Ushauri wa bure kwa CHADEMA kuelekea 2014-2015!
Kanda ya MASHARIKI Dar es Salaam na Pwani ni
miongoni mwa Kanda kumi zilizoundwa ili kukidhi mkakati wa M4C na Chaguzi ndani
ya Chama, aidha mfumo huu unatumika kama mwanzo wa utekelezaji wa mapendekezo ya
sera ya majimbo ambayo CHADEMA imekuwa ikipendekeza kwenye Ilani yake ya Uchaguzi
kipindi cha Kampeni 2010, lengo ikiwa kupunguza Madaraka ya Rais na ukubwa wa
Serikali ili kuharakisha maendeleo kwa
kutumia rasilimali za maeneo husika. Kanda zingine ni KUSINI ambayo ni Lindi na Mtwara, KASKAZINI Kilimanjaro, Arusha na Manyara,
KANDA YA KATI Morogoro,
Dodoma na Singida, NYANDA
ZA JUU KUSINI Njombe, Iringa, Mbeya na Ruvuma,
MAGHARIBI Rukwa, Katavi, Tabora na Kigoma, Kanda ya ZIWA MASHARIKI
Shinyanga, Simiyu
na Mara, ZIWA MAGHARIBI Mwanza, Geita na Kagera na kwa
upande wa ZANZIBAR Pemba na Unguja.
Kamati Kuu katika Kikao cha
tarehe 09/11/2012 iliazimia kwamba, mara baada ya Muundo wa Kanda kukamilika na
waratibu wa Kanda kuajiliwa, M4C inatakiwa kuongoza zoezi la Uchaguzi wa ndani ya Chama. Uchaguzi wa Chama
unatakiwa kukamilika ndani ya mwaka 2013. Mapendekezo haya yalitolewa mwanzoni
mwa mwaka 2011, baada ya kubaini kwamba tunapokwenda kwenye Uchaguzi wa Chama
na wakati huo huo kuna Chaguzi za Kiserikali madhalani kuchagua Wenyeviti wa Serikali
ya Vijiji/Serikali ya Mtaa karibu na
Uchaguzi Mkuu inaleta mkanganyiko mkubwa ndani ya Chama kama vile kushughulikia
rufani mbalimbali za wagombea ambao kwa
namna moja au nyingine hajaridhika na matokeo katika chaguzi ndani ya chama na
wakati mwingine kusababisha kukosa ushindi, hivyo msisitizo ukawa Uchaguzi
ndani chama unatakiwa ufanyike mapema kabla ya Chaguzi za Kiserikali bila
kuathili Utaratibu wa Uchaguzi kama Katiba ya Chadema inavyoelekeza katika Sura ya Sita Ibara ya 6.3.1 (a) – (e) na Muda wa Uongozi Ibara ya 6. 3 . 2 kifungu (a) – (e)
Lakini mpaka naandika makala hii kumekuwa
na sintofahamu ya muda mrefu kwa wanachama wengi na baadhi ya viongozi hasa wa
Ngazi ya Misingi, Matawi na Kata kuhusu mienendo ya uendeshaji wa shughuli za
chama hususani baada ya hizi kanda kuanzishwa, pia kumekuwa na ukiukwaji mkubwa
wa Katiba ya chama tangu Uanzishwaji wa hizi Kanda, kumekuwa na Mifumo
kandamizi na lazimishi bila kufuata Kanuni, Misingi, Falsafa na Itifaki za
CHAMA kwa kuzingatia wajibu na nafasi ya kila Kiongozi katika eneo lake la
kazi.
