Mjumbe wa Bunge maalum la Katiba Mhe. Tundu Lissu alipokuwa akitoa Hotuba ya Maoni ya walio wachache kutoka katika Kamati Na. 4 kabla ya Kukatiwa matangazo na Kituo cha matangazo cha TBC
<<<<<<<<<Sehemu ya tatu>>>>>>>>
NCHI MOJA AU NCHI MBILI?
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Tarehe 13 Agosti, 2010, wakati Bunge la Jamhuri ya Muungano likiwa limevunjwa kwa ajili ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2010, Baraza la Wawakilishi la Zanzibar lilipitisha Sheria ya Mabadiliko ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar, 1984. Mabadiliko haya yaliweka msingi wa kikatiba wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar inayoshirikisha CCM na Chama cha Wananchi (CUF). Kwa sababu hiyo, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba imepigiwa upatu kama Katiba ya Muafaka na, kwa kiasi fulani, hii ni kweli.
Hata hivyo, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba imekwenda mbali zaidi. Sheria hii sio tu imehoji uhalali wa orodha ya Mambo ya Muungano ya tangu mwaka 1964 na nyongeza zake zilizofuata, bali pia imehoji pia misingi muhimu ya Sheria ya Muungano iliyoridhia Makubaliano ya Muungano. Kwa mtazamo huu, Katiba ya sasa ya Zanzibar inaelekea kuwa ni tangazo la uhuru wa Zanzibar zaidi kuliko waraka wa muafaka kati ya vyama viwili vilivyokuwa mahasimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Aya ya (i) ya Makubaliano ya Muungano na kifungu cha 4 cha Sheria ya Muungano vilitangaza muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na kuundwa kwa “Jamhuri moja huru itakayoitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.” Makubaliano ya Muungano hayakuua nchi washirika wa Muungano huu. Hii inathibitishwa sio tu na masharti ya Makubaliano ya Muungano yanayoashiria kuendelea kutumika kwa sheria za Tanganyika na Zanzibar ‘katika maeneo yao’ tu, bali vifungu vya Katiba zilizofuatia Makubaliano ya Muungano.
Hivyo basi, hata baada ya mabadiliko ya jina kwenda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Katiba na sheria mbali mbali ziliendelea kutumia jina la Tanganyika na Zanzibar. Kwa mfano, Sheria ya Kuongeza Muda wa Kuitisha Bunge la Katiba, 1965, iliyosainiwa na Rais Nyerere tarehe 24 Machi, 1965, inataja, katika vifungu vyote vitatu, ‘Sheria za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.’
Aidha, Sheria ya Kutangaza Katiba ya Muda ya Tanzania ya tarehe 11 Julai, 1965, ilitangaza kwamba ‘Tanzania ni Jamhuri Huru ya Muungano’; kwamba eneo lake ni “... eneo lote la Tanganyika na Zanzibar ...” na kwamba chama kimoja cha siasa “... kwa Tanganyika kitakuwa Tanganyika African National Union (TANU)....” Kwa wakati wote wa uhai wake, Katiba ya Muda haikuwahi kutamka kuwa Tanzania ni nchi moja. Kwa upande wake, licha ya kuanza kutumia jina la Tanzania Bara na Tanzania Visiwani kwa mara ya kwanza, Toleo la Kwanza la Katiba ya sasa ya Muungano lilitamka kwamba Tanzania ni ‘Jamhuri ya Muungano.’ Hapa pia hapakuwa na tamko la ‘nchi moja.’
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Maneno ya ibara ya 1 ya Katiba ya sasa ya Muungano kwamba “Tanzania ni nchi moja na ni Jamhuri ya Muungano” yaliingia katika kamusi ya kikatiba na kisiasa ya nchi hii kufuatia ‘kuchafuka kwa hali ya kisiasa ya Zanzibar’ na kung’olewa madarakani kwa Rais Aboud Jumbe. Kufuatia hali hiyo, Katiba ya Jamhuri ya Muungano ilifanyiwa marekebisho makubwa ambayo, pamoja na mengine, yalitangaza kuwa “Tanzania ni nchi moja na ni Jamhuri ya Muungano.” Kwa sababu ya upinzani mkubwa wa Wazanzibari, Marekebisho hayo ya Katiba yaliondoa pia maneno ‘Tanzania Visiwani’ na kuweka ‘Tanzania Zanzibar’ badala yake. Maneno ‘Tanzania Bara’ yalibaki kama yalivyowekwa mwaka 1977.
Kwa maana hiyo, dhana ya Tanzania kama nchi moja haijatokana na Makubaliano ya Muungano bali ilitokana na siasa za Muungano, yaani mvutano kati ya viongozi wa Tanganyika wakiwa wamevalia joho la Jamhuri ya Muungano na viongozi wa Zanzibar waliotaka uhuru zaidi kwa nchi yao. Pili, dhana hiyo haina umri mkubwa sana kuliko inavyodhaniwa, kwani iliingia kwenye Katiba mwaka 1984, miaka thelathini iliyopita, na miaka ishirini baada ya Muungano.
Tatu, Makubaliano ya Muungano hayakuua Tanganyika, licha ya mabadiliko mengi ya kikatiba na ya kisheria ya tangu siku za mwanzo kabisa za Muungano. Bali kilichoiondoa Tanganyika katika lugha ya kikatiba na kisheria ni Katiba ya sasa ya Muungano pale ilipoacha kutumia neno Tanganyika na badala yake ikaingiza neno ‘Tanzania Bara’ mwaka 1977.
