Advertise with Us

Advertise with Us

DHall

DHall

Pages

April 12, 2014

Hotuba ya Tundu Lissu iliyokatishwa kwa makusudi na TBC- Sehemu ya Nne!

Mjumbe wa Bunge maalum la Katiba Mhe. Tundu Lissu alipokuwa akitoa Hotuba ya Maoni ya walio wachache kutoka katika Kamati Na. 4 kabla ya Kukatiwa matangazo na Kituo cha matangazo cha TBC 

<<<<<<<<<<<<Sehemu ya nne>>>>>>>>>

IBARA YA 8

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Ibara ya 8 ya Rasimu inahusu ‘Ukuu na utii wa Katiba’ na ilizua mjadala mkali sana katika Kamati Namba Nne. Wajumbe walio wengi kwenye Kamati hawakupendekeza marekebisho yoyote katika ibara hiyo. Hata hivyo, wajumbe hao walipiga kura kupinga marekebisho yaliyopendekezwa na wajumbe walio wachache.

Mapendekezo hayo ni kwamba ibara ya 8(1) iongezewe maneno ‘kwa kadri yatakavyohusika na utekelezaji wa mambo ya Muungano.’ Lengo la marekebisho haya ni kuhakikisha kwamba Katiba ya Shirikisho la Jamhuri inakuwa na ukuu katika mambo yote yanayohusu Shirikisho, na Katiba za Nchi Washirika zinakuwa na ukuu katika masuala yote yanayohusu Nchi Washirika ambayo sio mambo ya Shirikisho. Mapendekezo haya yatalinda u-shirikisho wa nchi yetu na mamlaka ya Nchi Washirika katika masuala yasiyo ya Shirikisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Mapendekezo haya hayaongezi kitu chochote kipya katika kamusi ya kikatiba ya nchi yetu. Hii ni kwa sababu, hata ibara ya 64(5) ya Katiba ya sasa ya Muungano inayohusu ukuu wa Katiba ya Muungano imeweka wazi kwamba ukuu huo unahusu mambo ya Muungano tu: “Bila ya kuathiri kutumika kwa Katiba ya Zanzibar ... kuhusu mambo yote ya Tanzania Zanzibar yasiyo mambo ya Muungano, Katiba hii itakuwa na nguvu ya sheria katika Jamhuri nzima ya Muungano na endapo sheria nyingine yoyote itakiuka masharti yaliyomo katika Katiba hii, Katiba ndiyo itakuwa na nguvu, na sheria hiyo nyingine, kwa kiasi inachokiuka Katiba, itakuwa batili.”

Ukuu huu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano katika mambo ya Muungano pekee unathibitishwa pia na ibara ya 4 ya Katiba ya Zanzibar inayohusu ukuu wa Katiba ya Zanzibar: “Katiba hii ni Katiba ya Zanzibar na itakuwa na nguvu za kisheria nchini kote na isipokuwa kutokana na kifungu cha 80 ikiwa sheria yoyote inatofautiana na Katiba hii, basi Katiba hii ndiyo itayokuwa na nguvu na sheria hiyo itakuwa batili kwa kiwango kile ambacho kinahitilafiana.”

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Kama ambavyo tumeeleza kwa kirefu kuhusu ibara ya 1 ya Rasimu, kwa miaka hamsini ya Muungano wetu, Serikali ya Jamhuri ya Muungano imenyakua mamlaka ya Zanzibar kwa mambo ambayo hayakuwa mambo ya Muungano kwa mujibu wa Hati ya Makubaliano ya Muungano. Hilo limefanyika kwa njia mbali mbali lakini kwa kiasi kikubwa kwa kuongeza orodha ya mambo ya Muungano kwenye Katiba au kwa kutunga sheria za kawaida na kuzifanya kuwa sheria za Muungano.

Endapo mapendekezo ya ibara ya 8 ya Rasimu yataachwa yalivyo bila kurekebishwa, athari yake kubwa itakuwa ni kufuta kabisa haiba ya u-shirikisho (federalism) ambayo imekuwa sehemu ya mfumo wetu wa kikatiba kwa nusu karne. Hakutakuwa tena na tofauti kati ya mambo ya shirikisho na mambo yasiyo ya shirikisho yaliyoko chini ya mamlaka ya Nchi Washirika.

Aidha, itakuwa ni halali kwa mamlaka za shirikisho kuingilia mambo yasiyo ya shirikisho ya Nchi Washirika kwa kisingizio cha ukuu wa Katiba ya Shirikisho. Pendekezo hili litakuwa na madhara makubwa sana kikatiba na kisiasa na litapelekea migogoro isiyoisha baina ya Nchi Washirika na Shirikisho la Jamhuri. Wajumbe walio wachache wa Kamati Namba Nne wanaliomba Bunge lako tukufu kukubali mapendekezo ya marekebisho ya ibara ya 8 ili kulinda federal character ya nchi yetu.

SURA YA SITA

IBARA YA 60

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Rasimu ya Katiba Mpya inapendekeza mabadiliko makubwa katika muundo wa Jamhuri ya Muungano katika maeneo mawili. Kwanza, ibara ya 60(1) ya Rasimu inapendekeza “... muundo wa shirikisho lenye serikali tatu ambazo ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar; na Serikali ya Tanzania Bara.”

Pili, Rasimu inapendekeza mabadiliko makubwa katika orodha ya Mambo ya Muungano. Kwa mujibu wa aya za 62(1) na 63 za Rasimu, Serikali ya Jamhuri ya Muungano itakuwa na mamlaka ya utekelezaji kwa mambo yote yaliyoorodheshwa katika Nyongeza ya Katiba kuwa Mambo ya Muungano. Mambo ya Muungano yaliyoorodheshwa katika Nyongeza hiyo ni Katiba na mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ulinzi na usalama, uraia na uhamiaji na sarafu na Benki Kuu. Mambo mengine ya Muungano ni mambo ya nje, usajili wa vyama vya siasa na ushuru wa bidhaa na mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na mambo ya Muungano. Kwa ujumla, Rasimu inapendekeza kuwa na Mambo ya Muungano saba.

