Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema
Mabilioni ya shilingi yaliyowekwa na Watanzania katika benki za Uswisi yameanza kuhamishwa kimyakimya.
Ripoti ya Benki za Uswisi ya 2012 inaonyesha kuwa fedha zinazotoka Tanzania zimepungua kwa karibu Sh.36.4 bilioni ikilinganishwa na zilizokuwapo 2011 nchini humo, lakini haielezi sababu ya kupungua kwake.
Taarifa za kuhamishwa kimyakimya kwa fedha hizo ambazo zinaaminika kuwekwa na Watanzania waliowahi kuwa katika utumishi wa umma, imekuja wakati ambao Serikali inasubiriwa kutoa taarifa yake kuhusu vigogo walioficha fedha nchini humo, ambazo zinaaminika walizipata kwa njia zisizo halali.
Awali, kiasi cha fedha kilichotajwa kufichwa katika benki hizo ni Sh.327.9 bilioni (Dola za Marekani 204.96 milioni), lakini taarifa mpya ya 2012 inaonyesha kuwa kiasi hicho kimepungua hadi Dola za Marekani 182.2 milioni (Sh.291.5 bilioni).
Kiasi hicho cha fedha kinaweza kujenga barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 300 ambao ni sawa na kutoka Morogoro hadi Iringa.
Akizungumzia ripoti hiyo, Balozi wa Uswisi nchini, Olivier Chave alisema: “Hadi mwisho wa 2012, fedha zilizopo kutoka Tanzania zimebaki Faranga za Uswisi 160 milioni (Dola za Marekani 182.2 milioni) na siyo zile za awali ambazo ni Faranga za Uswisi 180 milioni (Dola za Marekani 327.9 milioni)……. hivyo ndiyo kusema kuwa fedha hizo zinapungua,” alisema Chave na kuongeza:
“Inawezekana ni kutokana na kelele za vyombo vya habari hasa Mwananchi, pengine wenye fedha wameamua kuzihamishia kwenye benki za nchi nyingine. Sisi Serikali ya Uswisi tunapochapisha ripoti kama hizi kuonyesha jumla ya fedha kwa nchi zote duniani, haimaanishi kuwa fedha zote hizo ni haramu.”
Alisema ni makosa kwa vyombo vya habari kuendelea kuonyesha kwamba ni Uswisi pekee kunakofichwa fedha chafu, kwani zipo nchi nyingine ambako watu wa mataifa mbalimbali huweka fedha zao ambazo zimepatikana kwa njia haramu.
Benki za Uswisi zimekuwa zikidaiwa kutumika kuficha fedha chafu kutoka maeneo mbalimbali duniani kutokana na usiri wake katika kutunza taarifa za wateja.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa Kenya inaongoza kwa nchi za Afrika Mashariki kwa kuwa na kiasi kikubwa cha fedha ambacho ni karibu Sh.1.6 trilioni ikifuatiwa na Uganda Sh.376.7 bilioni, kisha Tanzania Sh.291.5 bilioni.
Rwanda ina Sh.55.1 bilioni na Burundi Sh.42.2 bilioni.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema alipoulizwa jana kuhusiana na taarifa hizo mpya alisema suala hilo la fedha zilizopo Uswisi si la kuzungumza kwenye vyombo vya habari.
“Hili jambo ni jambo nyeti sana kwa sababu kazi tuliyopewa kuchunguza suala hili bado hatujamaliza, kwa hiyo kuanza kulizungumza kwenye vyombo vya habari kunaweza kuathiri kazi hii,” alisema Jaji Werema.
Aliwaomba Watanzania kuvuta subira juu ya jambo hilo akisema kamati yake inaendelea kufuatilia na taarifa itawasilishwa.
No comments:
Post a Comment