Sasa mabadiliko haya ya Katiba ya Muungano yamehojiwa na maneno ya ibara ya 2 ya Katiba mpya ya Zanzibar yanayotamka kwamba “Zanzibar ni miongoni mwa nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.” Kwa maneno haya, Zanzibar imeturudisha rasmi kwenye Makubaliano ya Muungano kwamba Jamhuri ya Muungano haikuzaliwa kutokana na kifo cha nchi mbili zilizoungana, bali nchi hizo zimeendelea kuwepo. Kwa maana hiyo, Katiba ya Zanzibar ni tangazo la uhuru wa Tanganyika vile vile, kwani kwa miaka hamsini Tanganyika imejificha nyuma ya pazia la Tanzania.
Ibara ya 2(2) ya Katiba ya Muungano inampa Rais wa Jamhuri ya Muungano – kwa kushauriana kwanza na Rais wa Zanzibar - mamlaka ya kuigawa Tanzania Zanzibar katika mikoa, wilaya au maeneo mengineyo. Vile vile, ibara ya 61(3) ya Katiba ya Muungano inampa Rais wa Zanzibar mamlaka ya kuteua Wakuu wa Mikoa katika Tanzania Zanzibar ‘baada ya kushauriana na Rais.’ Masuala ya mgawanyo wa nchi katika mikoa na mamlaka za mikoa hiyo sio, na hayajawahi kuwa, Mambo ya Muungano kwa mujibu wa Sheria ya Muungano. Vile vile hayapo katika orodha ya Mambo ya Muungano.
Ni wazi kwa hiyo, kwamba ibara za 2(2) na 61(3) za Katiba ya Muungano zilikuwa zinakiuka matakwa ya Sheria ya Muungano na kwa hiyo ni batili. Sasa wazanzibari ‘wamejitangazia uhuru’ kwa kutangaza – katika ibara ya 2A ya Katiba mpya ya Zanzibar – kwamba “... Rais (wa Zanzibar) aweza kuigawa Zanzibar katika mikoa, wilaya na maeneo mengineyo kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi.” Aidha, kwa ibara ya 61(1), Rais wa Zanzibar hawajibiki tena kushauriana na Rais wa Muungano pale anapofanya uteuzi wa wakuu wa mikoa ya Zanzibar.
Wakati ambapo Sheria ya Muungano ilikuwa imetambua na kuhifadhi mamlaka ya Rais wa Zanzibar kama mkuu wa dola ya Zanzibar, Mahakama ya Rufani ya Tanzania – katika Kesi ya Machano Khamis Ali na Wenzake – ilitishia moja kwa moja msingi huo kwa kutamka kwamba Zanzibar sio nchi na wala sio dola na kwa hiyo haiwezi kutishiwa na kosa la uhaini. Sasa ibara ya 26(1) ya Katiba mpya Zanzibar ‘imerudisha’ dola ya Zanzibar kwa kutamka kwamba “kutakuwa na Rais wa Zanzibar ambaye atakuwa Mkuu wa Nchi ya Zanzibar, Kiongozi Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.”
Aidha, kwa kutambua kwamba ‘Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano’ sio moja ya Mambo ya Muungano kwa mujibu wa Sheria ya Muungano, Katiba ya sasa ya Zanzibar imetamka kwamba katika kesi zinazohusu ‘kinga za haki za lazima, wajibu na uhuru wa mtu binafsi’, uamuzi wa majaji watatu wa Mahakama Kuu ya Zanzibar “... utakuwa ni wa mwisho na hautokatiwa rufaa kwenye Mahakama ya Rufaa ya Tanzania.”
Kifungu cha 5(1)(a)(iii) na (iv) cha Sheria ya Muungano kinataja ‘ulinzi’ na ‘polisi’ kama sehemu ya mambo kumi na moja ya Muungano. Na hivyo ndivyo inavyosema aya ya (iv)(c) na (d) ya Makubaliano ya Muungano. Ijapokuwa ‘ulinzi’ ulichakachuliwa baadae kwa kuongezwa maneno ‘na usalama’, bado ni sahihi kusema kwamba masuala ya ulinzi na polisi ni masuala halali ambayo Sheria ya Muungano iliyakasimu kwa Serikali ya Muungano. Na kwa sababu hiyo, ni sahihi kwa Katiba ya Muungano kutamka – kama inavyofanya katika ibara ya 33(2) - kwamba “Rais (wa Jamhuri ya Muungano) atakuwa Mkuu wa Nchi, Kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu.”
Hata hivyo, katika kile kinachoonekana kama hojaji kubwa ya msingi huu wa Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano, ibara ya 121 ya Katiba ya sasa ya Zanzibar imeunda majeshi ya Zanzibar inayoyaita ‘Idara Maalum.’ Majeshi haya, kwa mujibu wa ibara ya 121(2) ni Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU); Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM); Chuo cha Mafunzo (cha wahalifu), na Idara Maalum nyingine yoyote ambayo Rais wa Zanzibar anaweza kuianzisha ‘ikiwa ataona inafaa....’
Kuthibitisha kwamba Idara Maalum ni majeshi, ibara ya 121(4) inakataza watumishi wa Idara Maalum ‘... kujishughulisha na mambo ya siasa....’ Makatazo haya hayatofautiani na makatazo ya wanajeshi kujiunga na vyama vya siasa yaliyoko katika ibara ya 147(3) ya Katiba ya Muungano.