Kama ambavyo tumeonyesha katika Sura ya Kwanza, suala la Mambo ya Muungano limekuwa na utata mkubwa katika miaka hamsini ya Muungano. Sasa Rasimu inapendekeza Mambo ya Muungano kuwa saba, na kati ya hayo ni Mambo matano tu – Katiba na mamlaka ya Jamhuri ya Muungano, ulinzi na usalama, uraia, uhamiaji na mambo ya nje - ambayo yalikuwepo kwenye orodha ya mwanzo ya Mambo ya Muungano. Na katika Mambo 11 yaliyoongezwa baada ya Muungano, ni mambo mawili tu – sarafu na Benki Kuu na usajili wa vyama vya siasa – ambayo yamebaki katika Rasimu. Kwa ujumla, Rasimu inapendekeza kuondoa Mambo 16 yaliyopo katika orodha ya sasa ya Mambo ya Muungano na kuongeza jambo moja jipya – ushuru wa bidhaa na mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na mambo ya Muungano – katika orodha hiyo.

Mapendekezo ya Rasimu kuhusu Mambo ya Muungano yanaashiria mabadiliko makubwa katika muundo wa sasa wa Muungano, na katika Hati za Makubaliano ya Muungano zilizosainiwa mwaka 1964. Kama tulivyoonesha kuhusu ibara ya 1 ya Rasimu, mapendekezo haya ya ibara ya 60 Rasimu hayawezi kuitwa ‘Mwendelezo wa Hati ya Makubaliano ya Muungano.’

SHIRIKISHO LA SERIKALI TATU

Mapendekezo ya muundo wa shirikisho lenye serikali tatu na Mambo ya Muungano yamezua mjadala mkubwa wa kisiasa na kitaaluma. Katika mhadhara wake juu ya Rasimu ya Kwanza, Profesa Shivji alihoji madai ya aya ya 1(3) ya Rasimu. Kwa mujibu wa Profesa Shivji, “... Hati (ya Makubaliano ya Muungano) iliweka serikali mbili; sasa iweje rasimu inayozungumzia serikali tatu iwe na msingi ambao ulijengeka kwenye serikali mbili?... Katiba iliyojikita kwenye serikali tatu haiwezi, kwa vyovyote vile, ikawa mwendelezo wa Hati (za Makubaliano ya Muungano).”

Kama lilivyo jina la mhadhara wake, hoja hii ya Profesa Shivji ina ‘utatanishi’ mkubwa, kwani kumekuwa na mabishano makubwa na ya kihistoria kuhusu tafsiri halisi ya Makubaliano ya Muungano juu ya muundo wa Muungano. Katika kitabu chake Pan Africanism or Pragmatism?, Profesa Shivji mwenyewe amedai kwamba Rais wa pili wa Zanzibar Aboud Jumbe Mwinyi na wasaidizi wake wa karibu waling’olewa madarakani mwaka 1984 kwa sababu ya kuhoji, pamoja na mambo mengine, muundo wa Muungano wa Serikali Mbili kwa madai kwamba Hati za Makubaliano ya Muungano zilikuwa zimeweka utaratibu wa muundo wa shirikisho lenye Serikali Tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Miaka kumi na saba kabla ya kuchapishwa kitabu hicho, Tume ya Nyalali iliyoteuliwa na Rais Ali Hassan Mwinyi kuchunguza kama Tanzania iendelee kuwa na chama kimoja cha siasa au vyama vingi ilipendekeza muundo wa Shirikisho lenye Serikali tatu. Mwaka mmoja baadaye, mwasisi wa Muungano na Rais wake wa kwanza, Mwalimu Nyerere aliandika yafuatayo kuhusu madai ya Rais Jumbe yaliyopelekea ‘kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa’ Zanzibar: “Huko nyuma baadhi ya viongozi wa Zanzibar wapinzani wa Muungano wamewahi kudai tufanye referendum kwa Zanzibar kuhusu Muungano. Tukakataa kwa sababu safi kabisa.”

Katika kitabu hicho hicho, Mwalimu Nyerere alisema yafuatayo juu ya kilichotokea kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano mwaka 1993:

“Tarehe 30 Julai, 1993 wakati mkutano wa bunge la bajeti ukiendelea, zaidi ya wabunge 50 kwa pamoja walitoa taarifa ya kusudio la kuwasilisha hoja Bungeni ambayo inadai (kwamba) kuendelea na mfumo huu wa Muungano usiowaridhisha wananchi wengi wa upande mmoja ni kuhatarisha kuendelea kudumu kwa Muungano.... Hivyo basi wabunge hawa wanaliomba Bunge ... liazimie kwamba Serikali ... ilete Muswada Bungeni kabla ya Februari 1994, kurekebisha katiba ya Jamhuri ya Muungano ili kuwezesha uundaji wa ‘Serikali ya Tanganyika’ ndani ya Muungano....

Tarehe 20 Agosti, 1993 wabunge wahusika waliwasilisha taarifa nyingine ... iliyokuwa inalitaka Bunge ... liazimie kwamba Serikali ... iandae kura ya maoni ambayo itafanyika kabla ya 31 Desemba, 1994 ili kupata maoni ya wananchi wa Tanzania juu ya kuundwa kwa “Serikali ya Tanganyika” ndani ya Muundo wa Muungano....”

Aidha, miaka kumi na moja kabla ya kuchapishwa kwa kitabu cha Profesa Shivji, Tume ya Kissanga iliyoteuliwa na Rais Benjamin Mkapa kuchunguza masuala mbali mbali ya kikatiba, nayo ilipendekeza muundo wa Shirikisho lenye Serikali tatu.

MUUNDO WA SERIKALI MBILI UMESHINDWA!!!

