa Makubaliano ya Muungano:
(i) “Ilikuwa ni asubuhi ya Aprili 22, 1964 pale Julius Kambarage Nyerere alipowasili Zanzibar. Rais huyo wa Jamhuri ya Tanganyika alikuja na nakala ya mapendekezo ya Mkataba uliotayarishwa Tanganyika na ulioandikwa kwa lugha ya Kiingereza. Waraka huo uliwakilisha jumla ya makubaliano ambayo yalifikiwa siku hiyo hiyo baina ya Rais wa Jamhuri ya Tanganyika, Julius Nyerere na Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, Abedi Amani Karume. Makubaliano hayo kwanza kabisa yalitiwa sahihi katika Ikulu ya Zanzibar na hapo baadae kuwa ndio Mkataba wa Muungano, 1964.”
(ii) Aidha, “mimi nilikuwa Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi, kwa wakati mmoja au mwengine, kwa cheo kimoja au chengine kutokea kuanzishwa kwa Baraza hilo hapo Januari 1964 hadi mwaka 1984 na nimeshindwa katika kumbukumbu zangu kupata ushahidi wa kufanyika kikao cha Baraza la Mapinduzi kama ni Zanzibar au Dar es Salaam ili kuthibitisha Mkataba wa Muungano.”
Kwa hiyo, Makubaliano ya Muungano yalipata ridhaa ya upande mmoja tu, yaani Watanganyika kwa kupitia Bunge lao, wakati Wazanzibari kwa kupitia Bunge lao, yaani Baraza la Mapinduzi, hawakuwahi kutoa ridhaa yao kwa Muungano huu. Ni wazi, kwa hiyo, kwamba - kwa sababu hiyo - Jamhuri ya Muungano ilizaliwa bila uhalali wowote wa kisheria. Kwa maneno ya Profesa Shivji, “Hakuna shaka kwamba Muungano ‘ulilazimishwa.’”