Sio tu kwamba Katiba mpya ya Zanzibar inaanzisha majeshi bali pia inamfanya Rais wa Zanzibar kuwa Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi hayo. Kwa mujibu wa ibara ya 123(1) ya Katiba hiyo, “Rais atakuwa Kamanda Mkuu wa Idara Maalum na atakuwa na uwezo wa kufanya chochote kile anachohisi, kwa maslahi ya Taifa (la Zanzibar), kinafaa.” Kwa maoni yetu, hakuna tofauti yoyote ya msingi kati ya maneno ‘Amiri Jeshi Mkuu’ na ‘Kamanda Mkuu’ bali, kwa kiasi kikubwa, ni mpangilio wa maneno hayo tu.
Aidha, kwa mujibu wa ibara ya 123(2), mamlaka ya Rais wa Zanzibar chini ya ibara ndogo ya (1) yanaingiza “... uwezo wa kutoa amri ya kufanya shughuli yoyote inayohusiana na Idara hiyo kwa manufaa ya Taifa.” Kwa maoni yetu, haya ni mamlaka ya kutangaza au kuendesha vita ambayo, kwa mujibu wa ibara ya 44(1) ya Katiba ya Muungano, ni mamlaka pekee ya Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Kifungu cha 5(1)(b) cha Sheria ya Muungano kilitamka kwamba muundo wa Serikali ya Zanzibar utakuwa kama utakavyoamuliwa na sheria za Zanzibar pekee. Na hivyo ndivyo ilivyokubaliwa katika aya ya (iii)(a) ya Makubaliano ya Muungano. Hata hivyo, licha ya muundo wa Serikali ya Zanzibar kutokuwepo katika orodha ya Mambo ya Muungano, Katiba ya Muungano imetenga Sura ya Nne nzima kuzungumzia ‘Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Baraza la Mapinduzi la Zanzibar na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.’
Kwa mujibu wa Profesa Shivji katika The Legal Foundations of the Union, Sura ya Nne ya Katiba ya Muungano “... haina ulazima wowote na ni kuingilia, bila kualikwa, kwenye mambo ambayo yako ndani ya mamlaka pekee ya Zanzibar.” Ndio maana Katiba mpya ya Zanzibar – kwa usahihi kabisa - imefanya mabadiliko katika muundo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar bila ya kuzingatia matakwa ya Sura ya Nne ya Katiba ya Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Katiba mpya ya Zanzibar sio tu kwamba ‘imetangaza uhuru’ wa Zanzibar kwa kuhoji misingi muhimu ya Makubaliano ya Muungano, Sheria ya Muungano na Katiba ya Muungano, bali pia imehakikisha kwamba uhuru huo utalindwa dhidi ya tishio lolote la Serikali ya Muungano. Hii imefanywa kwa kuweka utaratibu wa kuwepo kura ya maoni ya wananchi wa Zanzibar kuhusu mabadiliko ya vifungu kadhaa vya Katiba ya Zanzibar. Kwa mujibu wa ibara ya 80A(1) ya Katiba hiyo, “... Baraza la Wawakilishi halitaweza kufanya mabadiliko ya Katiba kuhusiana na sharti lolote lililomo katika kifungu chochote kilichoainishwa katika kijifungu cha (2) cha kifungu hiki, mpaka kwanza mabadiliko hayo yakubaliwe na wananchi kwa kura ya maoni.”
Vifungu vinavyohitaji kura ya maoni ni vifungu vyote vya Sehemu ya Kwanza ya Sura ya Kwanza inayohusu Zanzibar kama nchi na/au dola; kifungu cha 9 kinachohusu Serikali na watu wa Zanzibar; vifungu vyote vya Sura ya Tatu inayohusu kinga ya haki za lazima, wajibu na uhuru wa mtu binafsi; na kifungu cha 26 kinachohusu Rais wa Zanzibar na mamlaka yake. Vifungu vingine ni pamoja na kifungu cha 28 kinachohusu muda wa urais; Sehemu ya Pili na ya Tatu ya Sura ya Nne zinazohusu Makamu wawili wa Rais, Baraza la Mawaziri na Baraza la Mapinduzi; kifungu cha 80A kinachohifadhi haki ya kura ya maoni; na vifungu vya 121 na 123 vinavyohusu Idara Maalum na mambo yanayohusiana nayo.
Kuweka masharti ya kura ya maoni kuhusu mabadiliko ya vifungu tajwa vya Katiba mpya ya Zanzibar kuna athari ya moja kwa moja kwa uhai wa Muungano wetu. Hii ni kwa sababu hata vifungu ambavyo tumeonyesha kwamba vinakiuka misingi mikuu ya Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano haviwezi kubadilishwa bila kura ya maoni ya Wazanzibari. Kwa maneno mengine, kwa mujibu wa Katiba ya sasa ya Zanzibar, masuala ya kama Tanzania ni nchi moja au la, majeshi ya ulinzi, polisi, n.k. ambayo yamekuwa Mambo ya Muungano kwa mujibu wa Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano sio Mambo ya Muungano tena hadi hapo wananchi wa Zanzibar watakapoamua – kwa kura ya maoni – kuyarudisha kwa mamlaka ya Muungano. Huku ni kutangaza uhuru wa Zanzibar bila kutaja neno uhuru!
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Kwa mtazamo wa Katiba ya sasa ya Zanzibar, hakuna tena ‘nchi moja’ inayozungumzwa katika Katiba ya sasa ya Muungano bali tuna ‘nchi mbili’ zinazozungumzwa katika Makubaliano ya Muungano. Kwa mtazamo huo huo, masuala ya ulinzi na usalama, polisi, n.k. sio tena Mambo ya Muungano kwa sababu sasa kila nchi ina majeshi yake na kila moja ina Amiri Jeshi Mkuu wake. Aidha, tuna marais wawili, wakuu wa nchi wawili na viongozi wa serikali wawili.