Mapendekezo ya kubadili muundo wa Muungano yaliyotolewa na Tume mbali mbali za kikatiba pamoja na Rasimu yanathibitisha mambo mawili. Kwanza, Muungano umekuwa na migogoro isiyoisha na ambayo haijapatiwa ufumbuzi hadi sasa. Jambo la pili ni kwamba, baada ya karibu nusu karne ya maisha yake, muundo wa Muungano wenye Serikali mbili umeshindwa na hauwezi tena kutatua migogoro ya Muungano.

Sehemu kubwa ya migogoro hiyo inatokana na historia ya kuanzishwa kwake. Kama ambavyo wasomi wa historia ya Muungano wameonyesha, Muungano huu ulianzishwa kwa sababu ya shinikizo la mataifa makubwa ya Magharibi yaliyokuwa na hofu kwamba Mapinduzi ya Zanzibar yangeleta siasa za kijamaa katika pwani ya Afrika Mashariki kwa sababu, mara tu baada ya Mapinduzi hayo, Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ilitambuliwa na nchi za kijamaa za wakati huo. Aidha, watawala wa nchi za Afrika Mashariki, na hasa waasisi wa Muungano Mwalimu Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume, walikuwa na hofu ya tawala zao kupinduliwa kutokana na mfano wa Mapinduzi ya Zanzibar.

Sababu zote hizi zilipelekea Muungano kufanywa kwa siri kubwa, na kwa vyovyote vile, bila kupata ridhaa ya wananchi wa Tanganyika au Zanzibar au ya vyombo vyao vya uwakilishi. Kama ambavyo tumekwishaonesha katika maoni haya, sio tu kwamba Baraza la Mapinduzi lililokuwa linatawala Zanzibar wakati huo lilikataa pendekezo la Muungano, bali pia halikutunga sheria ya kuridhia Hati za Makubaliano ya Muungano baada ya Sheikh Karume kuamua kuunganisha Zanzibar na Tanganyika bila ridhaa ya Baraza la Mapinduzi!

Kwa upande wake, Bunge la Tanganyika liliitishwa kwa dharura siku tatu baada ya kusainiwa kwa Hati za Makubaliano ya Muungano na kutakiwa kupitisha Sheria ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar siku hiyo hiyo kwa kutumia hati ya dharura! Sheria hiyo ilipitishwa bila mjadala wowote wa maana na kesho yake, tarehe 26 Aprili, 1964, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ukazaliwa rasmi! Kwa hiyo, kama ambavyo Profesa Shivji na wasomi wengine wa Muungano wameonyesha, Muungano ulizaliwa bila uhalali wa kisheria wala baraka za kisiasa za wananchi wa nchi hizi mbili.

Sehemu nyingine kubwa ya migogoro ya Muungano imetokana sio kwa sababu ya namna ulivyozaliwa, bali na utekelezaji wa masharti ya Hati za Makubaliano ya Muungano. Hii ni kwa sababu, wakati Muungano umetukuzwa katika majukwaa ya kisiasa, umekuwa ukikiukwa kwa vitendo - hasa hasa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano - wakati wote wa historia yake ya karibu miaka hamsini. Kama tulivyoonesha, mbinu kubwa iliyotumiwa kukiuka masharti ya Hati ya Makubaliano ya Muungano ilikuwa kuongeza Mambo ya Muungano kwenye orodha ya Mambo ya Muungano yaliyokuwa kwenye Hati za Makubaliano ya Muungano zilizosainiwa mwaka 1964.

‘KERO ZA MUUNGANO’ AU ‘MUUNGANO WA KERO’?

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Mfano mwingine unaoonyesha kwamba muundo wa Muungano wa Serikali Mbili umeshindwa kutatua matatizo ya Muungano ni kile kinachojulikana katika kamusi ya kisiasa ya nchi yetu kama ‘Kero za Muungano.’ Tangu kung’olewa madarakani kwa Rais Jumbe mwaka 1984, mjadala wowote juu ya ‘Hati ya Kuzaliwa’ ya Muungano – kama Jumbe alivyoziita Hati za Makubaliano ya Muungano wakati akijitetea mbele ya Kikao Maalum cha Halmashauri Kuu ya CCM – imekuwa, kwa maneno ya Jumbe, ‘dhambi.’ Na tangu wakati huo, migogoro inayohusu Mambo ya Muungano imeacha kutaja ‘Hati za Makubaliano ya Muungano’, badala yake migogoro hiyo imefichwa ndani ya lugha ya ‘Kero za Muungano.’

Kinachoitwa ‘kero za Muungano’ kiuhalisia ni migogoro juu ya Mambo mbali mbali ya Muungano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Hii inadhihirishwa na ‘Hoja za Muungano’ zilizojadiliwa katika vikao mbali mbali vilivyofanywa kati ya Serikali zote mbili kati ya Oktoba 2012 na Machi 2013: hisa za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki; usajili wa vyombo vya moto; malalamiko ya wafanya biashara wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili; mapendekezo ya Tume ya Pamoja ya Fedha; mgawanyo wa mapato; ushiriki wa Zanzibar katika taasisi za nje; utafutaji na uchimbaji mafuta na gesi asili; ajira kwa watumishi wa Zanzibar katika taasisi za Muungano; uvuvi kwenye ukanda wa uchumi wa bahari kuu; ongezeko la gharama za umeme kutoka TANESCO kwenda ZECO; na ushiriki wa Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Katika ‘hoja’ hizi ni ongezeko la gharama za umeme kati ya TANESCO na ZECO pekee ambayo haina uhusiano wowote na masuala ya Muungano. Kwa upande mwingine, hisa za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki, wafanya biashara wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili; mapendekezo ya Tume ya Pamoja ya Fedha na mgawanyo wa mapato yana uhusiano wa moja kwa moja na ‘mikopo na biashara za nchi za nje’, ‘kodi ya mapato na ushuru wa forodha’, mambo yanayohusiana na ‘sarafu na fedha’ yaliyoko katika orodha ya Mambo ya Muungano ambayo ni Nyongeza ya Kwanza ya Katiba ya Muungano.