Kuna zoezi la CHADEMA ni MSINGI
ambalo limekuwa ni Siri. Na limekuwa siri
kwa viongozi waliopo bila kujua kinachoendelea ni kitu gani ambacho ni
Siri katika Ujenzi wa Chama mpaka wengine msishirikishwe. Lakini zoezi
limegundulika kuwa ni maandalizi ya kuelekea CHAGUZI za ndani ya CHAMA aidha waendeshaji wa mazoezi haya wanafanya
kwa interests zao yaani kujijenga na sio kujenga CHAMA ndio maana hawapiti kwenye ofisi za Chama wala kuwaona viongozi wa
Kata husika. Kwa madai kwamba wamefundishwa
wasiitumie Katiba ya chama kama mwongozo na pia wasipite kwenye Ofisi wala
kuuona Uongozi uliopo isipokuwa watumie mbinu kutoka kwenye kitabu cha mafunzo na
Programme za Chama kuanzisha Misingi na Brigedi Nyekundu (Kikosi cha Ulinzi) na
kamwe wasiwahusishe wadau kama vile Uongozi wa Wilaya/Jimbo au Kata na
anayefahamu ni Mbunge pekee na watu wachache waliohudhuria Mafunzo hayo katika
Mkoa wa DODOMA, “anayeona
zoezi hili si shirikishi mlango upo wazi anaweza kujiondoa CHADEMA” je
kauli kama hizi za kuogofya ni nzuri kwenye muktadha wa afya ya Demokrasia ?
Ukitaka kujua njia hata zilizotumika
ni haramu na kufanya zoezi lote kuwa
haramu hata namna ya kuwapata watu walioenda kuchukua mafunzo, hakuna waraka
wowote kwenda kwenye Majimbo/Wilaya, Kata au Matawi ambayo ndio yenye watu
kutoka kwenye Misingi wala hakukua na vigezo vilivyotolewa kwa ajili Ushiriki
wa Semina ya Mafunzo. Kwa mfano utaratibu huu uliokiuka Katiba ya Chama umeleta
mkanganyiko mkubwa hasa katika Jimbo la Kawe. Aidha haya yote yamefanywa sio
kwa bahati mbaya, ni kwa makusudi kwa sababu Jimbo la Kawe ni jimbo ambalo lilikuwa na mgogoro
wa muda mrefu dhidi ya ugumu wa kuwandoa viongozi waliokula Fedha za Jimbo (
Ruzuku iliokuwa ikitolewa kila mwezi na Chama ), lakini kuna msemo usemao
“usipo stahajabu ya Musa utayaona ya firahuni”, hao mafisadi ndio miongoni mwa waliopata nafasi ya kuhudhuria
mafunzo ya CHAMA na ndio wamekuwa
wakufunzi wa CHADEMA ni MSINGI na Kamanda Mkuu wa Red Brigade katika lilelile
Jimbo wanalotuhumiwa na hakuna chombo ama Kikao chochote cha Chama
kilichowasafisha tangu mwaka jana hadi tarehe 6 mwezi January 2013 wakati
Kamati ya Kikosi Kazi ya Jimbo kuundwa.
Mtindo wanaoutumia ni njia ya
kupigiana simu na wakati mwingine kutafuta sehemu iliojificha na endapo
watabahatika kumpata mwanachama au mpenzi wa CHADEMA ambao hawajui tuhuma zao
katika eneo husika wanamwapisha asitoe taarifa yoyote kwa Mwenyekiti au Katibu wake wa Msingi,
Tawi au Kata katika eneo lake kwa gia ya kuwaaminisha kuwa mkakati huo wa
programme ya Chadema ni MSINGI ni sawa na Usalama wa Taifa hivyo haipaswi Kiongozi
wako kujua wala kuhoji.
Ki-ukweli na ki-uhalisia zoezi linaloendelea
katika Kanda ya Mashariki Dar es Salaam na Pwani hususani katika JIMBO
LA KAWE sijui hali ikoje katika Majimbo ya TEMEKE, UKONGA, ILALA, SEGEREA,
KIGAMBONI, UBUNGO na KINONDONI ni zoezi tenganifu na si shirikishi isipokuwa
linaleta makundi na migogoro isiyo ya lazima kati ya viongozi waliopo na
vikundi vinavyoundwa bila Kamati tendaji za viongozi husika katika Kata au Tawi
kwa maana ya Mtaa kushiriki. Jambo hili linaweza likaonekana dogo na kubezwa na Uongozi wa Kitaifa
na wakati mwingine hoja zao zinaweza zikapuuzwa kwa sababu mbalimbali; mfano wa kipuuzi kusema
Chama hakipo
kwenye eneo fulani au kazi
haziendi na kufikiri mifumo kandamizi ambayo siyo shirikishi ndio bora katika
Ujenzi wa Chama kuelekea 2014 na 2015 Uchaguzi wa Serikali ya Mtaa na Uchaguzi
Mkuu.