Mabadiliko haya ya kikatiba yanadhihirishwa wazi na taratibu za kiitifaki wakati wa Sherehe za Mapinduzi Zanzibar ambako siku hizi Rais wa Zanzibar ndiye anayekagua gwaride rasmi la vikosi vya ulinzi na usalama, kupigiwa mizinga ishirini na moja na anakuwa wa mwisho kuingia, na wa mwisho kutoka, uwanjani huku Rais wa Jamhuri ya Muungano akiwa wa pili kiitifaki.
Kwa upande mwingine, kwa mtazamo wa Katiba ya sasa ya Zanzibar, Rais wa Muungano hana tena mamlaka ya kugawa mikoa na wilaya kwa upande wa Zanzibar, na wala hawezi kumshauri tena Rais wa Zanzibar anapoteua Wakuu wa Mikoa wa Tanzania Zanzibar. Aidha, Mahakama ya Rufani ya Tanzania – licha ya kuwa moja ya Mambo ya Muungano kwa mujibu wa Katiba ya Muungano - haina tena mamlaka ya kusikiliza na kuamua rufaa zinazohusu haki za msingi na uhuru wa mtu binafsi zinazotoka Zanzibar. Yote haya hayapo na hayajawahi kuwapo katika Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano.
MUUNGANO USIO WA USAWA
Tangu mwanzo Muungano wa Tanganyika na Zanzibar haukuwa Muungano wa usawa. Huu ni Muungano ulioipa Tanganyika – ikiwa imevalia koti la Jamhuri ya Muungano - mamlaka ya kuingilia uhuru na mamlaka ya Zanzibar. Hii inathibitishwa na Hati ya Makubaliano ya Muungano yenyewe. Kwanza, kwa kutamka kwamba katika kipindi cha mpito “Katiba ya Jamhuri ya Muungano itakuwa ni Katiba ya Tanganyika...”, ni wazi kwamba Mshirika wa Muungano aliyekuwa na nguvu katika Muungano huu ni Tanganyika.
Pili, kwa kuweka orodha ya mambo 11 ya Muungano, ni wazi kwamba Zanzibar ilinyang’anywa mamlaka juu ya masuala hayo na mamlaka hayo yalihamishiwa kwa Tanganyika ikiwa imevaa koti la Jamhuri ya Muungano. Kwa maana hiyo, Zanzibar ilinyang’anywa mamlaka yake juu ya masuala ya nchi za nje, ulinzi, polisi, mamlaka ya hali ya hatari, uraia, uhamiaji, biashara ya nje na mikopo na masuala mbali mbali ya kodi. Hati ya Makubaliano ya Muungano yenyewe inasema wazi kwamba “Bunge na Serikali (ya Jamhuri ya Muungano) litakuwa na mamlaka kamili kwenye mambo hayo kwa Jamhuri ya Muungano na, kwa nyongeza, mamlaka kamili kwa ajili ya mambo mengine yote ya na kwa ajili ya Tanganyika.”
Tatu, kwa kutangaza kwamba rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano atakuwa Mwalimu Nyerere na Makamu wa kwanza wa Rais atakuwa Sheikh Abeid Karume; na kwa kutangaza kwamba Makamu wa Kwanza wa Rais atakuwa ndiye msaidizi mkuu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano katika utekelezaji wa majukumu yake ya kiutendaji kuhusu Zanzibar, ni wazi kwamba Hati ya Makubaliano ya Muungano nafasi ya chini (subordinate position) ya Zanzibar katika Muungano.
Nne, kwa kuzifanya alama za utaifa (national emblems) za Tanganyika kuwa ndio alama za taifa za Jamhuri ya Muungano, kuna-emphasize superior position ya Tanganyika ndani ya Muungano na subaltern position ya Zanzibar katika Muungano huu. Ukweli huo huo unahusu masuala ya kuzifanya taasisi na watumishi wa Serikali ya Tanganyika kuwa ndio taasisi na watumishi wa Jamhuri ya Muungano. Kama Maalim Seif Shariff Hamad anavyomalizia Maoni yake kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba tarehe 13 Januari, 2013: “Mfumo (wa Muungano) uliopo sasa hauinufaishi Zanzibar na hivyo haukubaliki kwa Wazanzibari. Koti la Muungano kama lilivyo sasa linabana sana. Wakati umefika tushone koti jipya kwa mujibu wa mahitaji ya zama hizi.”
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Baada ya nusu karne ya ukiukaji wa Hati ya Makubaliano ya Muungano, na kwa hali ya sasa ya kisiasa na kikatiba ya Zanzibar, ni wazi Hati ya Makubaliano ya Muungano haiwezi kuwa msingi wa Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar tunayoipendekeza. Aidha, Katiba Mpya haiwezi kuwa ni mwendelezo wa Hati ya Makubaliano ya Muungano ambayo, kama ambavyo tumeonyesha, haijawahi kuheshimiwa katika miaka hamsini tangu kusainiwa kwake.
Kwa maoni ya wajumbe walio wachache wa Kamati Namba Nne, wakati umefika wa kujenga mahusiano kati ya nchi hizi mbili katika msingi ulio imara zaidi na wa usawa zaidi. Ndio maana tunapendekeza kwamba Katiba Mpya ndiyo iwe msingi wa Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar.