Aidha, ushiriki wa Zanzibar katika taasisi za nje na katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ni masuala yenye uhusiano wa moja kwa moja na ‘mambo ya nchi za nje’ kwenye orodha ya Mambo ya Muungano. Vile vile, utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asili yanahusiana na ‘maliasili ya mafuta ... na gesi asilia’ katika orodha ya Mambo ya Muungano; wakati uvuvi katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari Kuu yanahusiana moja kwa moja na ‘Katiba ya Tanzania’ inayotangaza sehemu ya bahari inayopakana na Tanzania kuwa ni sehemu ya eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mwisho, ‘hoja’ ya ajira kwa watumishi wa Zanzibar katika taasisi za Muungano iko katika ‘utumishi katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano’ kwenye orodha ya Mambo ya Muungano.

UTARATIBU WA KUTATUA MIGOGORO YA MUUNGANO UMESHINDWA!!!

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Tumeonyesha jinsi ambavyo ‘Kero za Muungano’ zimekuwa sehemu ya historia yote ya Muungano. Kwa mujibu wa Katiba ya Muungano, kero hizi zinazohusu tafsiri ya masuala ya Muungano zilitakiwa kuamuliwa na Mahakama Maalum ya Katiba iliyoundwa chini ya ibara ya 125 ya Katiba. Idadi ya wajumbe wa Mahakama hiyo haijatajwa lakini ibara ya 127(1) inatamka kwamba wajumbe wake ni “... nusu ya jumla ya wajumbe wote watakaoteuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano na nusu nyingine ... watateuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.” Kwa mujibu wa ibara ya 128(2) ya Katiba, akidi ya kikao cha Mahakama hiyo ni wajumbe wote; na “kila suala linalohitaji uamuzi ... litaamuliwa kwa kufuata kauli ya theluthi mbili ya wajumbe kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya wajumbe kutoka Tanzania Zanzibar.” (ibara ya 128(3) Na kwa mujibu wa ibara ya 126(3), uamuzi wa Mahakama Maalum ya Katiba “... utakuwa ndio wa mwisho (na) hakutakuwa na haki ya kukata rufaa popote.”

Licha ya Katiba ya Muungano kuweka utaratibu huu wa kutatua migogoro ya tafsiri ya Katiba kuhusu masuala ya Muungano, Mahakama Maalum ya Katiba haijawahi kuitishwa kusikiliza migogoro mingi kuhusu tafsiri ya Katiba kuhusu masuala ya Muungano. Jaribio pekee la kukiitisha chombo hiki cha kikatiba kutatua migogoro hiyo lilizimwa mwaka 1984 wakati aliyekuwa Rais wa Zanzibar Aboud Jumbe, Waziri Kiongozi Ramadhani Haji Faki na Mwanasheria Mkuu Bashir Kwaw Swanzy walipong’olewa madarakani kwa kile kilichoitwa ‘kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa’ Zanzibar. Profesa Shivji yupo sahihi anaposema - katika Pan Africanism or Pragmatism? – kwamba ‘pengine Mahakama hiyo haikupaswa kufanya kazi’!

Badala ya kutatua matatizo ya Muungano kwa njia zilizowekwa kikatiba, Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zimeanzisha taratibu za kirasimu zilizoko nje kabisa ya mfumo wa kikatiba wa Muungano. Ndio maana Taarifa ya Utekelezaji Bajeti Mwaka wa Fedha 2012/13: Kipindi cha 01 Julai hadi 31 Desemba, 2012, iliyowasilishwa Bungeni tarehe 23 Januari mwaka huu inaelezea uratibu wa vikao vitatu vya Sekretarieti ya Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, iliyoundwa mwaka 2006 ili “... kushughulikia changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa Mambo ya Muungano....”

Vile vile, kwa mujibu wa Taarifa hiyo, vikao vya Kamati ya Makatibu Wakuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na mawaziri wa Serikali hizo vilivyokaa kati ya tareje 20 Desemba 2012 na 13 Januari 2013 vilikutana kujadili ‘Hoja za Muungano.’ Haihitaji msisitizo kusema kwamba vikao hivyo vyote havitambuliwi kikatiba. Katika mazingira haya, ni halali kuuliza swali kama pande zote mbili za Muungano zinataka kuendelea na Muungano kabla hata ya kujadili muundo wake.

MUUNGANO AU UHURU???

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Katika mhadhara wake wa kuaga Kigoda cha Mwalimu, Profesa Shivji amehitimisha uchambuzi wake wa Rasimu kwa kusema kwamba muundo wa Muungano unaopendekezwa “... ni tegemezi na ... ni dhaifu kwa sababu umejengwa juu ya mchanga wa dhamira na nia nzuri badala ya msingi wa mawe ya nguvu za kikatiba zilizowekwa na wananchi wenyewe. Ni kama kwamba suala la Muungano ni (la) ujirani mwema badala ya umoja wa nchi.” Kwingineko katika mhadhara huo, mwanazuoni huyu maarufu ‘amediriki kusema’ kwamba “muundo wenyewe wa serikali tatu uliopendekezwa (na Rasimu) ni compromise kati ya wale waliosimamia serikali mbili na wale waliopigania muungano wa mkataba, kwa maneno sahihi, kuuvunja muungano.”

Ijapokuwa hajasema wazi wazi, Profesa Shivji anaonyesha kupendelea kwamba muundo wa sasa wa Muungano wa serikali mbili ni bora zaidi na hauna budi kuendelea. Kwa maneno yake, “... compromise inazaa uamuzi legelege. Compromise juu ya muundo ... imezaa muundo wa muungano legelege. Kuna maeneo mengi ... yatazaa migogoro ambayo hatimaye inaweza kuuvunja Muungano. Kero za Muungano zitaendelea, safari hii kutoka pande zote mbili.”