(d) Katika kitabu chake kiitwacho 50 Years of Independence: A Concise Political History of Tanzania, kilichochapishwa Januari ya mwaka huu 2014, Mzee Pius Msekwa, Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM na Katibu Mtendaji wake wa kwanza amesema yafuatayo kuhusu mambo yaliyofanyika baada ya Makubaliano ya Muungano kusainiwa:
(i) Tarehe 26 Aprili, 1964, yaani Siku ya Muungano, Rais Nyerere alitunga Presidential Decree (Amri ya Rais) iliyoitwa The Transitional Provisions Decree, 1964, yaani, Amri ya Masharti ya Mpito ya mwaka 1964, iliyochapishwa katika Gazeti la Serikali la siku hiyo. “Amri hiyo iliwabadilisha watu waliokuwa watumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Tanganyika na kuwafanya watumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Mahakama Kuu ya Tanganyika iligeuzwa kuwa Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano; na nembo ya taifa ya Jamhuri ya Tanganyika iligeuzwa kuwa nembo ya taifa ya Jamhuri ya Muungano.”
(ii) Tarehe hiyo hiyo, Rais Nyerere alitunga Amri nyingine ya Rais iliyoitwa The Interim Constitution Decree, 1964, yaani, Amri ya Katiba ya Muda ya mwaka 1964. “Amri hii iliitangaza Katiba ya Tanganyika kuwa ndiyo Katiba ya Muda ya Jamhuri ya Muungano. Kifungu cha 4 cha Amri hii ndicho kilichoipatia Serikali ya Muungano majukumu kuhusu mambo yote ya Muungano katika Jamhuri ya Muungano yote na vile vile kwa mambo yasiyokuwa ya Muungano kwa upande wa Tanganyika.”
(iii) Tarehe 15 Juni 1964 Mwalimu Nyerere alitunga Amri nyingine tena iliyoitwa The Transitional Provisions (No. 2) Decree, 1964, yaani, Amri ya Masharti ya Mpito (Na. 2) ya mwaka 1964. Amri hii ilielekeza kwamba mahali popote ambapo sheria zilizopo zimetaja jina la ‘Tanganyika’ basi jina hilo lifutwe na badala yake jina la ‘Jamhuri ya Muungano’ liwekwe. Vile vile, Amri hiyo ilielekeza, mahali popote ambapo ‘Serikali ya Tanganyika’ imetajwa, au kwenye jambo au kitu chochote ambacho kwa namna yoyote kinamilikiwa au kinahusishwa na Serikali hiyo, basi itachukuliwa kuwa ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano ndiyo iliyotajwa.
(iv) Kwa maneno ya Mzee Msekwa mwenyewe: “Tanganyika was thus decreed out of existence. The cumulative effect of these legislative measures was that the political entity which was Tanganyika, was decreed totally out of existence. That is the reason why even the name of the geographical unit formerly known as Tanganyika, had to be changed to Tanzania Mainland.” Tafsiri ya maneno haya ni kwamba “uhai wa Tanganyika ulitolewa kwa njia hiyo ya amri. Athari za jumla za Amri hizi ni kwamba eneo la kisiasa ambalo ndio ilikuwa Tanganyika lilitolewa uhai wake moja kwa moja kwa amri. Hii ndiyo sababu hata jina la eneo la kijiografia lililojulikana zamani kama Tanganyika ilibidi libadilishwe na kuwa Tanzania Bara.”
2. Vitendo vya kuivika Jamhuri ya Tanganyika joho la Muungano na kuigeuza kuwa ndio Jamhuri ya Muungano hakikuwa na uhalali wowote kwa mujibu wa Makubaliano ya Muungano:
(a) Aya ya (v) ya Hati ya Makubaliano ya Muungano ilitamka wazi kwamba “sheria zilizopo za Tanganyika na za Zanzibar zitaendelea kutiliwa nguvu katika maeneo yao....” Kwa maana hiyo:
(i) Rais Nyerere hakuwa na mamlaka yoyote kwa mujibu wa Makubaliano ya Muungano wala chini ya Katiba na Sheria za Tanganyika ya kugeuza sheria zote za Jamhuri ya Tanganyika kuwa sheria za Jamhuri ya Muungano hata kwa mambo yasiyokuwa ya Muungano;
(ii) Rais Nyerere hakuwa na mamlaka yoyote kwa mujibu wa Makubaliano ya Muungano wala kwa mujibu wa Katiba na Sheria za Tanganyika ya kuwageuza watumishi wote wa Jamhuri ya Tanganyika kuwa watumishi wa Jamhuri ya Muungano hata kwa mambo yasiyokuwa ya Muungano;
(iii) Rais Nyerere hakuwa na mamlaka yoyote kwa mujibu wa Makubaliano ya Muungano au kwa mujibu wa Katiba na Sheria za Tanganyika ya kugeuza Mahakama Kuu ya Tanganyika kuwa Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano;
(iv) Rais Nyerere hakuwa na mamlaka yoyote kwa mujibu wa Makubaliano ya Muungano au kwa mujibu wa Katiba na Sheria za Tanganyika ya kugeuza Nembo ya Taifa ya Jamhuri ya Tanganyika kuwa Nembo ya Taifa ya Jamhuri ya Muungano. Nembo za Taifa, yaani ‘Bibi na Bwana’ inayotumika hadi leo hii ni Nembo ya Taifa ya Jamhuri ya Tanganyika!
(v) Rais Nyerere hakuwa na mamlaka yoyote kwa mujibu wa Makubaliano ya Muungano au kwa mujibu wa Katiba na Sheria za Tanganyika ya kufuta matumizi ya jina la Tanganyika katika sheria zote za Jamhuri ya Tanganyika au katika mambo au vitu vyote vilivyokuwa vinamilikiwa ama kuhusishwa na Jamhuri ya Tanganyika hata kwa mambo yasiyokuwa ya Muungano ya Tanganyika;
(vi) Rais Nyerere hakuwa na mamlaka yoyote kwa mujibu wa Makubaliano ya Muungano au kwa mujibu wa Katiba na Sheria za Tanganyika ya ‘kutoa uhai wa nchi ya Tanganyika kwa njia ya Amri ya Rais’ au kwa njia nyingine yoyote ya kisheria na kuigeuza kuwa Jamhuri ya Muungano.
MAMBO YA MUUNGANO NA KUMEZWA KWA ZANZIBAR

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Kama tulivyokwishaonesha, kwa mujibu wa aya ya (iv) ya Makubaliano ya Muungano na kifungu cha 5(1) cha Sheria ya Kuthibitisha Mapatano ya Muungano, Mambo ya Muungano yaliyokubaliwa kwenye Makubaliano ya Muungano yalikuwa kumi na moja. Haya ni mambo yaliyoko katika vipengele vya 1 hadi 11 vya Nyongeza ya Kwanza ya Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano.