Ibara ya 2
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Ibara ya 2 ya Rasimu inafafanua eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. “Eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni eneo lote la Tanganyika likijumuisha sehemu yake ya bahari na eneo lote la Zanzibar likijumuisha sehemu yake ya bahari.” Wajumbe walio wachache wa Kamati Namba Nne wanapendekeza ibara hiyo ifutwe yote na kuandikwa upya kama ifuatavyo: “Eneo la Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar ni eneo lote la Tanganyika likijumuisha sehemu yake ya bahari, maziwa na mito, pamoja na eneo lake la anga; na eneo lote la Zanzibar ikiwa ni pamoja na visiwa vidogo vinvyozunguka Visiwa vya Unguja na Pemba na eneo lake la bahari pamoja na eneo lake la anga.”
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Mapendekezo haya ya wajumbe walio wachache katika Kamati Namba Nne yanashawishi kutambuliwa na kufafanuliwa kwa mipaka ya nchi hizi mbili Washirika wa Muungano. Hii itasaidia kuepusha migogoro inayoweza kujitokeza hasa hasa kuhusu rasilmali zinazopatikana baharini kama vile mafuta, gesi asilia na rasilmali uvuvi. Aidha, kwa sababu ya kuwepo kwa migogoro ya mipaka katika maeneo ya maji kama ule kati ya Jamhuri ya Muungano na Malawi, wajumbe walio wachache wa Kamati Namba Nne wanafikiri kwamba ni muhimu kwa Sheria kuu ya nchi kutamka na kufafanua mipaka yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977, imefafanua eneo la Jamhuri ya Muungano kama ifuatavyo: “Eneo la Jamhuri ya Muungano ni eneo lote la Tanzania Bara na eneo lote la Tanzania Zanzibar, na ni pamoja na sehemu yake ya bahari ambayo Tanzania inapakana nayo.” Aidha, ibara ya 1 ya Katiba ya Zanzibar, 1984, inafafanua ‘Zanzibar na mipaka yake’ kama ifuatavyo: “Zanzibar ni nchi ambayo eneo la mipaka yake ni eneo lote la Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na Visiwa vidogo vilivyoizunguka na bahari yake ambayo kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ikiitwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.”
Wajumbe walio wachache wa Kamati Namba Nne wanatambua ukweli kwamba ufafanuzi wa mipaka ya Jamhuri ya Muungano uliopo katika Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano ni mfinyu sana na hautoshelezi mahitaji ya sasa ya kiuchumi na kisiasa. Kwanza, licha ya Jamhuri ya Muungano kupakana na maziwa kama vile Victoria, Tanganyika na Nyasa ambayo tunayachangia na nchi jirani za Kenya, Uganda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Zambia, Malawi na Msumbiji; na Mto Ruvuma tunaouchangia na Msumbiji, maelezo haya ya Katiba ya sasa hayatambui uwepo wa maeneo hayo.
Pili, Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano haitofautishi kati ya eneo la bahari la Tanganyika na eneo la bahari la Zanzibar. Hii ni hatari kwani inaweza kuwa chanzo cha migogoro ya mipaka kati ya nchi hizi mbili hasa kwa vile masuala ya rasilmali asilia zilizoko baharini zimeondolewa kinyemela katika orodha ya mambo ya Muungano ama yanapendekezwa na Rasimu kuondolewa katika orodha hiyo.
Tatu, Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano na hata ya Zanzibar hazitambui milki ya Jamhuri ya Muungano au ya Zanzibar juu ya anga la Jamhuri ya Muungano au la Zanzibar. Anga ni rasilmali muhimu hasa katika masuala ya usafiri wa anga, na mawasiliano ya simu na redio. Mapendekezo haya ya wajumbe walio wachache kuhusu eneo la nchi yetu yatatua matatizo yaliyotajwa hapa.
IBARA YA 3
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Ibara ya 3 ya Rasimu inahusu ‘Alama na Sikukuu za Taifa.’ Ibara ya 3(1) inapendekeza Alama za Taifa kuwa ni Bendera ya Taifa, Wimbo wa Taifa na Nembo ya Taifa kama zitakavyoainishwa katika sheria husika za nchi. Kwa upande wake, ibara ya 3(2) inapendekeza Sikukuu za Kitaifa kuwa ni “Siku ya Uhuru wa Tanganyika itakayoadhimishwa tarehe 9 Disemba; Siku ya Mapinduzi ya Zanzibar itakayoadhimishwa tarehe 12 Januari; Siku ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar itakayoadhimishwa tarehe 26 Aprili; na Sikukuu nyingine zitakazoainishwa na sheria za nchi.” Kwa mujibu wa ibara 3(3), kila Sikukuu ya Kitaifa itakuwa ni siku ya mapumziko.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Alama za Taifa ni suala muhimu sana kwa utambulisho wa historia na utamaduni wa nchi yoyote. Kwa sababu mbali mbali za kihistoria tulizozielezea kwa kirefu katika maoni yetu kuhusu ibara 1 ya Rasimu, suala la alama za taifa za Jamhuri ya Muungano limejaa utata mtupu. Kwa upande mmoja, alama za taifa ambazo zimeendelea kutumika katika kipindi chote cha miaka hamsini ya Muungano ni Alama za Taifa la Tanganyika ambazo zilifanywa kuwa za Jamhuri ya Muungano pale Tanganyika ilipovikwa joho la Jamhuri ya Muungano kati ya tarehe 26 Aprili na 15 Juni, 1964.