Si sahihi kupuuza hoja na kauli za mwanazuoni huyu maarufu. Hata hivyo, ni muhimu kuhoji uhalali wake kwa kuangalia historia halisi ya Muungano wetu. Kwanza kabisa, kama ambavyo Profesa Shivji mwenyewe amedhihirisha katika maandishi yake ya zaidi ya miaka ishirini, Muungano huu haujawahi kuwa Muungano wa watu wa Tanganyika na Zanzibar, bali ulikuwa na umeendelea kuwa Muungano wa watawala kwa maslahi ya watawala wa ndani ya nchi yetu na wa nchi za kibeberu!

Pili, Muungano huu wa watawala haujawahi kuheshimiwa na watawala wenyewe kwa miaka yote ya uwepo wake, kama ambavyo historia ya Mambo ya Muungano na utaratibu wa kutatua migogoro yake inavyothibitisha.

Tatu, kwa kuangalia mwelekeo wa siasa za sasa za kikatiba za Zanzibar, ni wazi kwamba wananchi wa Zanzibar wanapendelea uhuru kuliko kuendelea na Muungano huu. Profesa Shivji anathibitisha hili kwa kauli yake kwamba “Wazanzibari kwa muda mrefu tu wamedai haki yao ya kujiamulia mambo yao wenyewe.” Nne, kwa sababu ya kuwa Muungano wa watawala badala ya kuwa Muungano wa wananchi; kwa sababu ya kutoheshimiwa na watawala hao; na kwa sababu ya mwelekeo wa siasa za Zanzibar za sasa, ‘Kero za Muungano’ haziwezi kutatuliwa kwa kutumia muundo wa sasa wa Serikali mbili. Compromise ya serikali tatu, katika mazingira haya, ni njia pekee iliyobaki ya kuwa na Muungano, hata kama ni muundo dhaifu na legelege kama anavyolalamika Profesa Shivji! Nje ya serikali tatu ni uhuru kamili wa ‘Washirika wa Muungano’ na kuzaliwa upya kwa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.

BILA MUUNGANO KUWEPO NI VITA???

Katika hitimisho la mhadhara wake, Profesa Shivji ametoa ‘picha ya kiama’ (doomsday scenario) endapo Muungano utavunjika kwa sababu ya kukubaliwa muundo wa shirikisho lenye serikali tatu: “Muungano ukivunjika hakuna mwananchi atakayenusurika, awe wa Tanganyika au wa Zanzibar.”

Kwingineko katika hitimisho la mhadhara huo, msomi huyu maarufu anaendeleza dhana yake ya ‘serikali tatu ni kiama’: “Suala la Muungano sio letu tu. Kuna nchi za kibeberu zina maslahi makubwa ya rasilmali pamoja na ya kijeshi katika eneo letu, hasa Bahari ya Hindi. Tukibeza mambo haya nyeti kwa sababu tu ya uchu wa madaraka ya viongozi wachache, tutawapeleka watu wetu kwenye hali mbaya.” Ili kutilia nguvu hoja yake kwamba kuvunjika kwa Muungano kutaleta vita, Profesa Shivji ametumia mifano ya vita na migogoro ya mipaka iliyotokea baada Urusi ya Kisovieti, Shirikisho la Yugoslavia na, katika Afrika, Sudan kuvunjika.

Hoja hii ya Profesa Shivji na mifano yake inastahili majibu. Kwanza, mifano aliyoitumia ni ya upande mmoja na ya kiitikadi zaidi. Hii ni kwa sababu kuna mifano ya nchi zilizovunja muungano wao bila kuwepo vita au migogoro ya mipaka. Jamhuri za Czech na Slovakia zilizotokana na kuvunjika kwa Jamhuri ya zamani ya Czechoslovakia ni mfano mzuri. Haiyumkini kwamba Profesa Shivji anaufahamu mfano huu vizuri.

Pili, kuna nchi nyingi ambazo zimepigana vita ya wenyewe kwa wenyewe kwa muda mrefu kwa sababu ya kulazimisha muungano usiokubaliwa na upande mmoja au mwingine katika umoja huo. Ethiopia na Eritrea ni mfano mmojawapo. Mwaka 1952 Ethiopia ilisaini makubaliano kati yake na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa yaliyoifanya Eritrea sehemu ya Shirikisho la Ethiopia na hivyo kumaliza utawala wa Uingereza katika koloni hilo la zamani la Italia.

Hata hivyo, tarehe 14 Novemba, 1962, Mfalme Haile Selassie I wa Ethiopia alivunja makubaliano hayo kwa nguvu na kuifanya Eritrea kuwa sehemu ya Himaya yake. Vita vya ukombozi vilivyosababishwa na kitendo hicho vilichukua karibu miaka thelathini hadi Ethiopia iliposhindwa mwaka 1991 na Eritrea kujipatia uhuru kamili. Vile vile Profesa Shivji anaufahamu mfano huu vizuri sana, kwa sababu alikuwa mmoja wa wanazuoni wengi waliounga mkono wa Chama cha Ukombozi wa Watu wa Eritrea (Eritrean People’s Liberation Front - EPLF), kilichoongoza mapambano ya uhuru wa nchi hiyo.