Hata hivyo, kati ya mwaka 1964 and 1973 mambo mengine sita – yanayoonekana katika vipengele 12 hadi 16 vya Nyongeza ya Kwanza – yaliongezwa katika orodha ya Mambo ya Muungano. Hivyo basi, mwaka 1965 masuala ya fedha, sarafu na benki yaliongezwa; mwaka 1967 leseni ya viwanda na takwimu, elimu ya juu na mambo yaliyokuwa katika Nyongeza ya X ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yaliongezwa; mwaka 1968 yaliongezwa mambo ya maliasili ya mafuta, petroli na gesi asilia; na mwaka 1973 mambo yanayohusu Baraza la Mitihani la Taifa yaliongezwa.

Aidha, Mabadiliko ya Tano ya Katiba ya mwaka 1984 yaligawa kipengele cha Nyongeza ya X ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kutengeneza vipengele vinne vinavyojitegemea katika orodha ya Mambo ya Muungano, yaani usafiri na usafirishaji wa anga, utafiti, utabiri wa hali ya hewa na takwimu. Vile vile, Mabadiliko hayo yaliongeza kitu kipya katika orodha ya Mambo ya Muungano: Mahakama ya Rufani ya Tanzania. Aidha, kipengele cha 3, yaani ulinzi, kilifanyiwa marekebisho na kuwa ‘ulinzi na usalama.’ Na mwaka 1992 ‘uandikishwaji wa vyama vya siasa’ nao uliongezwa katika orodha ya Mambo ya Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Mambo yote yaliyoongezwa katika orodha ya Mambo ya Muungano baada ya mwaka 1964 yalikuwa nje ya Makubaliano ya Muungano na nje ya Sheria ya Mapatano ya Muungano na kwa hiyo yalikuwa batili. Hii ni kwa sababu Sheria ya Mapatano ya Muungano – na sio Katiba za Muda za 1964 au 1965 au ya sasa - ndio Sheria Mama iliyozaa Muungano na kuweka mgawanyo wa madaraka kati ya mamlaka za Jamhuri ya Muungano na mamlaka za Zanzibar. Sheria ya Mapatano ya Muungano ilitungwa na Bunge la Katiba tofauti na sheria za kawaida.

Aidha, Katiba ya Muda, 1965 iliyotawala Tanzania hadi 1977 iliiweka Sheria ya Mapatano ya Muungano kama Nyongeza ya Pili katika Katiba na kuweka masharti kwamba Sheria hiyo haiwezi kurekebishwa bila marekebisho hayo kuungwa mkono na theluthi mbili ya Wabunge wote wa Tanganyika na wale wa Zanzibar. Vile vile, Katiba ya sasa ya Muungano inataja kwamba moja ya Sheria ambazo mabadiliko yake yahitaji kuungwa mkono na theluthi mbili ya Wabunge wote ni “Sura ya 557 (Toleo la 1965), Sheria ya Kuthibitisha Mapatano ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ya mwaka 1964.”

Zaidi ya hayo, kwa mujibu wa Katiba hiyo, Orodha ya Mambo ya Muungano haiwezi kufanyiwa ‘mabadiliko yoyote’ bila kuungwa mkono na theluthi mbili ya wabunge wote kutoka Tanganyika na theluthi mbili ya wabunge wote kutoka Zanzibar. Utafiti wetu umethibitisha kwamba hakuna nyongeza ya Mambo ya Muungano hata moja iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa kutumia utaratibu wa kupigiwa kura ya kuungwa mkono na theluthi mbili ya wabunge wote wa Tanganyika na idadi hiyo hiyo ya wabunge wa kutoka Zanzibar.

Kifungu cha 5 cha Sheria ya Muungano, ambacho ndicho chenye misingi mikuu ya Muungano hakijawahi kurekebishwa tangu Sheria yenyewe ilipotungwa mwaka 1964. Badala yake, Bunge limekuwa na tabia ya kukwepa kuigusa kabisa Sheria ya Muungano na badala yake limekuwa likifanya marekebisho ya orodha ya Mambo ya Muungano iliyowekwa kwa mara ya kwanza katika Katiba za Muda za mwaka 1964 na 1965 kwa kuongeza vipengele katika orodha hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Lengo la marekebisho haya limekuwa mara zote ni kuinyang’anya Zanzibar mamlaka yake chini ya Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Kuthibitisha Mapatano ya Muungano. Ndio maana katika Mapendekezo ya Halmashauri Kuu ya CCM Kuhusu Marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano na Katiba ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yaliyotolewa tarehe 27 Januari, 1983, CCM ilitamka kwamba “... msingi wa kuwa na orodha ya mambo ya muungano katika Katiba ni kuonyesha mamlaka ya Serikali ya Zanzibar ambayo yalikabidhiwa kwa Serikali ya Muungano; na msingi wa kuongeza mambo zaidi katika orodha ya mambo ya muungano, kama ambavyo imefanyika mara kwa mara, ni kuhamisha mamlaka zaidi ya Serikali ya Zanzibar kwenda kwa Serikali ya Muungano.”