Mfano mzuri ni wa Nembo ya Taifa, maarufu kama ‘Bibi na Bwana.’ Alama hiyo ya Taifa iliwekwa na Sheria ya Nembo ya Taifa, Sura ya 504 ya Sheria za Tanganyika, yaani The Public Seal Act, Chapter 504 of the Laws, ya mwaka 1962 na ilianza kutumika Siku ya Jamhuri, yaani tarehe 9 Disemba 1962. Hata hivyo, kufuatia kuzaliwa kwa Muungano, Alama hiyo ya Taifa la Tanganyika iligeuzwa na kuwa Nembo ya Taifa ya Jamhuri ya Muungano kwa kutumia Amri ya Masharti ya Mpito ya Mwalimu Nyerere ya tarehe 26 Aprili, 1964.
Kwa upande mwingine, matumizi ya Alama nyingine za Taifa ni kielelezo kingine cha utamaduni wa ukiukaji sheria ambao umejengeka katika nusu karne ya Muungano. Suala hili linahusu Bendera ya Taifa na Wimbo wa Taifa. Kwanza, wakati Bendera ya sasa ya Taifa ilianza kutumika kufuatia kushushwa kwa Bendera za Taifa za Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar katika Umoja wa Mataifa, baada ya maelekezo ya Mwanasheria Mkuu wa Umoja wa Mataifa Stavropoulos ya tarehe 13 Mei, 1964, Bunge la Jamhuri ya Muungano halikutunga sheria yoyote ya kuwezesha uwepo wa Alama hii muhimu ya Taifa hadi tarehe 7 Mei, 1971, zaidi ya miaka saba baada ya kuzaliwa Muungano!
Pili, baada ya kutungwa kwake na ikiwa na lengo la kuficha ukweli kwamba Bendera ya Taifa ilikuwa imetumika kwa zaidi ya miaka saba bila uhalali wowote wa kisheria, Sheria ya Bendera ya Taifa na Nembo ya Taifa, yaani The National Flag and Coat of Arms Act, ilitamka kwamba Bendera ya Taifa imeanza kutumika tangu tarehe 26 Aprili 1964, yapata miaka saba kabla sheria yenyewe haijatungwa!
Tatu, licha ya ukweli kwamba ‘Bibi na Bwana’ ilianza kutumika tangu tarehe 9 Disemba, 1962, na licha ya Mwalimu Nyerere kuigeuza Nembo hiyo ya Tanganyika kuwa ya Jamhuri ya Muungano kwa Amri yake ya tarehe 26 Aprili, 1964, kifungu cha 4 cha Sheria ya Bendera ya Taifa na Nembo ya Taifa kilishurutisha kwamba ‘Bibi na Bwana’ nayo itakuwa Nembo ya Taifa ya Jamhuri ya Muungano kuanzia tarehe 26 Aprili, 1964.
Nne, Wimbo wa Taifa unaotumiwa sasa, yaani ‘Mungu Ibariki Afrika’, ni Wimbo wa Taifa wa Tanganyika ambao ulifanywa kuwa Wimbo wa Taifa wa Jamhuri ya Muungano bila ya msingi wowote wa kisheria. Hii ni kwa sababu, Sheria ya Alama za Taifa haitambui Wimbo wa Taifa kama mojawapo ya Alama za Taifa. Aidha, Amri ya Masharti ya Mpito ya Mwalimu Nyerere iliyohalalisha Nembo ya Taifa ya Tanganyika kutumika kama Nembo ya Taifa ya Jamhuri ya Muungano haikuhusu Wimbo wa Taifa.
Kwa nchi na serikali ambayo imejidai kwa ‘upekee’ wake katika mambo mengi, kushindwa kutambua hata Wimbo wake Taifa ni kitendo cha fedheha kubwa sana kwa nchi yetu na wale ambao wameitawala tangu uhuru. Nchi nyingine za ki-Afrika zimetupita mbali katika kuenzi Alama zao za Taifa kwa kuzitambua kikatiba. Hivyo, kwa mfano, ibara ya 9(1) na (2) na Nyongeza ya Pili ya Katiba ya Kenya, 2010, imefafanua Alama za Taifa za Kenya pamoja na kuweka maneno ya Wimbo wa Taifa wa nchi hiyo. Vivyo hivyo, ibara ya 4 na Nyongeza ya Nne ya Katiba ya Zimbabwe, 2013, nayo imeweka Alama za Taifa za Zimbabwe pamoja na maneno na muziki wa Wimbo wa Taifa wa nchi hiyo. Sisi, tunaojidai kuwa mfano wa kuigwa na nchi nyingine duniani, hatujaitaja Bendera yetu ya Taifa mahali popote katika Katiba na Sheria zetu!
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Zaidi ya kupendekeza nyongeza ndogo kwenye ibara ya 3(2), wajumbe walio wengi wa Kamati Namba Nne hawakuona tatizo lolote la mapendekezo ya ibara ya 3 ya Rasimu. Hata hivyo, mkanganyiko ambao tumeuonyesha kuhusu jambo hili muhimu unaonyesha haja kubwa ya kuwa na mwanzo mpya kikatiba katika masuala ya Alama za Taifa. Kwa sababu hiyo, wajumbe walio wachache wanapendekeza kwamba ibara ya 3(1) ya Rasimu ifanyiwe marekebisho ili iweze kusomeka ifuatavyo:
“3(1) Alama za Taifa zitakuwa ni:
(a) Bendera ya Taifa ya Shirikisho na Bendera za Taifa za Nchi Washirika wa Shirikisho;
(b) Wimbo wa Taifa wa Shirikisho na Nyimbo za Taifa za Nchi Washirika wa Shirikisho;
(c) Nembo ya Taifa ya Shirikisho na Nembo za Taifa za Nchi Washirika wa Shirikisho,
kama zitakavyoainishwa katika sheria husika za nchi.”