Demokrasia ndio Msingi Mkuu wa
kutoa haki sio tu ya kuomba Uongozi na kupigiwa kura au fursa ya kupiga kura
bali pia kushirikishwa kikamilifu na kutoa mawazo pia kupata taarifa sahihi. Kwa mujibu wa nyaraka mbalimbali kuhusu Ujenzi
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo ( CHADEMA ) haioneshi kuwabagua viongozi
wa kada mbalimbali katika Chama, lakini hili zoezi la CHADEMA ni Msingi ambayo dhana
yake inatokana na operation za M4C
zinaendeshwa kwa minajili ya kuwatenga baadhi ya viongozi ambao kwa namna moja au nyingine
wameonekana wakifanya kazi za Chama bila ya kujipendekeza kwa wabunge au
madiwani wao, dhana yao kubwa ikiwa ni kusimamia Falsafa, Kanuni na Misingi ya Chama,
aidha wameonekana kuwa mwiba kwa watu wachache wenye maslahi binafsi na kuamua kutumia nafasi au uwezo wao kuwatenga.
Hili jambo limeshaanza kuleta
mpasuko na mgogoro mkubwa, na ikiwa viongozi husika wa Kanda ya Mashariki au
Makao Makuu wasipofanyia kazi maoni na ushauri wa wadau hasa viongozi linaweza
kuwa janga hasa katika Kanda yetu ya Dar es Salaam na Pwani. Nini kifanyike, napendekeza kwamba hatua za
haraka zifanyike kwa Wakuu wa Kanda kukutana na Kufanya Vikao vya Majadiliano
na wadau ambao watakuwa viongozi wa Jimbo/Wilaya na Viongozi wote wa Kata
katika kila Jimbo kwa nyakati tofauti ili kupata njia bora na nyepesi ambayo
itawashirikisha viongozi wote bila kuwabagua.
Pili napendekeza pia programu
zote katika Ujenzi wa Chama zihakisi mifumo yote ya Kiongozi Kikatiba kwa
kufuata na kuzingatia falsafa, kanuni na itifaki za Chama.
Na mwisho ninaonya lugha za
kibaguzi kutumika wakati wa kutengeneza team work, mfano kutumia maneno kwamba, "unajua viongozi wengi ni
wakukaimishwa na mamluki" lugha hizo zisitumike au kitendo cha Kiongozi au Mwanachama kusema "mimi tu na fulani ndio tulichaguliwa" iwe
kwenye Ngazi ya Wilaya/Jimbo au Kata, haiwezi kuleta dhana ya ujumla ya kupoka matumizi ya Katiba ya Chama
katika shughuli za Ujenzi wa Chama; ikumbukwe kila zoezi la muundo wa Ujenzi wa
Chama ikiwemo Chadema ni Msingi ni lazima izingatie mashariti ya: Muundo wa Uongozi wa Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) unaanza Ngazi ya chini kabisa ambayo
ndio Msingi wa CHAMA kwa mujibu wa KATIBA YA CHAMA Ibara ya 7.1.1 ikifuatiwa na Ngazi zingine Tawi Ibara ya 7.2.1 , Kata
Ibara ya 7.3.1, Wilaya/ Jimbo la Uchaguzi Ibara ya 7.4.1 , Mkoa Ibara ya 7.5.1
na Ngazi ya juu kabisa ni Ngazi ya Taifa Ibara ya 7.7.1.
Athari na adha ya zoezi hili zimekwisha anza
kujitokeza kwenye baadhi ya majimbo mbalimbali katika Mkoa wa Dar es Salaam
inawezekana tukapuuza kama tulivyozoea kujipa matumaini ya kusadikika bila
kufanya utafiti au kufika kwa wadau na kuhoji ni nini hasa kinachopingwa katika
zoezi hili zuri lisilo na malipo ambalo kila Kiongozi angependa kushiriki kwa
uwazi na hatimaye kutengeneza timu nzuri ili kufikia malengo ya Programu ya
CHADEMA ni MISINGI kwa wakati. Tuchukue hatua
Mapema
CHADEMA TUMAINI LA WATANZANIA
Na: Msomaji wetu
No comments:
Post a Comment