Sudan ya zamani ni mfano mwingine wa vita vilivyosababishwa na kulazimisha muungano usiotakiwa na upande mmoja. Mnamo Februari, 1953, Uingereza na Misri zilizokuwa zinatawala Sudan ya Kusini na ya Kaskazini kama maeneo tofauti kwa utaratibu wa Condominium zilikubaliana kukabidhi uhuru kwa shirikisho la Sudan ifikapo tarehe 1 Januari, 1956. Hata hivyo, kabla ya tarehe hiyo kufika, viongozi wa Sudan Kaskazini walikiuka makubaliano ya kuunda serikali ya shirikisho. Matokeo yake ni kwamba wananchi wa Sudan Kusini waliasi na kuanzisha kile kinachojulikana katika historia kama Vita ya Kwanza ya Wenyewe kwa Wenyewe ya Sudan (First Sudanese Civil War au Anyanya I Rebellion). Vita hiyo ilianza Agosti, 1955 na ilimalizika kwa kusainiwa kwa Makubaliano ya Amani ya Addis Ababa ya mwaka 1972. Makubaliano hayo yalirudisha mfumo wa Shirikisho ulioipa Sudan Kusini mamlaka makubwa ya utawala wa ndani. Makubaliano ya Addis Ababa hayakudumu muda mrefu kwa sababu Serikali Kuu ya Sudan iliyahujumu. Matokeo yake, mwaka 1978 Maasi ya Anyanya II yalianza tena. Makubaliano ya Addis Ababa yalivunjika kabisa mwaka 1983 na Vita ya Pili ya Wenyewe kwa Wenyewe ya Sudan (Second Sudanese Civil War) ilianza mwaka 1983 hadi ilipoisha baada ya kusainiwa kwa Mkataba wa Amani wa Nairobi wa tarehe 9 Januari, 2005.

Chini ya Mkataba wa Amani wa Nairobi, Sudan Kusini ilijitawala kwa masuala ya ndani kwa miaka sita hadi 2011 wananchi wa Sudan Kusini walipopiga kura ya maoni na kuamua kujitenga na Sudan ya Kaskazini. Tarehe 9 Julai, 2011, Jamhuri ya Sudan Kusini ilizaliwa kama nchi huru. Ni kweli kwamba bado kuna mgogoro wa mpaka kati ya Jamhuri hiyo mpya na Sudan Kaskazini. Hata hivyo, mgogoro huo hauwezi kulinganishwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe iliyochukua miaka hamsini kuanzia 1955 hadi 2005! Hapana shaka kwamba Profesa Shivji anaifahamu historia hii vema, kwani zama za ujana wake alisoma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na Dk. John Garang, mwasisi wa Chama/Jeshi la Ukombozi wa Watu wa Sudan (Sudanese People’s Liberation Movement/Army – SPLM/A).

Tatu, zipo nchi ambazo zinaendelea kuwa na vita kwa sababu ya kulazimisha umoja ambao upande mmoja unaukataa. India (mgogoro wa Jimbo la Kashmir), Hispania (Jimbo la Basque) na Angola (Jimbo la Cabinda) ni mifano mizuri. Ni vigumu kuamini kwamba Profesa Shivji hafahamu mifano ya nchi hizi pia. Ni wazi, kwa hiyo, kwamba hoja serikali tatu = kuvunja Muungano = vita na maangamizi ni hoja yenye lengo la kutisha wananchi ili wasiweze kujadili masuala yote yanayohusu Muungano ikiwamo kuachana nao.

Na nne, hoja ya Profesa Shivji kwamba wanaodai kuwe na Muungano wa shirikisho lenye serikali tatu ni ‘viongozi wachache’ wenye ‘uchu wa madaraka’ ni ya kusikitisha sana. Hii ni sawa sawa na kuwaita Rais Aboud Jumbe na wasaidizi wake, au wajumbe wa Tume ya Nyalali, au ya Kissanga au hata ya sasa ya Warioba, au Wabunge wa G55, waroho wa madaraka kwa sababu tu hawakukubaliana na mfumo wa serikali mbili ambao Shivji mwenyewe amekiri mara nyingi umeshindwa kutatua matatizo na ‘Kero za Muungano’!

SERIKALI TATU NI GHARAMA KUBWA!!!

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Tangu kuchapishwa kwa Rasimu, kumejitokeza kauli kwamba kuwa na muundo wa Muungano wenye serikali tatu itakuwa ni gharama kubwa kwa nchi maskini kama ya kwetu. Viongozi na makada wa CCM wameidaka hoja hii ya gharama za Muungano kama ndio turufu yao ya kuendelea na muundo wa sasa wa Muungano wa Serikali mbili. Katika Ufafanuzi wake, CCM imedai kwamba “gharama za uendeshaji wa Serikali zilizopo hivi sasa ni kubwa. Kuwepo kwa Serikali ya tatu kutakuwa ni gharama ya ziada na hivyo kuwa mzigo mkubwa kwa wananchi.”

Kwa upande wake, Profesa Shivji amezungumzia suala hili kama ifuatavyo: “Kwa upande wa gharama, ni wazi kwamba kuendesha serikali ya muungano kutakuwa na gharama kubwa. Kazi inayofanywa na taasisi moja au idara moja katika muundo uliopo sasa itahitaji taasisi mbili. Kwa mfano, badala ya kuwa na Tume moja ya uchaguzi, sasa kutakuwa na tume mbili, moja ya Muungano na nyingine ya Bara. (Ukiongeza ya Zanzibar kutakuwa na Tume tatu za uchaguzi. Na hivyo hivyo kuhusu tume nyingine. Ukiangalia juu juu tu, licha ya taasisi na idara za kawaida katika serikali, kuna tume karibu nane na mabaraza mawili yenye wajumbe wazito ambao bila shaka watakuwa na mishahara minono na marupurupu poa. Wananchi wamekwishaanza kuonyesha wasiwasi wao kwa kuwaongezea mzigo wa kubeba serikali kamili nyingine, zaidi ya hizi mbili tulizonazo.”

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Hoja hii ya gharama za kuendesha serikali tatu ni red herring, yaani ina lengo la kuwatoa wananchi kwenye mjadala wa msingi juu ya kushindwa kwa muundo wa sasa wa Muungano kutatua ‘Kero za Muungano’, kwa kuwaaminisha kwamba muundo wa sasa una gharama nafuu zaidi kuliko muundo wa serikali tatu. Kwanza, kwa kadri ya ufahamu wetu, hadi sasa hakuna mtu yeyote aliyefanya uchambuzi wa ulinganifu wa gharama za kuendesha serikali – iwe moja, mbili au tatu – katika nchi yetu. Hata Ufafanuzi wa CCM uko kimya juu ya jambo hili. Kwa sababu hiyo, hakuna ushahidi wowote wa kuthibitisha kwamba kuendesha serikali tatu ni ghali zaidi kuliko kuendesha serikali mbili. Kwa vyovyote vile, kama suala la gharama za kuendeshea serikali ndio jambo muhimu zaidi katika kuamua muundo wa Muungano, kwa nini tusiwe na serikali moja tu, kuliko mbili za sasa au tatu zinazopendekezwa na Rasimu?