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Wajumbe walio wachache wa Kamati Namba Nne wanapendekeza pia marekebisho katika ibara ya 3(2) ya Rasimu. Kama ilivyo hivi sasa, ibara hiyo inaendeleza upotoshaji wa historia ya Jamhuri ya Muungano na ya nchi washirika wa Muungano. Kwanza, kupendekeza kuendelea kuadhimisha Siku ya Uhuru wa Tanganyika wakati Tanganyika yenyewe haitambuliwi kikatiba ni kuendeleza unafiki wa kikatiba na wa kisiasa ambao umeendelea kwa nusu karne. Kama taifa, hatuwezi kuendelea kuishi katika uongo kwa namna hii.
Pili, Zanzibar haikupata uhuru wake Siku ya Mapinduzi ya tarehe 12 Januari, 1964. Zanzibar ilipata uhuru wake siku ya tarehe 10 Disemba, 1963, ikiwa na Serikali halali iliyochaguliwa na wananchi kwenye uchaguzi huru na wa haki kwa mujibu wa sheria zilizokuwepo wakati huo. Uhuru huo ulitambuliwa na jumuiya ya kimataifa pale Zanzibar ilipokubaliwa kujiunga kama mwanachama wa 99 wa Umoja wa Mataifa tarehe 16 Disemba, 1963. Hata Sheikh Abedi Karume, aliyekuja kushikilia uongozi wa Zanzibar ya baada ya Mapinduzi na mwasisi wa Muungano, alitambua uhuru huo wa Zanzibar. Katika hotuba yake ya kuukaribisha Uhuru wa Dola ya Zanzibar wa tarehe 10 Disemba, 1963, Sheikh Karume alitamka maneno yafuatayo:
“Leo tarehe 10 Disemba, 1963, ZANZIBAR imekuwa Huru. Hii leo sisi watu wa visiwa hivi tumepata haki ya kuchukuwa mahala petu kuwa ni Dola sawa na nyengine katika umoja wa Nchi za Dola za Commonwealth. Kwa uchache, kuwa mwanachama katika umoja huo, kuna maana kwamba nchi hii ni huru chini ya mpango wa Sirikali ambayo msingi wake umejengwa juu ya kuendelea kwa ridhaa ya wananchi.
“Ili kufikilia matarajio yetu hayo tunayo moja katika Katiba zenye msingi madhubuti iliyohusika na shuruti za haki za binadamu, haki za mambo ya siasa na uhuru wa dola yoyote nyengine. Ni wajibu wa watu wote wa dola yetu mpya, kila mmoja katika sisi bila ya kujali fikra zetu za siasa au madaraka yetu kusaidia kweli kweli Katiba yetu iweze kufanya kazi. Pamoja na manufaa, haki na uhuru ambayo yote hayo yamepatikana baada ya nchi kuwa huru.”
Mwezi mmoja baada ya kutamka maneno hayo, ‘Sirikali ambayo msingi wake umejengwa juu ya ... ridhaa ya wananchi’ ilipinduliwa kwa nguvu za kijeshi, na Sheikh Karume akafanywa kuwa Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar iliyotokana na Mapinduzi hayo!
Ukweli huu wa kihistoria, hata kama utakuwa ni mchungu kwa baadhi ya watu, unahitaji kutambuliwa ili kuiwezesha nchi yetu kuwa na mapatano na mwafaka wa kitaifa. Na mahali pa kuanzia mchakato wa mapatano ya kitaifa ni kufichua historia hii iliyofichwa kwa nusu karne kwa kuifanya Siku ya Uhuru wa Zanzibar kuwa Sikukuu ya Kitaifa sawa na Siku ya Uhuru wa Tanganyika na Siku ya Mapinduzi. Kwa sababu hiyo, wajumbe walio wachache wa Kamati Namba Nne wanapendekeza marekebisho yafuatayo katika ibara ya 3(2) ya Rasimu:
(a) Kwa kufuta aya yote ya (c) na kuibadilisha na aya mpya ya (c) itakayosomeka ‘Siku ya Uhuru wa Zanzibar itakayoadhimishwa tarehe 10 Disemba.’
(b) Kwa kuingiza aya mpya ya (d) itakayosomeka ‘Siku ya Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar itakayoadhimishwa katika tarehe ya kupitishwa Katiba Mpya ya Shirikisho la Jamhuri za Tanganyika na Zanzibar.’
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Mapendekezo haya yanaiondoa Siku ya Muungano kama Sikukuu ya Kitaifa. Kwa sababu ambazo tumezielezea kwa kirefu kuhusiana na ibara ya 1 ya Rasimu, ni wazi kwamba Muungano wa aina hii haustahili kuendelea kupewa enzi ya kuwa na Sikukuu yake ya Kitaifa.
IBARA YA 4
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Wajumbe wa Kamati Namba Nne walikuwa na mjadala mkali sana kuhusu mapendekezo ya ibara ya 4 ya Rasimu. Ibara hiyo inahusu ‘Lugha ya Taifa na lugha za alama.’ Ibara ya 4(1) inakifanya Kiswahili kuwa Lugha ya Taifa ambayo “... itatumika katika mawasiliano rasmi ya kitaifa na kiserikali.” Ibara ya 4(2) inaruhusu matumizi ya lugha ya Kiingereza au ‘lugha nyingine yoyote’ kama “... lugha rasmi ya mawasiliano ya kiserikali pale itakapohitajika.” Mwisho, ibara ya 4(3) inaitaka Serikali kuweka “... mazingira yatakayowezesha kuwepo kwa mawasiliano mbadala zikiwemo lugha za alama, maandishi yaliyokuzwa na nukta nundu kwenye sehemu muhimu za umma na katika vyombo vya habari vinavyotangaza habari zake kitaifa kwa ajili ya watu wenye mahitaji maalum.”