Profesa Shivji anasema - katika The Legal Foundations of the Union - kwamba Bunge la Jamhuri ya Muungano halikupewa mamlaka ya kuongeza Mambo ya Muungano bali lilipewa mamlaka ya kutunga sheria zinazohusu Mambo ya Muungano kama yalivyofafanuliwa katika Sheria ya Muungano. Kwa maana hiyo, nyongeza zote zilizofanyika katika orodha ya Mambo ya Muungano tangu mwaka 1964 zilikiuka Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano na ni batili. Ndio maana, kwa muda mrefu, Wazanzibari wamelalamikia masuala haya, hasa hasa masuala ya fedha, sarafu na mafuta na gesi asilia.

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Vitendo hivi vya kukiuka Makubaliano ya Muungano vilipata Baraka za kikatiba mwaka 1984 wakati ibara mpya ya 64(4) ya Katiba ya sasa ya Muungano ilipotungwa: “Katiba yoyote iliyotungwa na Bunge kuhusu jambo lolote haitatumika Tanzania Zanzibar ila kwa mujibu wa masharti yafuatayo:

(a) Sheria hiyo iwe imetamka wazi kwamba itatumika Tanzania Bara na vile vile Tanzania Zanzibar au iwe inafuta inabadilisha, kurekebisha au kufuta Sheria inayotumika Tanzania Zanzibar; au
(b) Sheria hiyo iwe inabadilisha au kurekebisha au kufuta sheria iliyokuwa inatumika tangu zamani Tanzania Bara ambayo ilikuwa inatumika pia Tanzania Zanzibar kwa mujibu wa Mapatano ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ya mwaka 1964, au kwa mujibu wa Sheria yoyote ambayo ilitamka wazi kwamba itatumika Tanzania Bara na vile vile Tanzania Zanzibar....”
Ibara hii ya Katiba ililipa Bunge la Jamhuri ya Muungano mamlaka ya kutunga ‘sheria yoyote’ kuhusu ‘jambo lolote’, hata kama sio la Muungano na sheria hiyo itatumika Tanzania Zanzibar! Ibara hii inakiuka moja kwa moja masharti ya aya ya iii(a) ya Makubaliano ya Muungano ambayo ilisema wazi kwamba Bunge la Zanzibar “... litakuwa na mamlaka kamili ndani ya Zanzibar kwa mambo yale ambayo hayajawekwa chini ya mamlaka ya Bunge na Serikali ya Jamhuri ya Muungano....” Aidha, ibara hiyo inakinzana na ibara ndogo ya (2) ya ibara ya 64 inayotamka kwamba “mamlaka yoyote ya kutunga sheria katika Tanzania Zanzibar juu ya mambo yote yasiyo mambo ya Muungano yatakuwa mikononi mwa Baraza la Wawakilishi.”

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Vitendo vya kupuuza Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano iliyoridhia Makubaliano vilifikia kilele chake tarehe 21 Novemba, 2000 pale Mahakama ya Rufani ya Tanzania ilipotamka – katika kesi ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar dhidi ya Machano Khamis Ali na Wenzake 17 – kwamba Zanzibar sio nchi na wala sio dola. Bali, kwa mujibu wa Mahakama ya Rufani, “hakuna ubishi wa aina yoyote kwamba Jamhuri ya Muungano ni nchi moja na dola moja.” Kama tulivyokwisha kuonyesha, suala la Mahakama ya Rufani ya Tanzania yenyewe kuwa suala la Muungano liliingizwa kwenye orodha ya Mambo ya Muungano kinyemela na kinyume na Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano. Jibu la Wazanzibari juu ya ukiukwaji wa muda mrefu wa Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano iliyoridhia Makubaliano hayo lilikuwa ni kupitisha Sheria ya Mabadiliko ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar mwaka 2010.

No comments:

Post a Comment