Pili, na muhimu zaidi, kama tukichukua mapendekezo ya Mambo ya Muungano kama kigezo cha kupima ukubwa wa serikali – na kwa hiyo gharama za kuiendeshea – basi gharama za serikali ya Muungano zinaweza kuwa ndogo sana. Hii ni kwa sababu, haiwezekani – kwa mambo saba ya Muungano yanayopendekezwa na Rasimu – kuwa na serikali kubwa ya Muungano. Kwa Mambo hayo ya Muungano, hakutakuwa na zaidi ya wizara nne za Serikali ya Muungano. Hivyo, kwa mfano, kutakuwa na wizara ya katiba na sheria itakayoshughulikia masuala ya Katiba na mamlaka ya Jamhuri ya Muungano; wizara ya ulinzi itakayokuwa na majukumu ya ulinzi na usalama wa Jamhuri ya Muungano; wizara ya fedha itakayoshughulikia masuala ya sarafu na benki kuu, na ushuru wa bidhaa na mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na Mambo ya Muungano; na wizara ya mambo ya nje. Masuala yaliyobaki, yaani uraia na uhamiaji na usajili wa vyama vya siasa hayastahili kuwa na wizara zinazojitegemea kwa hiyo yanaweza kuwekwa chini ya mojawapo ya wizara zilizotajwa hapo juu.

Ibara ya 98(2) ya Rasimu inapendekeza ukomo wa ukubwa wa Baraza la Mawaziri la Jamhuri ya Muungano kuwa mawaziri wasiozidi kumi na tano. Kwa upande mwingine, ibara ya 98(3) inaelekeza kwamba “Serikali ya Jamhuri ya Muungano itakuwa na Wizara kwa kuzingatia mamlaka ya Serikali kwa mujibu wa Katiba hii.” Sasa kama mamlaka ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano yako kwenye mambo saba ya Muungano kwa mujibu wa Rasimu hii, je, hao mawaziri wasiozidi kumi na tano watatoka wapi na watatimiza majukumu gani? Ni wazi kabisa kwamba mapendekezo ya ibara ya 98(2) yanakinzana na matakwa ya ibara za 62(1) na 63 zinazohusu mamlaka ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano juu ya Mambo ya Muungano.

Kwa mtazamo huo huo wa ibara ya 98(3) na orodha ya Mambo ya Muungano kama kipimo cha ukubwa wa Serikali ya Muungano, taasisi nyingine zinazopendekezwa na Rasimu haziwezi kuwa kubwa sana na nyingine hazitakuwepo kabisa. Kwa mfano, Katibu Mkuu Kiongozi na Makatibu Wakuu wanaopendekezwa katika ibara za 105 na 106 za Rasimu hawawezi kuzidi idadi ya Wizara nne zilizotajwa hapo juu zitakazoshughulikia Mambo ya Muungano. Kwa maana hiyo, kwa kuzingatia idadi ya Makatibu Wakuu wenyewe, Kamati Maalumu ya Makatibu Wakuu inayoelezwa katika ibara ya 107; na Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri inayotajwa katika ibara ya 108, hazina maana wala umuhimu wowote kikatiba.

Au tuchukue mapendekezo yanayohusu Bunge la Jamhuri ya Muungano. Kwa mujibu wa ibara ya 105(4) ya Rasimu, kila Jimbo la Uchaguzi litawakilishwa na wabunge wawili kwa kuzingatia jinsia zao. Ibara ya 113(2)(a) inabainisha ‘Jimbo la Uchaguzi’ kuwa ni kila mkoa kwa upande wa Tanzania Bara na wilaya kwa upande wa Zanzibar. Aidha, kwa mujibu wa ibara ya 113(2)(b), kutakuwa na wabunge watano wa kuteuliwa na Rais kuwakilisha watu wenye ulemavu. Tukichukua idadi ya mikoa ishirini na tano ya Tanzania Bara na wilaya 10 za Zanzibar kwa sasa, Bunge la Jamhuri ya Muungano litakuwa na wabunge 75.

Kwa mapendekezo ya muundo wa serikali tatu, Bunge la Zanzibar litakuwa na Wabunge hamsini wa majimbo ya sasa ya uchaguzi; wakati bunge la Tanganyika litakuwa na wabunge 189 wa majimbo ya uchaguzi ya sasa. Kwa maana hiyo, muundo wa Muungano wa serikali tatu utakuwa na mabunge matatu yenye jumla ya wabunge 314.

Kwa kulinganisha, Bunge la Jamhuri ya Muungano la sasa lina idadi ya wabunge 239 wa majimbo ya uchaguzi – 189 wa majimbo ya uchaguzi ya Tanzania Bara na hamsini ya Zanzibar. Vile vile, kuna wabunge 102 wa Viti Maalumu, 10 wa kuteuliwa na Rais na watano wanaowakilisha Baraza la wawakilishi Zanzibar na Mwanasheria Mkuu, kwa idadi ya jumla ya wabunge 357.

Kwa upande wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, kuna wawakilishi hamsini wanaowakilisha majimbo ya uchaguzi, kumi wa kuteuliwa na Rais wa Zanzibar, ishirini wa Viti Maalum na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, kufanya jumla ya wawakilishi themanini na moja. Kwa maana hiyo, kwa muundo wa sasa wa Muungano, mabunge mawili tuliyonayo yana idadi ya wabunge 438. Idadi hiyo ni kubwa kuliko idadi ya wabunge wa mabunge matatu yatakayokuwepo chini ya muundo wa serikali tatu kwa wabunge 124!