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Wajumbe walio wachache wa Kamati Namba Nne wanapendekeza marekebisho yafuatayo katika ibara ya 4 ya Rasimu.
“4(1) Lugha ya Taifa ya Shirikisho itakuwa ni Kiswahili na itatumika katika shughuli zote za umma na mawasiliano yote rasmi ya kitaifa na kiserikali.
“4(2) Kiswahili kitakuwa ndio Lugha ya Mahakama za Shirikisho na pia Lugha ya Mabunge ya Shirikisho na Sheria, Muswada, Maazimio na nyaraka nyingine za kibunge zitakuwa katika Lugha ya Kiswahili.
“4(3) Bila ya kuathiri masharti ya ibara ndogo ya (1) na (2), lugha ya Kiingereza au lugha nyingine yoyote inaweza kutumika kuwa lugha rasmi ya mawasiliano ya kiserikali pale itakapohitajika.
“4(4) Mamlaka ya nchi-
(a) zitakuza na kulinda utajiri wa lugha za watu wa Shirikisho la Jamhuri; na
(b) zitakuza uendelezaji na matumizi ya lugha za makabila na jumuiya za Shirikisho la Jamhuri pamoja na kuweka mazingira yatakayowezesha kuwepo kwa mawasiliano mbadala zikiwemo lugha za alama, maandishi yaliyokuzwa na nukta nundu kwenye sehemu muhimu za umma na katika vyombo vya habari vinavyotangaza habari zake kitaifa kwa ajili ya watu wenye mahitaji maalum.”
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Sababu za mapendekezo haya ya wajumbe walio wachache zinajionyesha wazi. Tanzania ni nchi ya asili ya Kiswahili. Hata hivyo, na licha ya matamko ya wanasiasa na watawala katika kipindi chote cha uhuru wa Tanganyika na Zanzibar na tangu Muungano wa mwaka 1964, Kiswahili hakijawahi kutambuliwa rasmi kikatiba kama Lugha ya Taifa au hata lugha rasmi ya shughuli za kiserikali. Tofauti pekee ni Zanzibar ambayo Katiba yake imetambua Kiswahili kuwa lugha rasmi ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar na lugha ya sheria za Zanzibar. Hata Kenya, ambayo Kiswahili chake ni cha kuungaunga, imetambua Kiswahili kuwa Lugha ya Taifa ya Jamhuri ya Kenya na moja ya lugha mbili rasmi za nchi hiyo.
Sababu ya pili ni haja ya kuondokana na utamaduni tuliourithi kutoka kwa wakoloni ambao ulifanya Kiswahili iwe na hadhi ya chini kulinganisha na Kiingereza katika shughuli za kiserikali, kimahakama na kibunge. Hadi sasa lugha rasmi ya Muswada na Sheria zinazotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano ni Kiingereza.
Hata pale ambapo Sheria imetafsiriwa kwenda kwenye Kiswahili, kama ambavyo imetokea mara kwa mara, sheria za tafsiri za sheria zimeelekeza kwamba panapotokea mgongano wa kisheria kati ya lugha hizo mbili, basi lugha iliyotungiwa sheria hiyo, yaani Kiingereza, ndiyo inayotiliwa nguvu na tafsiri ya Kiswahili inatanguka.
Aidha, licha ya sheria za nchi kuweka bayana kwamba lugha ya Mahakama ni Kiswahili au Kiingereza, sheria hizo zimesisitiza kwamba lugha ya kumbukumbu za Mahakama itakuwa ni Kiingereza. Katiba Mpya ni fursa muhimu ya kupandisha hadhi lugha yetu ya taifa kwa kuifanya kuwa lugha ya shughuli zote za kiserikali, kimahakama na kibunge.
Tatu, Katiba Mpya inatupa fursa muhimu ya kutambua, kulinda na kukuza lugha zetu za asili na lugha za alama. Lugha ni sehemu muhimu ya utambulisho na utajiri wetu wa kiutamaduni. Hata hivyo, tangu uhuru, lugha za makabila yetu zimepigwa vita kuwa kuzitambua, kuzikuza na kuziendeleza kutajenga ukabila na utengano wa kitaifa. Aidha, dhana potofu imejengwa kwamba kukuza na kuendeleza Kiswahili ndio njia pekee ya kujenga umoja na utengamano wa kitaifa.
Mwelekeo wa sasa wa kikatiba katika nchi za Afrika ni kutambua na kuendeleza lugha za watu wa Afrika kama sehemu ya utu wetu, utambulisho wetu na utajiri wetu wa kiutamaduni. Kwa mfano, Katiba za nchi za Ghana, Kenya na Zimbabwe zimetambua lugha za asili za nchi zao kama sehemu ya utambulisho na utajiri wao wa kiutamaduni.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Ibara za 5, 6 na 9 za Rasimu zilipitishwa na Kamati Namba Nne kwa kuungwa mkono na theluthi mbili za wajumbe wote wa Kamati kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya wajumbe wote wa kutoka Zanzibar kama inavyotakiwa na kifungu cha 26(2) cha Sheria na kanuni ya 64(1) ya Kanuni. Hivyo, kwa mujibu wa kanuni ya 32(3) ya Kanuni, maoni haya hayahusu ibara hizo za Rasimu.
No comments:
Post a Comment