Waziri Mulugo: Aliaibisha Taifa- Asema "Tanzania ilitokana na muungano wa visiwa vya Pemba na Zimbabwe"!
Naibu
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo
Naibu
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, amemwaibisha Rais
Jakaya Kikwete na taifa kwa ujumla mbele ya jamii ya kimataifa, baada
ya kuitangazia dunia kuwa Tanzania imetokana na muungano wa visiwa vya
Zimbabwe na Pemba vilivyoungana na Tanganyika.
Mbali na hilo,
aliwaambia mamia ya wajumbe kutoka mataifa mbalimbali katika Bara la
Afrika kuwa, Tanzania ilizaliwa mwaka 11964.
“Wasilisho langu
litakuwa na sehemu saba…Utangulizi, Tanzania iliundwa mwaka 11964 kwa
kuunganisha visiwa vya Bahari ya Hindi vya Zimbabwe na Pemba
vilivyoungana na nchi ya Bara iliyokuwa ikiitwa Tanganyika…,” alisema
Naibu Waziri Mulugo kwa kujiamini na bila kuonyesha dalili yoyote kuwa
alikuwa amekosea.
Naibu waziri huyo alikuwa akiwasilisha mada
katika mkutano wa viongozi na wataalamu wa elimu katika Bara la Afrika,
ambao ulifanyika Afrika Kusini kuanzia Oktoba 5-7, mwaka huu.
Kuboronga huko kwa naibu waziri huyo kumeibua mjadala mkubwa na mzito
miongoni mwa Watanzania wa kada na rika mbalimbali, huku wengi wakianza
kupata wasiwasi juu ya uwezo wa watu wanaoteuliwa na Rais Kikwete
kushika nyadhifa mbalimbali serikalini.
Watu wengi waliotoa
maoni yao juu ya suala hili kupitia mitandao ya kijamii ya Jamii Forum,
Wanabidii, Facebook na Twiter wameonyesha wasiwasi mkubwa na kiwango cha
elimu na weledi wa Mulugo na kuuliza swali; “elimu ya waziri huyu
inatosheleza kumudu majukumu yake ya Naibu Waziri wa Elimu?”
Wasifu wa Naibu Waziri Mulugo uliopatikana kupitia mtandao wa Google,
unaonyesha kuwa ana elimu ya shahada ya kwanza aliyoipata kutoka Chuo
Kikuu Huria cha Tanzania, kati ya mwaka 2002 na 2008.
Anadai
katika wasifu huo kuwa kabla ya kuingia chuo kikuu, amesoma katika shule
za sekondari za Songea Boys High School kwa masomo ya kidato cha tano
na sita kuanzia mwaka 1994 mpaka 1996, na Sekondari ya Mbeya kwa masomo
ya kidato cha kwanza mpaka cha nne kuanzia mwaka 1990 mpaka 1993.
Mulugo amejieleza kuwa kati ya mwaka 2000 na 2004 alifanya kazi ya
ualimu katika Shule ya Sekondari Southern Highland, huku akiwa hajapata
mafunzo yoyote ya taaluma ya ualimu.
Alipotafutwa kwa njia ya
simu kufafanua alivyojieleza, Waziri Mulugo alisema alikuwa mjini Dodoma
kuhudhuria kikao cha Baraza la Mawaziri, hivyo hakuwa na muda wa
kuzungumza na Blog hii.
No comments:
Post a Comment