Na sio Bunge ambalo linaweza kuwa na gharama ndogo kuliko gharama za sasa. Taasisi za Muungano zinazopendekezwa kama vile Tume ya Uhusiano na Uratibu wa Serikali (ibara ya 109); Tume ya Utumishi wa Mahakama (ibara ya 180); na Tume ya Utumishi wa Umma (ibara ya 186) haziwezi kuwa kubwa sana kwa kuzingatia ukubwa wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa Rasimu.

Aidha, uwepo wa taasisi nyingine kama vile Tume ya Maadili ya Uongozi na Uwajibikaji (ibara ya 200) na Tume ya Haki za Binadamu (ibara ya 208) unakinzana na matakwa ya aya za 62(1) na 63 za Rasimu na kwa hiyo haziwezi kugharimiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano!

Vile vile, majukumu ya utekelezaji wa Mambo mengine ya Muungano kama uchaguzi na usajili wa vyama vya siasa yanaweza kutekelezwa na taasisi husika za Washirika wa Muungano kwa makubaliano na masharti maalumu chini ya aya ya 59(3) ya Rasimu. Hii nayo itapunguza gharama za kuendesha Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Ni wazi – kwa mtazamo huu – kwamba gharama za kuendeshea muundo wa shirikisho lenye serikali tatu zinaweza kuwa hata ndogo kuliko gharama za kuendeshea muundo wa Muungano wa serikali mbili za sasa.

FAIDA ZA MUUNGANO NI KWA WAZANZIBARI PEKE YAO?

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Pendekezo la Rasimu kuhusu muundo wa Serikali tatu limeleta hoja juu ya faida za Muungano kwa kila upande wa Washirika wa Muungano. Hivyo, kwa mfano, katika Ufafanuzi wake CCM imedai kwamba pendekezo hili litaleta “... urasimu na utata wa kisheria katika umiliki na uendeshaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii.” CCM inafafanua zaidi juu ya jambo hili: “Urasimu wa kibiashara na umilikaji ardhi utaongezeka kwa sababu biashara, ardhi na umilikaji wa mali wa aina nyingine si mambo ya Muungano.”

Kwingineko katika Ufafanuzi wake, CCM inadhihirisha kwamba msimamo wake juu ya muundo wa Serikali tatu unatokana na hofu ya athari za muundo huo kwa maslahi ya kiuchumi ya Wazanzibari walioko, au wenye vitega uchumi, Tanzania Bara. Hivyo basi, “muundo wa Serikali mbili una urasimu mdogo wa kisheria na hivyo kutoa fursa nyingi za kiuchumi na kijamii hususan kwa Wazanzibari ambao eneo lao la ardhi ni dogo wakati idadi ya wakaazi inaongezeka mwaka hadi mwaka.” Aidha, kwa mujibu wa CCM, “muundo uliopo unawawezesha Wazanzibari kumiliki ardhi na rasilmali nyingine zilizoko Tanzania Bara kama raia wa Tanzania, ingawaje ardhi na rasilmali nyingine za kiuchumi si masuala ya Muungano.”

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Inajulikana kwamba, kwa mujibu wa sheria za Zanzibar, Watanzania Bara hawana haki ya kumiliki ardhi Zanzibar, licha ya kuwa raia wa Tanzania. Aidha, licha ya kuwa raia wa Tanzania, Watanzania Bara wanaoajiriwa katika sekta binafsi Zanzibar wanatakiwa kutimiza masharti ya vibali vya ajira sawa na raia yeyote wa nchi za kigeni. Yote haya ni nje ya ukweli kwamba Watanzania Bara hawawezi kuajiriwa katika taasisi yoyote ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, tofauti na Wazanzibari ambao wanaajiriwa na taasisi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano hata kwa mambo yasiyokuwa ya Muungano.

Vile vile, yote haya ni nje ya ukweli kwamba wakati Wazanzibari wanaweza kikatiba kushiriki shughuli za kisiasa na kiutawala Tanzania Bara hata kwa mambo yasiyokuwa ya Muungano, Watanzania Bara hawana uwezo huo. Hivyo basi, kwa utaratibu huu, Wabunge wa Zanzibar katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wanashiriki katika mijadala ya mambo yasiyo ya Muungano ya Tanzania Bara, Wazanzibari wanashikilia nafasi za juu za kisiasa kama vile uwaziri katika wizara zisizokuwa za Muungano na Baraza la Wawakilishi Zanzibar lina uwakilishi maalum katika Bunge la Jamhuri ya Muungano. Wananchi wa Tanzania Bara hawana haki ya kushiriki katika mambo haya kwa upande wa Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Upinzani wa CCM dhidi ya pendekezo la Rasimu juu ya muundo wa Serikali tatu unadhihirisha ushawishi mkubwa wa Zanzibar katika siasa za ndani ya CCM, hasa hasa katika zama hizi za vyama vingi na vita za makundi mbali mbali ndani ya chama hicho. Katika mazingira haya, mtu yeyote anayetaka kupitishwa kuwa mgombea urais kwa kupitia CCM anakuwa anahitaji kura za CCM Zanzibar ili kushinda katika kinyang’anyiro hicho.

Kwa kauli ya Mwalimu Nyerere katika kitabu chake Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania: “Sababu moja kubwa iliyofanya viongozi wetu wasitake kuwaudhi ‘Wazanzibari’ ... ni umuhimu wa kura za Zanzibar katika kumteua mwanachama wa CCM kuwa Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano. Kwa kiongozi yeyote anayeliona jambo hilo kuwa ni muhimu kupita mengine yote, kuwaudhi ‘Wazanzibari’ ni dhambi ambayo haina budi iepukwe kwa kila njia.” Hofu hii ya ‘kuwaudhi’ Wazanzibari ndio imepelekea CCM kutaka kulinda maslahi ya kiuchumi ya Wazanzibari kwa kukataa muundo wa Serikali tatu.

No comments:

Post a Comment